25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

‘Vijana wana kila sababu ya kumuunga mkono JPM 2020’

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

JUKWAA la vijana wa Tanzania mpya limesema vijana wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu 2020 kutokana na utendaji kazi wake kuwagusa wananchi, hasa wao.

Akizungumza jana jijini hapa na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Taifa, Ramadhan Magambo, alisema wanaamini Rais Magufuli atapitishwa na chama chake (CCM), hivyo watamuunga mkono.

“Kwa miaka mingi vijana tumekuwa tukitumika kama daraja, zile zama za vijana kuonekana tuna umuhimu kwa kipindi fulani zimepita, vijana tupo zaidi ya asilimia 60 nchini, tunaamini vijana pekee tunatosha kusema tunayemtaka,” alisema Magambo.

Alisema vijana bila kujali itikadi zao wataenda kwa pamoja kumuunga mkono Rais Magufuli kama Watanzania ambao hawafungamani na chama chochote.

“Lengo sisi kama vijana tunataka kumpa zawadi Rais Magufuli katika Uchaguzi Mkuu, hakuna Mtanzania asiyejua mema yaliyofanywa na Rais Magufuli, tutampigia kura za kishindo, na tunataka kuandika historia ya taifa letu kwamba ndio rais atakayekuwa amechaguliwa kwa kishindo,” alisema Magambo.

Alisema watapita nchi nzima kuwafikia Watanzania ili wamchague Rais Magufuli katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa hilo, Frank Chirare, alisema Rais Magufuli ameweza kupambana na vitendo vya rushwa na hivi sasa wananchi wanahudumiwa bila kutoa chochote.

Alisema amefanya mengi ikiwemo kuongeza mapato ya nchi na hivyo kuiwezesha kuingia uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025.

“Kwa hiyo kwa hayo tuliyoyapima kwenye utendaji wake, na kiongozi tunayemtaka tumeshamuona kupitia uwajibikaji wake, Rais Magufuli amekaa ndani na kujishughulisha na mambo ya nchi yetu, hakuwa mtu wa kusafiri,” alisema Chirare.

Alisema wanaamini Rais Magufuli anaweza kuwafikisha kule wanapotaka kutokana na utendaji kazi wake.

“Tutaenda mbele na Rais Magufuli na kuhakikisha anarudi tena Ikulu ili kuiona Tanzania bora zaidi na kufikia uchumi wa juu zaidi,” alisema Chirare.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles