24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Viungo walivyoamua mbabe Ngao ya Jamii

Mohammed Kassara -Dar es salaam

PAZIA la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 limefunguliwa rasmi, baada ya kuchezwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulimazika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya  Azam.

Simba imetwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1 katika mchezo wa Ngao ya Jamii wa msimu uliopita uliochezwa Agosti 19, mwaka jana.

Mchezo wa Azam na Simba ulikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na staili za uchezaji za timu hizo, wachezaji kujuana na mbinu za makocha wa pande zote mbili.

Licha ya kandanda safi lililooneshwa na timu zote mbili, kingine kilichoongeza uhondo wa mchezo huo ni kitendo cha kufungwa mabao mengi, hiyo inaonyesha ulikuwa mchezo wa wazi kwa pande zote.

Hata hivyo, mchezo huo kwa kiasi kikubwa ulichezwa zaidi katikati ya uwanja na timu iliyoshinda vita ya eneo la kiungo ndiyo iliyoibuka na ushindi.

Kinachothibitisha kwamba, ulikuwa mchezo uliotawaliwa na vita ya katikati ya uwanja ni takwimu za mabao yaliyofungwa.

Katika mabao sita yaliyopatikana katika mchezo huo, matano yalifungwa na wachezaji wa eneo la kiungo.

Viungo wa Simba, Sharaf Eldin Shiboub alifunga mabao mawili , Clatous Chama na Francis Kahata walifunga bao moja kila mMoja, huku kiungo wa Azam, Frank Domayo akifunga.

Mshambuliaji Shabani Chilunda ndiye mchezaji pekee wa eneo hilo
 aliyefanikiwa kufunga bao katika mchezo huo.

Ni kawaida kwa mechi zinazoikutanisha Simba na Azam kuwa na shughuli kubwa hasa kwenye eneo hilo, na mara nyingi timu itakayotawala katikati ndiyo uibuka kidedea.

Katika mchezo huo, timu zote zilitumia mfumo unashabihiana wa 4:4:2,, hata hivyo kila upande ulianza na viungo watatu wa asili katika eneo la katikati.

Lakini mifumo hiyo ilikuwa inabadilika kulingana na mazingira, Simba ilikuwa ikihama  kutoka 4:4:2 kwenda 4:3:3, wanapokwenda kushambulia na pale wanapokuwa hawana mpira.

Azam ilikuwa ikibadilika kutoka 4:4:2 kwenda 3:5:2 inapokuwa haina mpira, hiyo ilikuwa inawafanya waweze kuwa na watu wengi katikati, lengo likiwa kuifanya Simba ishindwe kupitisha mipira.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alianza na Jonas Mkude, Shiboub na Hassan Dilunga, huku kocha wa Azam Etiene Ndayiragije akianza na Frank Domayo, Emmanuel Mvuyekure na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mkude alicheza kiungo cha ulinzi akisaidiana na Shiboub, huku Dilunga akitokea pembeni kidogo na kuingia kati kuongeza nguvu katika eneo hilo.

Azam kwa upande wao, Domayo ndiye aliyekuwa na jukumu la kucheza chini, akishirikiana na Mvuyekure, huku Sure Boy akicheza kama kiungo huru.

Hata hivyo, Simba ndiyo iliyonufaika na uwepo wa viungo hao kutokana na kumiliki mchezo kwa sehemu kubwa na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Viungo wa Simba waliwazidi wapinzani wao katika usahihi wa kupiga pasi kwani nyingi zilifika kwa walengwa tofauti na Azam ambayo  nyingi zilinaswa.

Shiboub alikuwa mhimili mkuu wa eneo hilo mkutokana na uwezo wake wa kucheza katika maeneo yote (box to box), kwani alikuwa na  uwezo mzuri wa kubaka, kumiliki mpira na kupiga pasi sahihi, lakini pia alikuwapo kwenye eneo la kushambulia.

Dilunga naye, alikuwa na faida ya kutokea pembeni na kuukata uwanja kuingia ndani, akipiga pasi za kupenyeza kuelekea kwa Meddie Kagere na John Bocco.

Kutokea pembeni kulimfanya awe na faida mbili, timu inapokuwa haina mpira anakuwa pembeni kumdhibiti beki wa kushoto wa Azam, Nicolas Wadada asikimbia kwenda kupiga krosi za hatari.

Pili timu inapokuwa na mpira alikuwa katikati, hivyo kumpa fursa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ,kukimbia eneo kulia na kupiga pasi au krosi.

Viungo wa Azam walishindwa kumudu kasi ya mchezo kutokana na ubora waliokuwa nao wachezaji wa Simba waliocheza eneo hilo, badala yake muda mwingi walijikuta wakiutumia kukaba.

Licha ya uhodari mkubwa wa Sure Boy, lakini mara nyingi pasi zake za mwisho  kuelekea kwa washambualiji zilishindwa kupenya katika ukuta wa Simba.

Azam ilikuwa na mtu mwenye kasi sana, Joseph Mahundi ambaye alitegemewa kwa uwezo wake wa kutembea na mpira ungekuwa mwiba mchungu kwenye safu ya ulinzi ya Simba.

Hata hivyo, Mahundi alishindwa kutamba kutokana na kukosa nafasi ya kukimbia na mpira ili kupiga pasi au mashuti hatari ambayo yanaweza kuzaa matunda.

Mechi ilizidi kuwa ngumu kwa Azam pale Simba ilipokuwa na viungo wanne katikati, baada ya John Bocco kuumia na kutoka kisha kuingia Clatous Chama,eneo hilo lilizidi kuimarika na kutawala mpira wanavyotaka.

Mtazamo wa Mayay

Baada ya mchezo huo, MTANZANIA lilimtafuta mchambuzi wa soka nchini na mchezaji wa zamani wa Yanga na timu Taifa Tanzania ‘Taifa Stars ambaye alisema Azam ilifanya kosa kubwa kushindana na Simba katikati ya uwanja.

Alimshangaa Ndayiragije kwa uamuzi wake wa kucheza kwa kufunguka mbele ya Simba, huku akijua ubora wa wapinzani wake hao hasa eneo la kiungo.

“Kosa kubwa alilolifanya kocha wa Azam ni kushindana na Simba, siyo dhambi kama angeingia kwa staili ya kupaki basi, wapinzani wake walikuwa na muunganiko mzuri kuliko kikosi chake, hivyo lilikuwa ni suala la kuwaheshimu tu.

“Viungo wa Simba walikuwa na muunganiko mzuri, pia walikuwa na usahihi mkubwa wa pasi ukilinganisha na Azam, mtu pekee ambaye alikuwa kwenye ubora ni Sure Boy, lakini wengine walikuwa chini sana,”alisema.

Mayay alisema Ndayiragije alipaswa kuanza na viungo wawili wakabaji chini na siyo kumuanzisha Domayo na Mvuyekure ambao wote walikuwa wakisogea juu na kushambulia.

“Mchezo huo umeonyesha Ndayiragije bado ana kazi nzito ya kufanya ili kupata kikosi cha kwanza, ukiangalia kikosi chake kimekuwa kikibadilika mara kwa mara, hiyo ni shida nyingine, lazima apate ufumbuzi mapema,”alisema Mayay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles