29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi Bavicha kufikishwa kortini leo

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

VIONGOZI wakuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) waliokamatwa juzi kwa tuhuma za kuikashfu Serikali, watafikishwa mahakamani leo mjini hapa.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alitoa taarifa hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari.

Aliwataja watakaofikishwa mahakamani kuwa ni Mwenyekiti wa   Bavicha, Patrobas Katambi, Katibu wa baraza hilo, Julius Mwita, Mwenyekiti wa Baraza hilo Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mratibu wa Uenezi na Uhamasishaji wa Bavicha, Edward Simbeye.

Kuhusu watu wanaopanga kuvuruga mkutano mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu mjini Dodoma, Kamanda Mambosasa alisema watu hao watachukuliwa hatua kwa kuwa Jeshi la Polisi limekwisha kujiandaa kukabiliana nao.

“Kuna viashiria vya kutokea vurugu katika mkutano huo, hivyo nawataka wale watakaothubutu kufika Dodoma kwa lengo la kufanya vurugu  cha moto watakiona.

“Nawaambia tena, watu hao hawataweza kutekeleza vitendo,  hivyo tutahakikisha mkutano unafanyika kwa amani na kumalizika kwa amani. Ole wao waliopanga kufanya vurugu,” alisema Kamanda Mambosasa.

Aliwataka wamiliki wa nyumba za wageni kutokuwa tayari kuwahifadhi watu wanaofika mjini Dodoma kwa ajili ya kuvuruga mkutano huo kwa kuwa wakigundulika watachukuliwa hatua.

“Wakati tukiwaonya wamiliki wa nyumba binafsi, wananchi waelewe kwamba, tayari tuna taarifa za uwepo wa watu waliopanga kufikia kwenye nyumba za watu binafsi badala za kulala kwenye nyumba za wageni.

“Kwa hiyo, yeyote atakayebainika akiwahifadhi watu hao, ajue atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa   kuwahifadhi watu hao,” alionya.

Mwishoni mwa wiki, viongozi hao wa Bavicha walikamatwa mjini Dodoma kwa tuhuma za kuikashfu Serikali kwa kuvaa mavazi yenye ujumbe wa uchochezi.

Ujumbe huo uliokuwa kwenye fulana ulisomeka kama hivi: ‘Tuungane tuukatae udikteta uchwara’ na mwingine ulisema, ‘Mwalimu Nyerere demokrasia inanyongwa’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles