23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

UVCCM ARUSHA WACHAPANA MAKONDE

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

UCHAGUZI wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Arusha Mjini umeanza kwa vurugu, baada ya baadhi ya wajumbe kupigana ngumi hadharani.

Vurugu hizo zilijitokeza kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, uliowahusisha pia wajumbe wa mkutano wa wilaya wa UVCCM uliofanyika jana, ukumbi wa Hoteli ya Golden Rose, baada ya wapambe wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti kuzichapa nje ya ukumbi huo wakati walipoanza kutuhumiana.

Kutokana na vurugu hizo, uongozi wa hoteli hiyo ulilazimika kuita gari la ulinzi la Kampuni ya Ultimate Security.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, vurugu hizo zinadaiwa kutokea kwa muda wa dakika 15 hadi 20, baada ya wapambe hao kudaiwa kushikana mashati na kutwangana ngumi nje ya ukumbi huo, huku umati ukishuhudia tukio hilo, wakiwamo watembea kwa miguu na watu wenye ofisi katika hoteli hiyo.

Wagombea nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo ni Jimmy Pamba na Godliving Kisila, wanaochuana kumrithi Martin Munisi, anayemaliza muda wake na inadaiwa kuwa ugomvi huo ulianza baada ya wapambe wao kutofautiana.

Mmoja wa wapambe wa Kisila, Hussein Abdallah, anadaiwa kumtuhumu Lameck Dudu, anayedaiwa kuwa kambi ya Pamba, kuwa si mjumbe wa mkutano huo na kudai kuwa ni tapeli wa kisiasa, hivyo hakupaswa kuwapo katika uchaguzi huo.

Kutokana na kauli hiyo, Dudu anadaiwa kumrushia ngumi Hussein na kuanguka chini, hali iliyofanya wapambe wengine wa pande zote mbili kutokukubaliana na hali hiyo na kuanza kupigana.

Vurugu hizo zilisababisha askari mmoja wa kike wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) aliyekuwa karibu na eneo hilo kujaribu kutuliza vurugu hizo, ila ilishindikana na baadaye kikosi cha askari polisi walifika katika eneo hilo na kutuliza vurugu hiyo na kuwataka wajumbe hao kurudi katika ukumbi wa mkutano.

Mmoja wa vijana aliyepigwa na aliyejitambulisha kwa jina la Silvester Meda, alidai kuwa, licha ya kupigwa na kuchaniwa nguo zake, hajui kosa lake ni lipi.

“UVCCM Arusha imezungukwa na wahuni, hivyo chama kinapaswa kuwachukulia hatua wote walioiaibisha jumuiya hiyo kwa maslahi yao,” alisema.

Naye Katibu Hamasa wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Abdi Marijana, alidai kuwa, Dudu ndiye chanzo cha vurugu hizo, pia si mjumbe halali wa mkutano huo.

“Polisi walipaswa kumkamata Dudu kwa sababu ni chanzo cha vurugu hizo, ila sijui kwanini polisi hawajamkamata,” alisema.

Baada ya vurugu hizo, wajumbe wa mkutano huo walirejea katika ukumbi na kuendelea na uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles