24.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Uvamizi walemavu wa ngozi waanza upya Rukwa

Mussa Mwangoka, Rukwa

HUWEZI kuamini kwamba hadi leo hii walemavu wa ngozi (Albinism) bado wanaishi maisha ya hofu, licha ya matukio ya mauaji na kukatwa viungo dhidi yao kupungua tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza na MTANZANIA, Gaudensia Zumba (58) mkazi wa Kijiji cha Mtimbwa, mkoani Rukwa, ambaye ni mlemavu wa ngozi, anasema yeye na familia yake bado wanaishi kwa hofu.

Gaudensia ambaye anatoka familia ya watoto 12, wanne wakiwa na ulemavu wa ngozi, anasema hata hivyo, hofu waliyonayo sasa si sawa na ilivyokuwa awali.

Anasema tofauti na awali, siku hizi wanaweza hata kujitokeza na kushiriki shughuli za kijamii.

Anasema kuwa hivi majuzi mdogo wake, Maria Zumba (38) alivamiwa nyakati za usiku na kutaka kumdhulu.

Anasema watu hao walifika nyumbani kwake na kutishia kumkata viungo vyake lakini ujasiri wa mume wake, aliyejulikana kwa jina moja la Milambo ulisaidia kuepusha tukio hilo lisitokee.

“Kuna watu walikuja zaidi ya mara tatu kwa nyakati tofauti, usiku wa manane, mara ya kwanza walibomoa ukuta na kuingia ndani lakini tulivyowasikia tulipiga kelele wakakimbia.

“Kuna mwingine alikuja akavunja mlango tukamfahamu, tukatoa taarifa polisi ambapo alikamatwa na kupelekwa mahakamani, lakini baadae alichiwa huru kwa kuwa ushahidi haukupatikana.

Gaudensia anasema mazingira hayo yamewafanya wawe na wakati mgumu kushiriki katika baadhi ya shughuli za uzalishaji mali zitakazowaongezea kipato.

“Nikienda shambani sitakiwi kuwa peke yangu kwa sababu kuna watu huwa wananiwinda ili wanijeruhi, wakate viungo vyangu na kutimiza haja zao.

“Kuna wakati nilikuwa bustanini peke yangu, ghafla kuna watu wawili nikasikia wanazungumza kuhusu kunivamia, tena walikuwa wamejificha na mapanga.

“Nilipiga kelele wakakimbia, sasa kwa maisha haya utawezaje kufanya shughuli za uzalishaji mali, ni vipi tutajiongezea kipato?” anahoji Gaudensia.

Naye James Malocha, ambaye ni mtoto wa Gaudensia, anasemaa kutokana na hofu waliyonayo kuhusu maisha yao, amelazimika kuwa mlinzi wa ndugu zake wenye ulemavu wa ngozi.

“Kila wanakoenda nawasindikiza, wakiwa peke yao bila ulinzi ni rahisi kuvamiwa na watu wenye nia mbaya.

“Kuna wakati mama akitaka kwenda mjini au katika shughuli zake nyingine inabidi niwe naye,” anasema Malocha. 

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtimbwa, Willbroad Kapufi, anakiri kutokea kwa matukio hayo. Anasema kuwapo kwa walinzi kupitia mabaraza ya kata na vijiji kutasaidia kuwalinda na kuwabaini wale wenye tabia ya kutishia uhai wa maisha ya albino na kuwafikisha katika vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa na mikakati ya kuhakikisha walemavu wa ngozi wanaishi kwa amani pasipo hofu na shaka yoyote kama ilivyo kwa wananchi wengine.

Miongoni mwa wadau hao ni Muungano wa Asasi za Kiraia Sumbawanga Mjini (Sumango), inayotekeleza mradi wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Civili Society.

Mkurugenzi mtendaji wa Asasi hiyo, Vincent Kuligi, anasema huwa wanatoa mafunzo ya kuelimisha jamii kuona watu wenye ulemavu wa ngozi ni sawa na wengine na wanastahili haki zote za msingi.

Anasema pia wameuunda mabaraza ya kata 11 za Sumbawanga Mjini na Vijijini, ambayo yana jukumu la kuwalinda watu wenye ualbino wanaoishi ndani ya kata zao na maeneo mengine.

Anasema kitendo cha kutowapeleka shule watoto wenye ualbino ni makosa, wanawakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu.

“Ndio maana tumeanzisha mabaraza haya yakiwa na lengo la kuhakikisha wanalindwa kila mara na wasibughudhiwe kwa namna yoyote ile,” anasema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Wangabo, anasema ni jukumu la Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kulinda raia wake hivyo, si tu walemavu wa ngozi wanaohakikishiwa ulinzi bali wananchi wote kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles