Shilole avunja ndoa kisa ukatili wa mumewe

0
2936

CHRISTOPHER MSEKENA

LICHA ya kuonekana kuwa kwenye ndoa yenye furaha, staa wa Bongo Fleva na mjasiliamali, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ameweka wazi ukatili mkubwa anaofanyiwa na mumewe, Ashrafu Sadiki maarufu kama Uchebe kwa miaka kadhaa sasa.

Shilole ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili wanaofanyiwa wanawake kwenye ndoa zao, amewaomba radhi mashabiki kwa kutetea wengine huku yeye mwenyewe akichezea kichapo kila uchwao kutoka kwa Uchebe.

Akizungumzia ukatili anaofanyiwa na mumewe, Shilole alisema Uchebe amekuwa akimpiga na kuondoka zake bila kujali anaendeleaje huku akibaki kuuguzwa na watu baki, ukatili uliofanya ndoa yao ikose uhai na furaha.

“Watoto waniangalia kama baba na mama, leo nikubali kufa na kuacha wanangu barabarani, sitaweza, Uchebe ni mwanaume niliyempenda, nilimvumilia kwa madhaifu yote, nikampa kila kitu kama vile utu wangu, mali zangu na hata palipotakiwa kumuendeleza asimame mwenyewe nilifanya kwakuwa nilijua tuko pamoja lakini  hilo halikuwahi kuzuia vipigo, dharau na usaliti,” alisema Shilole.

Akizungumzia sababu za kupigwa vibaya na kuumizwa siku mbili zilizopita Shilole alisema: “Baada ya kutoka sabasaba kutafutia watoto wangu na kumtafutia yeye nilipigwa sana na sababu za kupigwa ni migogoro midogo ya kawaida ambayo ipo kwenye kila ndoa, sio kwamba amenifumania au mambo yanayoshindwa kuzungumzika, hapana tena namuheshimu sana lakini ‘solution’ aliyoiona ni kunipiga kinyama bila huruma, tena kwa kunishtua na ngumi nikiwa usingizini,” alisema.

Aidha Shilole ambaye alifunga ndoa ya Uchebe, Desemba 7, 2017 jijini Dar es Salaam alitangaza kuvunja ndoa hiyo akisema: “Maisha yangu ni maisha ya watu kwa kiasi kikubwa, jamii inanitazama kama mfano, nimefika mwisho na kuanzia sasa naomba nisitambulike kama mke wa Uchebe ila Mama aliyeamua kuweka maslahi ya watoto wake mbele na kuamua kuwa mwenyewe kwa usalama na furaha yake.

Katika kutaka kuthibista hilo, MTANZANIA lilimtafuta Uchebe kwa namba yake inayoishia 83, simu iliita bil haikupokewa na baadaye haikupatikana kabisa mpaka tunaingia mitamboni.

Tukio hilo ambalo Shilole ameamua kulitoa kupitia ukurasa wake wa Instagram, limewaibua mastaa kibao kama vile Flaviana Matata, Nay wa Mitego, Lulu Diva, Jacqueline Wolper, Riyama Ally, Linex, Rose Ndauka, Ben Pol, Aunt Ezekiel, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Nandy, Kajala, Marioo, Rosa Ree, Aika, Batuli na wengineo wengi waliompa pole na kupinga ukatili huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here