25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Wabunge Ulaya waonya EPA kuwa ‘kaburi’ kwa EAC

Marie Arena
Marie Arena

KIGALI, RWANDA

MAKUBALIANO ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU), si rafiki kwa ukanda huu na ni kaburi kwa sekta changa ya viwanda iwapo yatapitishwa, wabunge wa umoja huo wameonya mwishoni mwa wiki.

Katika mahojiano na gazeti la The New Times la hapa, wabunge hao walisema makubaliano hayo ni hatarishi kwa chumi za EAC kwa vile viwanda vyake vichanga vitaweza kukabiliana na ushindani usio wa haki wa bidhaa kutoka EU.

Akipinga mkataba huo na kupongeza hatua zilizochukuliwa na viongozi wa EAC kuahirisha kuusaini, mmoja wa wabunge hao, Marie Arena, alisema EU inafahamu EPA si ya haki na ndiyo maana inaitumia zaidi Kenya mnufaika pekee wa soko la Ulaya kushinikiza wenzake wasaini.

“Nadhani ni aina ya makubaliano yasiyo na haki kwa Afrika Mashariki. Ulaya inatumia nguvu nyingi kuishinikiza Kenya kama kinara. Kenya ni nchi pekee yenye maslahi kwa makubaliano haya kwa sababu wao ni taifa lililopiga hatua. Wao wanayahitaji ili waendelee kunufaika na soko la Ulaya,” alisema.

Kulikuwa na hofu kuwa iwapo makubaliano hayo hayatasainiwa kufikia Septemba 30, 2016, Kenya ingepoteza soko la Ulaya kwa vile haiko kundi la mataifa yaliyo nyuma kimaendeleo kama wenzake EAC

Hata hivyo, kufuatia msimamo wa Tanzania kwanini haiko tayari kusaini mkataba huo, ambao iliuweka wazi wakati wa mkutano wa kilele wa wakuu wa EAC mjini Dar es Salaam hivi karibuni, EU ilikubali ombi la kusogeza tarehe ya kuyasaini hadi mapema mwaka ujao ili kutoa muda wa kuyapitia upya.

“Iwapo makubaliano yatapita, hutakuwa na jinsi, utatakiwa kupokea bidhaa zote kutoka EU bila kizuizi, kitu ambacho si ushindani wa haki. Mtapoteza kodi zenu kwa sababu haitawezekana kuzitoza bidhaa hizi. Mtapoteza viwanda vyenu vichanga kwa vile bidhaa zenu hazitaweza kushindana na za Ulaya,” alililiambia gazeti hilo.

Katika jaribio la kurekebisha hali hiyo, Arena alisema wao kama wabunge wa EU wameanzisha kampeni za kuupinga kwa vile hautoi taswira nzuri katika kujenga uhusiano mwema baina ya Afrika na Ulaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles