23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Vyombo vya habari ya kimataifa vyadai kifo cha Rais wa Burundi kimetokana na Corona

BUJUMBURA, BURUNDI 

SHIRIKA La Utangazaji la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa duru za karibu na Rais Pierre Nkurunziza zimethibitisha kuwa kiongozi huyo wa Burundi amefariki baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

BBC katika taarifa yake hiyo imeleza kuwa  inatambua kwamba vyanzo vya karibu na rais Nkurunziza vimeuthibitishia mtandao wa habari wa SOS ambao unaendeshwa na wanahabari wa Kirundi kuwa rais huyo alikumbwa na corona.

Limeandika kuwa SOS imekusanya matukio yote ya mwisho ya kiongozi huyo ambaye alidharau ukubwa na hatari wa janga la corona kwa kuruhusu kampeni na uchaguzi wa mrithi wake kinyume cha ushauri wa wataalamu wa afya.

Kwa mantiki hiyo, shirika hilo limeripoti kuwa kiongozi huyo anakuwa wa kwanza wa nchi kufariki kwa corona duniani. 

Hata hivyo, serikali ya Burundi imetangaza kuwa rais huyo alikufa kutokana na shinikizo la moyo.

Taarifa hizo zinadai kuwa muda mfupi kabla ya kifo chake, Pierre Nkurunziza aliripotiwa kuwa anatafuta msaada kutoka kwa madaktari wakubwa wa Burundi.

Inaelezwa wale ambao walikuwa karibu na marehemu kabla ya kifo chake, wamekiambia chombo cha habari cha SOS kuwa timu ya wauguzi ilikuwa haijajiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Covid 19.

Kwamba Walimfanyia vipimo mara tu alipoanza kupata dalili.

Inaelezwa  kikosi cha wataalamu wa afya walikutana haraka baada ya hali yake ya afya ilipozorota. 

Kwamba walipambana kupeleka chombo cha kupumulia katika hospitali ya Karusi alipokuwa amelazwa lakini walikuwa wamechelewa tayari.

Mmoja wa wahudumu wa afya ambaye alikuwa anamhudumia Rais Nkurunzinza ameripotiwa kuwa na virusi vya corona.

Vivyo hivyo kuna baadhi ya mawaziri walikuwa wanatibiwa ugonjwa huo wa corona katika wiki chache zilizopita.

Jenerali Evariste Ndayishimiye alishinda nafasi ya uraisi Mei 20 na alikuwa anaendelea kuonekana na rais katika mikusanyiko ya maombi na sala.

Lakini hajaonekana tena hadharani tangu rais Nkurunzinza atangazwe kuwa amefariki siku ya Jumatatu.

Tayari Mahakama imeamuru Rais huyo mteule aapishwe mara moja.

Awali rais huyo mteule  ilikuwa aapishwe mwezi Agosti .

Wakati huo huo, Tanzania, Kenya na Rwanda ambazo ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameungana kumuomboleza rais Nkurunziza aliyefariki ghafla Jumatatu wiki hii.

Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo zilizoanza jana  Jumamosi Juni 13 hadi 15,2020 na bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania inatoa heshima hiyo kwa hayati Nkurunzinza kwa kutambua kuwa alikuwa rais wa nchi jirani ambaye amekuwa na mahusiano mazuri na ushirikiano mzuri wa kindugu, kirafiki na kihistoria na Tanzania.

“Burundi ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki na rais Nkurunzinza alipenda sana jumuiya hii, pia alipenda Tanzania na alishirikiana nasi kila alipohitajika, hivyo nimeona Watanzania tuungane na ndugu zetu kuomboleza na kumkumbuka Rais Nkurunzinza ambaye aliona Tanzania kama nyumbani” alisema rais Magufuli.

Nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta, ametoa maelekezo bendera ya nchi hiyo na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupeperushwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia jana Jumamosi kwa heshima ya rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.

“Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti katika majengo yote ya umma nchini na katika balozi zote za Kenya nje ughaibuni,” taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Rais Kenyatta ilisema.

Rais Kenyatta pia ametuma rambirambi zake kwa familia ya Nkurunziza, aliyefariki Jumatatu akiwa na umri wa miaka 55.

Wakati kwa upande wake Rwanda, Rais Paul Kagame ametangaza kuwa bendera za Taifa la Rwanda pamoja na bendera za Afrika Mashariki zitapepeka nusu mlingoti kuanzia jana Juni, 13 hadi siku ambayo hayati Pierre Nkurunzinza atakapozikwa.

Marais wote wametuma salamu za rambirambi kwa warundi na familia ya marehemu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles