25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Wabunge wataka wafungwa washiriki tendo la ndoa

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WABUNGE wameishauri kwa mara nyingine tena Serikali kuandaa mazingira wezeshi kwa wafungwa wenye ndoa kutembelewa na wenzi wao kisha kupata haki ya tendo la ndoa gerezani.

Wakichangia jana bungeni taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wabunge hao walidai kwamba ni muhimu kwa wafungwa kupata haki ya tendo la ndoa gerezani wakiwa na wenza wao.

KAHIGI

Mbunge wa Viti Maalum, Alfredina Kahigi (CUF), alisema wapo wafungwa waliofungwa kifungo kirefu, ikiwa hawatapata haki hiyo hata mbegu zao za uzazi zinaweza kuharibika.

GIGA

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Giga, alisema lengo la magereza ni mafunzo hata hivyo kuna vitendo vya ubakaji vinafanyika.

“Wafungwa wenye umri mdogo wamekuwa wakiwekwa pamoja na majambazi sugu na wauaji na wamekuwa wakiwalawiti.

“Vijana hao wakitoka magerezani wanakuwa wamekwisha haribika. Ni muhimu kwa wauaji na majambazi sugu wasichanganywe,” alisema.

KAMATI

Akiwasilisha taarifa ya mwaka 2018-2019 ya Kamati ya Kudumu ya Sheria na Katiba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, aliishauri Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wafungwa wenye ndoa kuwatembelea wenza wao.

 Mchengerwa alisema hatua hiyo itapunguza maambukizi ya magonjwa mbalimbali magerezani ikiwemo  Ukimwi.

“Serikali iandae na kutekeleza mpango mkakati chini ya magereza ambao utahakikisha wafungwa wenye ndoa wanawekewa mazingira yatakayohakikisha wanapata haki ya kutembelewa na wenzi wao  na kupata haki ya tendo la ndoa,” alisema.

Alisema hatua hiyo ifanyike kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na mamlaka husika ambapo hatua hiyo itasaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa magerezani ikiwemo Ukimwi.

Pia Kamati hiyo imeitaka Serikali kuongeza nguvu kudhibiti uvunjaji wa haki za makundi maalumu kama vile walemavu wa ngozi, wazee na wasichana wanaosafirishwa nje ya nchi kwa biashara haramu.

“Pia iendelee kudhibiti udhalilishwaji wa haki za watoto wa mitaani kwenye vituo vya mabasi na maeneo mengine,” alisema.

Katika kufanikisha hilo, aliiomba Serikali iendelee kuboresha bajeti ya fungu 55 la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akielezea maoni ya kamati hiyo kuhusu utoaji haki, Mchengerwa, alisema kamati imeiomba mahakama kuendelea kutekeleza kwa ufanisi utaratibu wake kwa kila Hakimu na Jaji kushughulikia na kukamilisha idadi ya mashauri kwa kipindi husika.

Alieleza kuwa Serikali inapaswa kutekeleza mkakati endelevu wa kuwajengea uwezo mawakili wa Serikali kufanya majadiliano, uandishi na uchambuzi wa mikataba ya kiuwekezaji na kutetea masilahi ya nchi.

Mwenyekiti huyo wa kamati pia alisisitiza umuhimu wa kudhibiti vyama hewa vya kuweka na kukopa (Saccos) ambavyo hukopeshwa na kusababisha fedha za Serikali kupotea.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles