23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

VYETI FEKI VYATIKISA MADAKTARI, WAUGUZI MUHIMBILI

Na Veronica Romwald– Dar es Salaam

SEKESEKE la vyeti feki limewakumba madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Hatua hiyo inatokana na ripoti ya uhakiki wa watumishi wa umma nchini iliyokabidhiwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kwa Rais Dk. John Magufuli mjini Dodoma.

Katika uhakiki uliofanywa katika hospitali hiyo kubwa ya taifa, watumishi 134 wamebainika kughushi vyeti, huku wengine 38 wakibainika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mshipa (MOI).

Tangazo lilitolewa jana hospitali hapo na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru, lilitaja majina na idara zao ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Profesa Museru alisisitiza katika andiko lake kwamba watumishi walioorodheshwa katika orodha hiyo kujiondoa  wenyewe kazini kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Alisema watumishi ambao hawajaridhika na uamuzi huo, wametakiwa kukata rufaa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kabla ya tarehe hiyo na kwamba barua hizo ni lazima zipitie kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya maoni yake.

“Wakuu wa Idara na Majengo mnatakiwa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanaohusika hawaendelei kutoa huduma,” alisema Prof. Museru.

Idara ambazo zinaongoza kwa kuwa na watumishi ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi ni Kurugenzi ya Uuguzi ambapo watumishi 70 wamekumbwa na fagio hilo, ikifuatiwa na Kurugenzi ya Tiba ambao wapo watumishi 20.

Mbali na hizo Kurugenzi ya Tiba Shirikishi imebainika watumishi 14, Kurugenzi ya Tehama watumishi 11, Kurugenzi ya Upasuaji watumishi wanne, Kurugenzi ya Rasilimali Watu watumishi wawili.

Orodha hiyo inaonesha Kurugenzi ya Ufundi wapo watumishi watatu, Kurugenzi ya Fedha na Mipango watumishi watatu Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) watumishi watatu.

Inaonesha pia vitengo vinavyoripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wapo watumishi watatu na katika Taasisi ya Sayansi Shirikishi za Afya yupo mtumishi mmoja.

Aidha, katika Kurugenzi ya Tiba watumishi wote walikuwa kitengo cha magonjwa ya dharura.

Upande wa wauguzi wengi walikuwa wakifanya kazi  Wodi ya Kibasila, jengo la wazazi namba moja na na namba mbili, Mwaisela, wodi ya wagonjwa wa nje na jengo jipya la wazazi.

Akifafanua zaidi kuhusu orodha hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),  Aminiel Eligaeshi, alisema kwenye Kurugenzi ya Tiba Shirikishi watumishi hao walikuwa wakifanya kazi katika maabara kuu ya hospitali hiyo.

“Muhimbili tulikuwa jumla ya wafanyakazi 2,859 baada ya uhakiki wa vyeti vya taaluma 134 waligundulika kuwa wamegushi vyeti vyao, kwa hiyo tumebaki wafanyakazi 2,725, tumejipanga na tunaendelea kutoa huduma kama kawaida.

“Watumishi watatu waliopo katika vitengo vinavyoripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji ni wale waliokuwa wakifanya utafiti na ushauri,” alisema.

Alisema wauguzi waliotajwa katika orodha hiyo wapo ambao walikuwa wakifanya kazi katika chumba cha upasuaji.

“Madaktari waliotajwa humo walikuwa wakifanya kazi katika Kurugenzi ya Tiba,” alisema Eligaeshi.

Naye, Ofisa Habari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Patrick Mvungi,  alisema wamebainika watumishi 38 wenye vyeti vya kughushi katika taasisi hiyo.

“Wapo wauguzi 16, wasaidizi wa wodini 16, mtaalamu mfumo wa IT mmoja, mtaalamu wa vipimo vya picha mmoja, fundi umeme mmoja, mtunza kumbukumbu mmoja, ofisa ugavi mmoja na mtaalamu wa maabara mmoja,” alisema.

Wafanyakazi wajaa kwenye mbao

MTANZANIA lilishuhudia baadhi ya wafanyakazi wakiwa wamejazana kwenye mabo za matangazo wakisoma tangazo hilo lililobandikwa katika jengo la utawala.

Wengi walionekana kuwa wenye masikitiko huku wakiwaonea huruma wenzao waliotajwa katika orodha hiyo.

“Wapo ambao walikuwa wanakaribia kustaafu, wametajwa kwenye orodha, inasikitisha kwa kweli wengi nawafahamu, sijui itakuwaje na wanatakiwa kuondoka mara moja,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Akipokea ripoti hiyo ya uhakiki mjini Dodoma, Rais Magufuli aliagiza watumishi ambao wamebainika kughushi vyeti wakatwe mshahara wa mwezi uliopita na pia wafukuzwe kazi na watakaoendelea kubaki kazini hadi Mei 15 wakamatwe na kufikishwa mahakamani wafungwe jela miaka saba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles