Derrick Milton, Simiyu
Zaidi ya viongozi 100 wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) wilayani Maswa, Mkoa wa Simiyu, wamekamatwa na Jeshi la Polisi wilayani humo fedha kwa madai ya kutafuna zaidi ya Sh milioni 242 za kampuni za kununua pamba.
Viongozi hao ni kutoka katika vyama vya msingi 52, kati ya 120 vilivyoko Wilayani humo, ambapo wanadaiwa kukopeshana kiasi hicho cha fedha huku baadhi yao wakidaiwa kukimbia kusikojulikana.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe, ndiye aliyetoa amri ya kukamatwa ambapo pia ameagiza kusimamishwa kazi Ofisa Ushirika wa Wilaya hiyo, George Budodi, kutokana na kutotimiza wajibu wake wa kubaini ubadhirifu huo mapema.
“Huu ni uhakiki wa awali ambao tumeufanya, bado tunaendelea, lakini matokeo ya awali yanaonyesha kwamba Kampuni za kununua pamba zinadai Sh milioni 317 na senti kadhaa na sio Sh milioni 461 kama zilivyowasilishwa awali,” amesema Dk. Shekalaghe.