28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 31,000 KUKOSA MIKOPO ELIMU YA JUU

Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

WANAFUNZI zaidi ya 61,000 wamewasilisha maombi ya mikopo katika Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa mwaka mpya wa masomo wa 2017/2018, unaotarajiwa kuanza Oktoba, mwaka huu, huku idadi kamili ya wanaotakiwa kupewa ni 30,000.

Pia kati ya hao, waliowasilisha maombi yaliyokamilika ni wanafunzi 43,811, huku 11,200 taarifa zao zilibainika kuwa na kasoro na upungufu mbalimbali.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razak Badru, alisema wanafunzi hao ni wale waliofanikiwa kuomba katika muda uliofikia ukomo Agosti 11, mwaka huu.

“Hawa tunaweza kusema ni incomplete kwa sababu wako ambao wamekosa baadhi ya nyaraka kama vile vyeti vya kuzaliwa au taarifa za wazazi,” alisema.

Pamoja na kuwapo kwa kasoro hizo, alisema wale wote walioomba katika muda maalumu uliopangwa watapata fursa ya kusahihisha taarifa zao.

Alisema kwa sasa wanaendelea kufanya uchambuzi wa taarifa za waombaji ili kubaini walio na sifa za kupewa mikopo na baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo watatoa majina ya wale waliopitishwa kupata mikopo hiyo na kuanza kuwapangia mikopo yao.

“Kwa mujibu wa kalenda yetu ambayo ndiyo inayotuongoza, inaonyesha kuwa, hadi kufikia Oktoba 10, mwaka huu, taratibu zote za uchambuzi na kutangazwa kwa majina ya wale walio na sifa ya kupata mikopo inatakiwa kuwa imekamilika na tayari wanafunzi waanze kupelekewa mikopo hiyo vyuoni kwao,” alisema.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole, alisema wataangalia vigezo mbalimbali kwa wanafunzi 30,000 wanaotarajiwa kupewa mikopo hiyo.

Alivitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni kwa wanafunzi waliopata nafasi katika vyuo vikuu, wawe raia wa Tanzania, wawe wamemaliza kidato cha sita si kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na vingine vyote vilivyoelekezwa na HESLB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles