23.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Vituo vya mafuta wekeni mabango ya bei-Ewura

Jacquiline Mrisho- MAELEZO

VITUO vya mafuta nchini vimekumbushwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili kuepusha usumbufu unaojitokeza kwa wateja na kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Nzinyangwa Mchany,  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu bei kikomo za mafuta aina ya petroli zilizoanza kutumika jana.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” alisema Mchany.

Alisema kuwa mabango hayo yanatakiwa kuonesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika ili wateja waweze kuwa na uwanja mpana wa kuchagua wapi pa kununua.

Aidha, Mchany ametoa rai kwa wateja kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

Kwa upande mwingine wauzaji wa mafuta ya petroli wamekumbushwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na wanunuzi wametakiwa kuhakikisha wanapokea stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Alisema stakabadhi hizo za malipo zitatumika kudhibiti watoa huduma wasio waaminifu pale ambapo wanunuzi wa mafuta watakuwa na malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, pia stakabadhi hizo zitasaidia kurahishisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na nishati mafuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles