VIAZILISHE DAWA UMASIKINI KIPATO, AFYA PEMBA

0
876

Na JOSEPH LINO,

UJIO wa mbegu ya viazilishe iliyoboreshwa umeleta mabadiliko ya kimtazamo kwa kilimo cha viazi kwa watu wengi, hasa wakulima wa kawaida.

Kilimo cha viazi lishe kimeanza kunufaisha wakulima wa vijijini, hasa katika kuinua kipato na afya katika upande wa kuongeza virutubisho, hasa kwa watoto wenye ukosefu wa vitamini A.

Hili limeonekana katika kilimo cha viazi lishe visiwani Zanzibar, ambako kuna uhitaji mkubwa wa mbegu iliyoboreshwa ya viazi lishe.

Mradi wa viazilishe unaojulikana kama Fast Track na kusimamiwa na Wizara ya Kilimo ya Zanzibar umeweza kuwafikia wazazi wengi kupitia watoto wao walioko shule za msingi.

Kilimo cha viazilishe katika visiwa vya Pemba na Unguja huko Zanzibar wanalima kwa ajili ya biashara na matumizi  ya chakula kama lishe.

Khamis Bakari, mkazi wa Bandari Kuu, Kata ya Kifundi Wilaya ya Micheweni, Pemba, ni miongoni mwa wanaonufaika na mradi wa Fast Track kama mkulima, mzalishaji na msambazaji wa mbegu za viazilishe.

Bakari, zao hili amelifanya kuwa kilimo biashara baada ya kupata fursa ya kipekee kwa kujikita katika kilimo cha viazilishe kama njia ya kuzalisha kipato na chakula.

Anasema kilimo cha viazi lishe ni kama ilivyo kwa viazi vingine, ni rahisi ikilinganishwa  na aina viazi vya kawaida.

Mbegu ya viazilishe ambayo Bakari hutumia imeboreshwa na kufanyiwa utafiti na  wataalamu kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Zanzibar, ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo.

Kwa mujibu wa mkulima huyu, viazi lishe hutumia muda wa kipindi cha takribani miezi mitatu toka kupandwa hadi kuvunwa.

Mwanakijiji huyu alikuwa miongoni mwa waliochaguliwa kupata mbegu hizo kutoka taasisi ya utafiti ya Zanzibar.

Ilikuwa mwaka jana mwezi Septemba, alipokea mbegu ya viazilishe aina tatu, ambazo ni Kobede, Mataya na Mayai.

“Nilitumia mbegu bora hiyo kupanda takribani ekari moja, ingawa ilikuwa kipindi kigumu lakini matokeo yake yalikuwa ya kunufaisha baada kuzalisha mbegu za kutosha,” anasema.

Kama mradi wa Fast Track unavyoeleza kuwa mzalishaji anatakiwa kusambaza kwa watu wengine ambapo alifanikiwa kuwagawia wanakijiji wenzake zaidi ya 25.

Pia alitoa mbegu bora hiyo kwa Idara ya Kilimo ya Matangatuani na Wete visiwani Pemba.

“Niliweza kuuza mbegu hizo ambazo zinahitaji kwa kiasi kikubwa wilaya hii ya Micheweni kwa kila roba kwa Sh 15,000,” anasema.

“Ukweli uliopo sasa tunategemea viazilishe zitatukomboa vizuri kwa sababu zina uhitaji mkubwa kuliko za kawaida,” anaelezea.

Hii imefanya apanue shamba lake kwa ajili ya kuzalisha na kulima viazilishe.

Kwa upande wa changamoto, anasema ni ukosefu wa taaluma ya kilimo cha viazilishe.

“Tunakosa taaluma, hususan uelewa wa namna ya kuendesha kilimo cha viazilishe, hasa katika wakati wa ugonjwa,” alifafanua Bakari.

Naye Salim Makame, ambaye ni mwezeshaji wa viazilishe na mkulima kutoka kijiji cha Msuka Mashariki, Kata ya Kifundi, Wilaya ya Micheweni Pemba, ameweza kugawa mbegu hizo kwa wanakijiji zaidi ya 20 bure.

Anaelezea uhitaji mkubwa wa mbegu bora ya viazi lishe katika Kijiji cha Msuka kutokana wananchi wa eneo kugundua umuhimu wa kilimo cha viazi lishe.

“Faida ya viazilishe ni chanzo muhimu cha vitamini A, na pia katika kutengeneza bidhaa mbalimbali, zikiwamo unga ambao hutumika kutengenezea bidhaa mbalimbali kama vile mikate, keki, maandazi, chapati, biskuti na vitafunwa vinginevyo,” anasema Salim.

Mradi wa Fast Track Wilaya ya Micheweni unaendeshwa kwenye shule za msingi nane tangu mwaka 2015.

Ofisa Mipango wa Wilaya ya Micheweni, Hamad Khamis, anasema huu ni utaratibu mwingine unaotumika katika kusambaza hizo mbegu bora.

Khamisi anaelezea kuwa, wanachagua wanafunzi 200 kila shule kila mmoja na anawapatia vipande 200 vya aina tatu ya mbegu.

“Kila mwanafunzi anatakiwa kurudisha au kugawa vipande 200 kwa majirani baada ya kuzalisha hivyo vipande, wanafunzi wanatakiwa warudishe vipande 200 baada ya kuzalisha.

“Mwitikio wa mradi huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa sababu ubora wa mbegu na uhamasishaji umechangia kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Mradi wa viazilishe unasimamiwa na Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, kupitia taasisi za utafiti na wadau wengi kama International Institute Tropical Agriculture (IITA) na Jukwaa Huru la Wadau wa Kilimo (ANSAF).

Mradi huo unatekelezwa katika mikoa 6, ikiwamo Morogoro, Pwani, Geita (Sengerema), Zanzibar na Shinyanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here