WADAU WATAKA MISWADA YA RASILIMALI INUFAISHE TAIFA

0
478
Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge, akitoa maoni jana wakati wa kikao cha wadau kutoa maoni kuhusu miswada ya kulinda rasilimali za nchi iliyopelekwa bungeni Dodoma. PICHA SILVAN KIWALE
Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge, akitoa maoni jana wakati wa kikao cha wadau kutoa maoni kuhusu miswada ya kulinda rasilimali za nchi iliyopelekwa bungeni Dodoma. PICHA SILVAN KIWALE

Na Ramadhan Hassan – DODOMA

KAMATI ya Bunge ya pamoja iliyoundwa na Spika Job Ndugai ya kujadili miswada mitatu ya ulinzi na rasilimali za nchi, imeendelea kupokea maoni ya wadau, walioshauri sheria zinazotungwa ziwe na manufaa kwa taifa.

Miswada iliyowasilishwa hivi karibuni bungeni ni ule wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali zenye upungufu  wa mwaka 2017, muswada wa sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu  masharti, hasa  katika mikataba ya maliasili wa mwaka 2017 na muswada  wa sheria ya mamlaka ya nchi kuhusu umiliki wa maliasili  wa mwaka 2017.

Kikao hicho kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni mkoani hapa,  kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dotto Biteko na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa.

Waliohudhuria kikao hicho ni mawaziri, wabunge na wadau mbalimbali ambao walipata nafasi ya kuchangia.

NSHALA

Wa kwanza kutoa maoni alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk. Rugemeleza Nshala ambaye alisema kuwa kuna ulazima wa kuzungumzia kuhusu mikataba ya pande mbili au tatu ambayo nchi itaingia.

“Kuhusu migogoro ya kiuwekezaji ikatatuliwe mahakama za nje, hapo ndo kuna tatizo kwa hiyo inabidi kiondolewe hicho kitu, tuseme mikataba yote ya pande mbili au tatu zinazoendelea kama inakiuka uwezo wa mahakama zetu kuweza kuamua migogoro, hii mikataba ni batili, naomba lizingatiwe,” alisema.

Dk. Nshala alisema kuna muswada unatoa nafasi kwa Serikali kuweza kujadiliana, lakini wao kama taasisi wanaona ni lazima muswada ueleze ni nani ataingia kwenye majadiliano hayo, huku akitaka sheria iseme wazi.

Alisema mahakama za hapa nchini ndio ziamue vipengele ambavyo vitaonekana vinakinzana na kuagiza mgogoro labda umalizike ndani ya muda fulani na kama vipengele hivyo ni vya msingi au si vya msingi.

Akizungumzia kuhusu kuundwa kwa Kamisheni ya Madini, alisema kuna udhaifu katika kuondoa madaraka ya waziri kujadiliana kwenye mikataba, wakati kuna dhana ambayo ipo ya mikataba kujadiliwa, lakini sheria haisemi ni nani ambaye atajadili.

“Haisemi ni waziri gani na taasisi gani ya Serikali ambayo itaanzisha majadiliano au kama ni Kamisheni ya Madini ndiyo itapatiwa madaraka hayo sheria haisemi,” alisema.

Pia Dk. Nshala alisema kama kamisheni haina utaalamu huo, ni namna gani itakuwa na utaalamu kwa kuwa na timu ya wataalamu kuweza kujadiliana.

“Kama tunaona kuna tatizo kuwa na mikataba, sisi tunaona kwamba kwa nini tusifuate mfano wa Zambia na Afrika Kusini ambako utaratibu wao unasema hakuna kujadiliana mambo ya mikataba, wameingiza kwenye sheria ambapo ukitaka leseni ya kuchimba madini omba leseni na masharti yake yatakuwa kwenye sheria,” alisema.

Alibainisha kuwa hakutakuwa na masuala ya kumuweka mtu sawa, hivyo mtu atatakiwa kufuata masharti yaliyowekwa kwenye matakwa ya sheria.

“Ni vyema sisi kama tunaona hatuna utaalamu wa kujadiliana haya na kufikia uwezo wa Botswana, sisi tufuate leseni, Afrika Kusini walitaka kufanya kuwa na mikataba wakakataa kwamba mtu ataomba leseni na kukutana na masharti ya kisheria humo na sio kuingia mikataba, tuangalie uwezekano wa hicho kitu, tusitake kuinyanyasa Serikali,” alisema mwanasheria huyo.

Vilevile, alisema sheria hizo hazizungumzii namna ya kujitoa kwenye hiyo mikataba lazima iseme Serikali itaingia kwenye mchakato wa kujitoa katika mikataba ambayo inaibana.

“Kwa nini Serikali isihakikishe hatuwezi kusaini kujifunga na mambo ya migogoro kutatuliwa kwenye mahakama za kimataifa kwa kuwa kutakuwa na ‘political risk’ hapa, maana watatupeleka nje na wakishinda wataenda kuchukua fedha, MIGA inatakiwa ilipe na itakuja hapa kudai nchi ilipe, tunabidi tujitoe kwa kuwa ni hatari sana,” alisema.

MWAKILISHI WAWEKEZAJI WAKUBWA

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Tanzania Chamber of Minerals, Gerald Mturi, ambaye alitoa maoni kwa niaba ya wawekezaji wakubwa, alidai kuwa katika mchakato wa kusafirisha madini nje ya nchi, kuna mambo hayajawekwa sawa ni nani atawajibika kama utatokea upotevu na mwekezaji atafidiwaje.

Kuhusu migogoro kutatuliwa kwenye mahakama za hapa nchini, Mturi alisema suala la mashauri yote kujadiliwa nchini litaleta shida kwa wawekezaji.

“Wawekezaji wa nje kwa utaratibu huo hauleti amani, suala hili linatakiwa kuangaliwa upya kwa kuwa tutawakimbiza wawekezaji,” alisema.

Aidha Mturi alisema kuna tatizo katika kifungu 10(1)-(3) kinachosema kwamba Serikali inaweza kuwa na asilimia 50 ya hisa kwenye mgodi na kampuni ikatakiwa kupeleka tena hisa 30 kwenye soko la hisa jambo ambalo litaifanya kubaki na asilimia 20.

“Sisi tunapendekeza kipengele hicho mfikirie namna ya kukiondoa, hasa cha upelekaji hisa asilimia 30 kwenye soko la hisa kwa kuwa kitakimbiza wawekezaji,” alisema Mturi.

BASHE ACHARUKA

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alimbana Mturi, kuwa amehusika na kudhulumu fedha za tozo za ushuru katika Halmashauri ya Nzega.

“Tunasema tukiweka kila kitu katika sheria tutakimbiza wawekezaji Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982, ilisema kuwe na Service Levy ya asilimia 0.03 wewe umeondoka Nzega bila ya kulipa, haujalipa umelipa ‘only’ 2 billion kwa hoja kwamba kulikuwa hakuna ‘by law’ ndiyo maana tunasema kila kitu  kiwekwe kwenye sheria.

“Ameongelea nchi kama Botswana wana miundombinu mizuri, lakini hajasema katika kikao hiki ana share holder ya asilimia 40 kwenye  migodi hiyo.

“Pia nataka nitoe mfano ukienda Nyamongo kwa Heche (John), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka polisi, inaweka wa nini wanalipwa hawa, hivyo ‘deposit’ iliyopo chini ya ardhi unayoenda kukopea ndio msingi wa wewe kukopa  kwa nini unadhani wewe ni vibaya kwa Serikali  kwamba wewe unakuja na teknolojia na mtaji  mimi nina maliasili,  kwa nini ni vibaya?” aliuliza Bashe.

Akijibu, Mturi alisema suala la ushuru katika Halmashauri ya Nzega lipo kisheria kwa sababu kuna Sheria ya Local Government Finance ambayo haiwezi kusimama yenyewe kwani hiyo sheria inaziruhusu halmashauri kutoza hadi asilimia 0.03.

MWAKILISHI WACHIMBAJI WADOGO

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimba Madini Wadogo Wadogo Tanzania, John Bina, akitoa maoni kwa niaba ya wachimbaji wadogo wadogo, alishauri madini ya Tanzanite yawe na sheria maalumu kutokana na kupatikana Tanzania pekee.

“Katima miswada yote mitatu hakuna sehemu inayohusu wachimbaji wadogo wadogo, lakini muda wa umiliki tunapewa miaka saba pekee, hili liangaliwe,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here