RAIS Dk. John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana alikuwa na mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoeri Museveni mjini hapa.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema kwa kauli moja, viongozi hao walikubaliana lijengwe bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga hadi Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Museveni alimtembelea Rais Magufuli Ikulu ndogo Arusha baada ya kuwasili nchini.
Museveni yuko nchini kuhudhuria mkutano mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto leo.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo ya faragha, Dk. Magufuli alisema wamekubaliana kutekeleza mradi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,120, huku mradi huo ukitarajia kuzalisha ajira ya watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli alisema pamoja na kujengwa bomba hilo, wamekubaliana kuongeza biashara ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi.
Alisema katika mkutano unaoanza leo, yatajadiliwa maombi ya Sudan Kusini kutaka kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sudan Kusini ikiwa mwanachama wa jumuiya hiyo itakuwa na uwezo wa kufanya biashara katika eneo lenye takriban watu milioni 150, alisema.
Naye Rais Museveni alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi wake.
Alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo sasa zitakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda na kasi ya Dk. Magufuli katika shughuli za maendeleo.