24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya Frederick Sumaye, Mary Nagu ngoma nzito

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye

NA MWANDISHI WETU, HANANG’

MGOGORO wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kati ya Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu, unaendelea kufukuta.

Hatua hiyo inatokana na viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Hanang’ kugawanyika kuhusu uteuzi wa Sumaye kuchukua nafasi ya Nagu kuwa kamanda wa UVCCM wa wilaya hiyo.

Wakizungumza juzi, vijana hao walisema viongozi wa UVCCM wilaya hiyo walifanya kosa kwa kupeleka jina moja la Sumaye badala ya majina matatu likiwamo la mbunge wa jimbo hilo, Dk. Mary Nagu na Charles Gapchojiga.

Vijana hao walidai kuwa kupitia kikao chao cha Baraza la UVCCM Wilaya, wanapinga uteuzi huo wa Sumaye kuwa kamanda wa UVCCM wilaya kwani utaratibu haukufuatwa kwa kupendekezwa jina moja badala ya majina matatu.

Baadhi ya wajumbe, Katibu wa UVCCM Kata ya Masqaroda, Shamimu Ally, Katibu UVCCM Kata ya Gidahababieg, Theresia Mahuka na Mwenyekiti UVCCM Kata ya Masakta, Emmanuel Manase, walidai kuwa uteuzi huo si halali kwani haukufuata utaratibu.

Katibu wa UVCCM Kata ya Measkron, Faustin Anselim, alisema wajumbe wanne kati ya sita wa Baraza la Utekelezaji UVCCM wilaya, walipitisha jina la Sumaye peke yake na kuacha majina mengine ya Gapchojiga na Dk. Nagu.

“Hata Mwenyekiti wa Chipukizi wa wilaya, ambaye ni mjumbe wa baraza hilo hakuwapo kupitisha jina hilo, hivyo sisi bado tunamtambua kamanda wa sasa Dk. Nagu, kuwa bado ni kamanda wa UVCCM wilayani humu,” alisema Anselim.

Alisema wao hawamtambui Sumaye kuwa kamanda wao kwani taratibu za kupitisha jina lake hazikufuatwa, hivyo wanamtambua Dk. Nagu, ambaye bado hajamaliza muda wake, ndiye Kamanda wa UVCCM Wilaya ya Hanang’.

SUMAYE ANENA

Akijibu madai hayo, Sumaye alisema alishapatiwa barua ya kuteuliwa kwake kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na anachosubiri hivi sasa ni kutawazwa kwenye nafasi hiyo ya ulezi wa vijana Oktoba 18, mwaka huu.

“Mchakato huo ulifanyika kwa njia ya halali kwani ulianza ngazi ya wilaya kwa UVCCM Wilaya ya Hanang’ kupendekeza jina langu lililopelekwa UVCCM mkoa, ambao nao walilipeleka UVCCM taifa, nao walipitisha jina hilo,” alisema Sumaye.

Alisema endapo kuna mtu ana wasiwasi kuhusu hilo waulizwe viongozi wa CCM mkoa au UVCCM mkoa wanaweza kujibu kwani akizungumza yeye ataonekana kwamba anajitetea mwenyewe.

Hata hivyo, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Ezekiel Mollel, alisema mchakato wa kupitisha jina la Sumaye kuwa kamanda wa UVCCM wilayani Hanang’ ulifuata utaratibu wote, hivyo amepatikana kihalali.

Mollel alisema walipata majina matano ya watu ambao walipendekezwa na UVCCM Hanang’ kuteuliwa kuwa kamanda na wao wakapitisha majina matatu kwenda taifa, ambao wamepitisha jina moja la Sumaye kuwa kamanda.

Vigogo hao wa CCM wamekuwa na tofauti kufikia hata kupingana hadharani, huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kujihusisha na tuhuma za rushwa ndani ya chama hicho tawala.

Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu na Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), waliingia katika mgongano, na mgogoro huu ulishika kasi mwaka jana wakati wa uchaguzi wa kumpata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, kupitia Wilaya ya Hanang’.

Katika uchaguzi huo, Nagu alimshinda Sumaye kwa kura, na baadaye, waziri huyo mstaafu aliibuka na kueleza kuwa kushindwa kwake kulitokana na rushwa iliyokithiri kwenye uchaguzi huo, ikiwa inasukumwa na makada kadhaa wa CCM.

Hata hivyo katika ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mapema mwaka huu wilayani humo, viongozi hao walitangaza kutokuwa na uhamasa wa kisiasa huku kila mmoja akiomba ushirikiano kutoka kwa mwenzake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles