23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau utalii wazungumzia BoT kufunga maduka ya kubadilisha fedha

ELIYA MBONEA Na ABRAHAM GWANDU-ARUSHA



WAKATI maduka ya kubadilishia fedha   Arusha yakiwa bado yamefungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na operesheni ya kukagua biashara hiyo juzi, wadau wa utalii jijini humo wamezungumzia hatua hiyo na maendeleo ya sekta ya utalii.

Mfanyabiashara mkubwa katika sekta ya utalii mkoani hapa Wilbert Chambulo, jana aliliambia gazeti hili kuwa  hatua ya BoT haijaathiri sekta ya utalii kwa vile  watalii wanaweza kupata huduma hiyo kwenye hoteli wanazofikia.

Chambulo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO) aliyewekeza katika Kampuni za Kibo, Tanganyika, hoteli na kambi hifadhi tofauti nchini, alisema  yeye binafsi anakubaliana na utaratibu uliotekelezwa na BoT.

“Kwa ujumla sekta ya utalii haijaathiriwa… Kama athari zipo basi walioathirika ni wale wafanyakazi wa sekta ambao ni Watanzania waliotaka kubadilisha fedha za kigeni wapate shilingi.

“Utaratibu huu, binafsi nakubaliana nao…hata kama ikiwezekana maduka yote yakafungwa na sheria ikatulazimisha kwenda kubadili fedha BoT bado itakuwa ni sahihi.

“Umeona wapi Dola ya Marekani imekuwa ya shida hapa mjini?  Nenda kwa wachuuzi wa bidhaa zinazouzwa kwa wageni…wote wanatumia dola. Hoteli za kawaida, shule mpaka migahawa ya kawaida nao wanachaji kwa Dola,” alisema.

Chambulo ambaye pia anamiliki duka la kubadilisha fedha   eneo la Mnara wa Saa jijini hapa, alisema operesheni ilichelewa kufanyika kiasi cha kuruhusu wafanyabiashara kulipisha wanunuzi wa huduma mbalimbali kwa kutumia fedha za kigeni.

“Kitu hiki ni aibu na tusi kwa sarafu yetu ya Tanzania, tofauti na jirani zetu sisi tulifanya uzembe. Ukienda Kenya au Afrika ya Kusini hawaruhusu haya mambo holela holela.

“Ukipata dola zako kabadilishe ukajieleze ulivyozipata ndipo uende kulipia huduma unayotaka, si vinginevyo,” alisema Chambulo.

Kuhusu madai kuwa BoT iliondoka na fedha za watalii kwa baadhi ya maduka, alisema madai hayo hayana ukweli kwa sababu watalii hawabebi fedha taslimu bali hulipia huduma zao moja kwa moja kupitia wakala.

“Wengine wanasema eti watalii wanahaha, huo ni uwongo, watalii watahaha vipi wakati wameshalipa huduma zao zote za safari?

Hata kama wana kiasi kidogo cha fedha taslimu wanabaki nazo ndizo wanazolipia ‘tip’ baada ya safari au ununuzi wa vitu mbalimbali na hulipa kwa fedha za kigeni,” alisema.

Nao baadhi ya madereva wa watalii  walisema pamoja na umuhimu wa hatua hiyo, bado kwao kulikuwa na usumbufu hususani walipotaka kuacha fedha za matumizi kwa familia zao.

“Hatua si mbaya isipokuwa lilileta usumbufu kwetu, madereva tuliokuwa tunasafiri na wageni. Kama unavyojua ukiwa na familia huwezi kusafiri bila kuiachia familia hela ya matumizi,” alisema Alex Murro na kuongeza:

“Tulipata usumbufu, familia zetu ziliathirika kwa sababu tulikuwa na fedha za kigeni na hapakuwa na mahali pa kubadilisha”.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara,   Viwanda na Kilimo (TCCIA), Walter Maenda, alipoulizwa kuhusu wanachama wake walioathirika na hatua hiyo,  alisema  hakuwa na taarifa yoyote inayoelezea kufungiwa maduka yao.

“Sijapata taarifa zozote kutoka BoT kwa  nini hawa wamefungiwa maduka yao, asante sana,” alisema Maeda na kukata simu.

MTANZANIA lilimtafuta kwa   simu Mkurugenzi wa BoT Tawi la Arusha, Charles Yamo kufahamu idadi kamili ya maduka yaliyokumbwa na operesheni hiyo lakini alisema bado ni mgeni  na ana wiki moja tu kwenye ofisi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles