23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

ACT ipo tayari kushirikiana na Ukawa

zito_kabweNa Bakari Kimwanga, Singida
CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kimesema kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kubomoa mfumo unaowanyonya wananchi
Kutokana na hali hiyo, kimewahakikishia Watanzania kuwa ujio wa chama hicho ni wa kuleta mageuzi ya kweli kwa taifa badala ya porojo kama vyama vingine vinavyofanya.
Akihutubia wananchi jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ukombozi, mjini hapa, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa hivi sasa Taifa limekuwa na shauku ya ACT kushirikiana na vyama vingine kama njia ya kufanikisha malengo ya kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madarakani.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni lazima Taifa lijengwe upya kwa matumaini, ikiwamo kuhakikisha vyama vinakuwa na ushirikiano wa dhati utakaoleta mageuzi ya kimfumo na uchumi kwa Watanzania wote.
“Kumekuwa na shauku ya wananchi kwa sisi kushirikiana na vyama vingine vya siasa ili kufanikisha malengo yetu ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuubomoa mfumo wa uchumi unaonyonya wananchi. Msimamo wetu upo wazi na tumeueleza mara kadhaa.
“ACT- Wazalendo tunaunga mkono juhudi zozote za kushirikiana kwa vyama na hili linathibitishwa na jina letu, Alliance na msimamo wetu kuhusu mabadiliko ya Katiba. Kubwa tunataka ushirikiano utakaonufaisha wananchi na si ushirikiano wa kugawana nafasi za uongozi,” alisema Zitto.
Kiongozi huyo wa ACT alisema chama chao hakina tatizo na kipo tayari kushirikiana na chama chochote kilichokuwa tayari kushirikiana nao, ikiwemo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kuunganisha nguvu kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema umoja huo ni lazima uwe na malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, wenye mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi wote na wenye kutokomeza umasikini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles