23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI WABAINI UDHAIFU SHERIA ZA MAFUTA, GESI

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

SHERIA zinazosimamia masuala ya mafuta na gesi nchini zimetajwa kuwa dhaifu, hali inayoweza kusababisha nchi kutofaidika kwa kiwango stahiki.

Hayo yamebainika baada ya taasisi ya kimataifa inayoangalia utawala wa maliasili (Natural Resource Governance – NRGI) kutoa ripoti yake ya utafiti kwa mwaka 2017 uliohusisha nchi 81 duniani.

Kati ya nchi hizo zilizofanyiwa utafiti, Tanzania imepata alama 53 kati ya 100 za ubora, matokeo yanayoiweka nafasi ya 36.

Akitoa dondoo zilizomo katika ripoti hiyo, Meneja wa NRGI Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Silas Olan’g, alisema Tanzania inapaswa kuboresha sera na sheria zake zinazosimamia masuala ya mafuta na gesi kabla ya kuanza uchimbaji mkubwa.

“Tanzania imegundua uwapo wa kiasi kikubwa cha gesi na mafuta kwenye eneo lake la Bahari ya Hindi, lakini bado haijaanza uzalishaji wa kiwango cha juu, ipo haja ya kuboresha sera yake ya usimamiaji wa maliasili hizo ili ziweze kulinufaisha taifa.

“Hatua hii ni muhimu kwa Tanzania, hasa ukizingatia kuwa nchi hii ni miongoni mwa nchi zenye ongezeko kubwa la watu duniani,” alisema.

Kwa mujibu wa utafiti huu, kipengele cha upatikanaji wa thamani ni eneo ambalo Tanzania inafanya vizuri kuliko usimamizi wa mapato yatokananyo na rasilimali hizo.

Upatikanaji wa thamani hupimwa kwa kuangalia utawala bora katika mfumo wa utoaji leseni, manufaa kwa jamii na ushiriki wa Serikali kwenye uvunaji wa rasilimali.

Katika sekta ya mafuta na gesi asilia, Tanzania imepata alama 48 kati ya 100 na kushika nafasi ya 27 nyuma ya Msumbiji iliyopewa nafasi ya kwanza kutokana na kupata alama 72.

Matokeo haya dhaifu kwa Tanzania yanatokana na kutokuwapo kwa taasisi huru yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria ya mafuta ya mwaka 2015.

Kwenye eneo la usimamizi wa mapato yanayotokana na maliasili ya mafuta na gesi, Tanzania imeachwa nyuma na nchi za Ghana, Msumbiji na Uganda.

Kwenye sekta ya madini, Tanzania imeshika nafasi ya 42, huku ikiwa ya 18 kati ya sekta 34 za madini zilizofanyiwa tathmini.

Aidha utafiti huo umebainisha kuwa kuwapo kwa shaka ya mgawanyo wenye manufaa baina ya wawekezaji, Serikali na jamii katika maeneo ya migodi, kumechangia kuifanya Serikali kuchukua hatua za kuboresha utawala na uwazi katika sekta hii.

Hata hivyo, matokeo ya NRGI yamebaini haja ya kuziba pengo kati ya matakwa ya kisheria na utekelezaji wake kwa vipengele vingi vilivyotathminiwa.

Aidha mageuzi yanahitajika katika kudhibiti rushwa na ufanisi katika utendaji wa Serikali – kama ufanyavyo utawala wa sasa.

Athari za mazingira na za kijamii inabidi zishughulikiwe kikamilifu kupunguza athari hasi kwa jamii.

Mikataba baina ya Serikali na wawekezaji ni sharti iwekwe wazi kwa umma kwa mujibu wa sheria ya uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ya mwaka 2015.

Akifafanua zaidi Olan’g alisema bado kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanyika ili kuleta usimamizi madhubuti katika sekta ya madini Tanzania.

Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji dhahabu Afrika.

Utafiti umekwenda mbali zaidi kwa kubaini kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ni miongoni mwa mashirika ya umma matano ya mwisho kati ya 45 katika nchi zinazotekeleza Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji Katika Tasnia ya Uziduaji (EITI).

STAMICO imetajwa kutoweka wazi taarifa za mwaka zinazoonyesha shughuli zake za kibiashara na matokeo yake, na kwamba hata taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinatoa baadhi tu ya taarifa hizo kwa umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles