26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Vurugu uapishaji wenyeviti wa mitaa

Pg 1ENEO la viwanja vya Anatouglou jijini Dar es Salaam, jana lilikumbwa na vurugu wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa mitatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala.
Katika vurugu hizo aliyekuwa mgombea wa CCM, Mtaa wa Kigogo Fresh B, Kata ya Pugu, Mariano Haruna, alijikuta akipata fedheha baada ya kudhalilishwa kwa kuvurumishiwa matusi, kukunjwa na kuchaniwa shati lake.
Haruna, alifanyiwa vitendo hivyo na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliofika kwa lengo la kushuhudia uapishaji huo.
Vurugu hizo, zilizosababisha mvutano mkubwa kati ya wasimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Ilala na wananchi, zilianza taratibu wakati washindi wa nafasi ya uenyekiti na wanakamati wa mitaa yao walipokuwa nje ya ukumbi huo wakisubiri kuapishwa.
Kadiri majina ya wenyeviti hao yalivyokuwa yakiitwa kwa ajili ya kuingia ndani kuapishwa, ndivyo presha ya wafuasi wa vyama mbalimbali waliofika kushuhudia shughuli hiyo ilivyozidi kupanda.
Hali ilibadilika baada ya jina la aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Kigogo Fresh B, Haruna kuitwa, badala ya yule wa Chadema, Patricia Mwamakula ambaye wananchi walimtaka.
Wakati Haruana akielekea kuingia ndani, wananchi walimzuia na kumvuta nje, hatua iliyowafanya wasimamizi wa uchaguzi kwa kushirikiana na polisi nao kumvuta huyo kuingia ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, baada ya mabishano na mvutano huo uliodumu kwa dakika kadhaa, wananchi waliwashinda askari hao na wasimamizi wa uchaguzi na kufanikiwa kumtoa nje.
Baada ya kutolewa nje, askari na wasimamizi walimgeuka na kumwamuru aondoke kwa ridhaa yake hadi mkurugenzi atakapomwita tena.
Baada ya kufika nje, wananchi walitumia mwanya huo kuanza kumsukuma na kumchania shati lake, huku wakimtolea maneno ya kashfa na lugha chafu.
Wananchi hao, walidai mgombea huyo awali alikubali kushindwa, lakini amekuwa akijitokeza kutokana na shinikizo la viongozi wa juu wa CCM.
“Mkurugenzi na baadhi ya viongozi wa CCM, wamekuwa wakimbeba kwani wanaona aibu chama chao kimeshindwa maeneo mengi, lakini sisi kama wananchi ni haki yetu kumchagua kiongozi tunayemtaka na siyo Serikali kutuchagulia.
“Kama wanataka kutuchagulia viongozi basi wataongozwa wao siyo sisi, tunaamini mgombea wetu ataapishwa na isipokuwa hivyo, tutafanya kama wenzetu wa Migombani walivyomwapisha mwenyekiti wao,” alisema Khalfani Mchopanga.
Baada ya kadhia hiyo, Haruna alijitetea kuwa yeye alipata taarifa za kuapishwa kupitia kwa ofisa mtendaji wake wa kata aliyemtaja kwa jina moja la Nyange.
Alisema usiku wa kuamkia jana, mtendaji alimpigia simu na kumtaarifu kuwa amepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Ilala, Isaya Mngulumi, kuwa asubuhi afike ukumbi wa Anatouglou kwa ajili ya kuapishwa.
“Mimi nilipigiwa simu usiku na mtendaji wangu, nimetekeleza agizo, nimekuja ili niapishwe nikawatumikie wananchi wangu na jina langu kweli nimelikuta, na hata nyie waandishi mashahidi kwani mmemsikia msimamizi wa uchaguzi akiniita.
“Lakini nawashangaa hawa Chadema wananishambulia na kunidhalilisha kiasi hiki mbele ya watu. Hata hivyo, kwa sasa sina cha kusema ila chama ndiyo kitatoa tamko la mwisho kufuatia hali hii kwani ni sehemu ya siasa,” alisema Haruna.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa Chadema, Mwamakula, alisema halmashauri haijafanya haki kwani hakuna aliyewahi kutangazwa mshindi katika kata hiyo, kutokana na uchaguzi kuharibika.
Alisema taarifa za kuapishwa alizipata usiku kupitia kwa wagombea wengine wa chama chake ambao walishaapishwa awali na ndipo alipoamua kufika ili kutetea haki yake.
Akizungumzia hali hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu, alisema hiyo ni hali ya kisiasa na siyo kitu kigeni kutokea.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamelazimika kuwaapisha wenyeviti wawili badala ya watatu kama ilivyopangwa, pamoja na wanakamati 15 kutoka katika mitaa mitatu.
Wenyeviti walioapishwa ni Japhet Kembo (Chadema) kutoka Mtaa wa Migombani, Kata ya Segerea na Ubaya Chuma (CCM) kutoka Kata ya Minazi Mirefu.
Kuapishwa kwa Kembo kumeweka historia mpya, baada ya kuapishwa mara mbili ndani ya wiki moja.
Mwenyekiti huyo, ambaye awali aliapishwa na wakili wa kujitegemea, Idd Msawanga, aliyekodiwa na wananchi, Januari 19, mwaka huu, ameapishwa kwa mara ya pili na Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, Hella Mlimanazi.
Katika hatua nyingine, vyama vya NCCR-Mageuzi na CCM kutoka Mtaa wa Migombani, vimepinga kitendo cha kuapishwa kwa Kembo.
Akizungumza hali hiyo, aliyekuwa mgombea wa CCM, Uyeka Rumbyambya, alidai uapishwaji huo ni batili kwani kata yao haikufanya uchaguzi wa marudio kama ilivyoamriwa awali na Mkurugenzi wa Manispaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles