26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi taasisi za dini wacharuka

GWAJIMAEsther Mbussi na Grace Shitundu, Dar es Salaam
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amezua jambo baada ya kuhusishwa na kauli ya Serikali kuhusu kuzifungia taasisi mbalimbali zikiwamo za kidini.
Hatua ya Askofu Gwajima kuziponza taasisi hizo, imetafsiriwa na viongozi wa dini siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kutangaza tishio la kuzifuta taasisi hizo.
Kutokana na hatua hiyo, viongozi wa dini wamemtaka Waziri Chikawe kufuta kauli yake ambayo wamesema ina vimelea vya mgogoro uliopo baina ya Serikali, Askofu Gwajima na tamko lililotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) kuwataka wananchi kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Juzi, Waziri Chikawe alisema sababu kubwa ya kutaka kuzifuta taasisi hizo ni kujihusisha na kazi nyingine kinyume cha sheria za vyama vya kijamii sura ya 337 na kanuni zake zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.

Askofu Mwamalanga
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini, Mchungaji William Mwamalanga, aliliambia MTANZANIA kuwa kauli ya Serikali imejaa vitisho kwa raia wake na inaonekana wazi inataka kuwatenganisha na Serikali yao.
Alisema tamko hilo limekuja baada ya mlolongo kati ya Serikali na Askofu Gwajima ambapo alimshauri waziri kuziita taasisi zote kabla ya uamuzi wa kuzifuta.
“Nafikiri jambo hili lina uhusiano na mgogoro kati ya wizara na Askofu Gwajima, cha kustaajabisha kama kulikuwa na tofauti hizo kabla kwa nini walimhifadhi hadi sasa.
“Wangetatua mambo yao kuliko kutumia kivuli cha Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhana Kardinali Polycarp Pengo kudhalilishwa… hapa Serikali inataka kuigawa jamii,” alisema Mchungaji Mwamalanga.
Alisema kauli ya Waziri Chikawe ina nia ya kuiondoa Serikali mioyoni mwa wananchi wake.
Mchungaji Mwamalanga alisema wakati huu ambao nchi inaelekea uchaguzi mkuu, wasingependa kuona makundi ya hasira yanazaliwa.
Alisema matamko yoyote yanapaswa kuwa ya kujenga na si kila kukicha kuzalisha mitafaruku.

Askofu Mgulu
Mchungaji wa Kanisa la Christian Ministry Fellowship, Askofu Dk. Mgulu Killimba, naye alisema inawezekana chanzo cha kauli hiyo ni Askofu Gwajima na tamko la TCF hatua inayosababisha Serikali kutaka kushusha rungu.
Alisema taasisi za dini zipo kuikosoa Serikali kwa nia ya kujenga, ingawa Serikali sasa inataka kuwanyamazisha Watanzania jambo ambalo si zuri.
“Jukwaa limeleta msimamo wake kuhusu Katiba Inayopendekezwa, wanasema wengi wape, kama jukwaa tulitoa msimamo wetu huenda tumeenda kinyume na matarajio yao, mtu anayekupinga asitazamwe kama adui, tusitumie njia hizo kuwagawa Watanzania ambao wameelimika kwa sasa.
“Taasisi za dini zipo kwa mujibu wa sheria, unapozifungia maana yake zisifanye kazi kwa uhuru, labda waunde sheria mpya.
“Kuna mambo mengi ya Serikali kushughulikia, lakini inalegalega kwa mfano tatizo la rushwa liko kila mahali unapokwenda, ebu waanze na hili kwanza,” alisema.
Kuhusu kupeleka ‘return’, alisema hawana ruzuku kama vyama vya siasa, lakini kama wanataka kukaguliwa wanawakaribisha.

Askofu Niwemugizi
Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi, alisema tamko la kuzifungia taasisi za dini zitakazotoa maelekezo kwa waumini wao juu Katiba Inayopendekezwa ni kwenda kinyume na sheria ya kura ya maoni.
Askofu Niwemugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), alisema sheria ya kura ya maoni inaeleza wazi kuwa kutakuwa na makundi mawili yatakayoipigia kampeni Katiba Inayopendekezwa.
Alisema kwa hali hiyo, Serikali itarajie upinzani mkubwa kutoka kwenye taasisi hizo kwani wanajua kuwa sheria inawaruhusu.
Hata hivyo, alisema anashukuru Serikali kutoa kauli hiyo kwani itasaidia wao kuanza kujipanga vizuri.

Jukwaa la Katiba
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda, alisema tamko hilo ni vitisho baada ya kuona joto la mwamko wa wananchi limepanda.
Alisema Serikali inajaribu kutisha wananchi ili wakubaliane na kila jambo ambalo wanalitaka viongozi wa juu.
“Tukiangalia kwa kina jambo la Katiba, wananchi wanapaswa kuelewa kuwa kura ya ndiyo haimilikiwi na Serikali, bali kura ya ndiyo au hapana ni uamuzi wa wananchi wenyewe,” alisema.
Kuhusu taasisi za dini kujihusisha na siasa, alisema inapaswa Serikali na wananchi waelewe ni siasa ya aina gani inayozungumziwa, kwani masuala ya Katiba ni ya wananchi wote, si ya vyama vya siasa tu.

Kituo cha Sheria
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema ameshangazwa na Waziri Chikawe ambaye kitaaluma ni mwanasheria kutangaza hatua hiyo.
“Sioni mantiki kubwa ya kutaka kuzifungia taasisi hizi, zaidi ya kutaka kukomoana na kutishia ili taasisi zinazoeleza ukweli wa mambo zikae kimya,” alisema Dk. Kijo-Bisimba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles