27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Utafiti MUHAS waibua mambo kinga ya malaria kwa wajawazito

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WAJAWAZITO wanaohudhuria vema kliniki na kupatiwa dawa kinga ya malaria, hujifungua watoto wenye uzito timilifu kuliko wale wanaosuasua.

Hayo ni matokeo ya awali ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambao ulihusisha wajawazito 1,191 waliokuwa wakihudhuria kliniki katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.

Yalielezwa hayo juzi jioni na Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia taaluma ya utafiti na ushauri wa kitaaluma, Profesa Aporilnary Kamuhabwa alipowasilisha mada kwenye kongamano la kisayansi la kitafiti kuhusu mchango wa MUHAS katika mapambano dhidi ya malaria Tanzania.

Alisema malaria ni miongoni mwa visababishi vya mtoto kuzaliwa na uzito pungufu na kwamba hali hiyo huambatana na changamoto mbalimbali kwa mtoto husika kipindi cha ukuaji wake.

“Majukumu ya chuo kikuu ni pamoja na kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu, huwa tunaangalia maeneo ambayo nchi imeweka kipaumbele, malaria ni miongoni mwa magonjwa ambayo tunapambana nayo nchini.

“Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana tuliamua kufanya utafiti kuangazia mapambano dhidi ya malaria kwa wajawazito,” alibainisha.

Alisema ni kweli Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanya kazi kubwa kupambana na malaria na sasa kiwango cha maambukizi kimeshuka kwa kiasi kikubwa.

“Hata hivyo bado kwenye maeneo kadhaa kuna changamoto, mengine kiwango kipo chini na mengine kipo juu zaidi ya wastani wa kitaifa. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kimepungua mno, ni chini ya asilimia moja,” alisema.

Alisema katika utafiti huo wataalamu wa MUHAS waliangalia iwapo dawa aina ya SP inayotumika kuwakinga wajawazito, inasaidia katika kukabili ugonjwa huo au laa.

“Dawa hiyo huwa wanapatiwa wajawazito wanapohudhuria kliniki, hasa mimba ikiwa imefikia wiki ya 13 na kuendelea baada ya uchunguzi, hupatiwa kila wiki kulingana na sera ya WHO na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii. jinsia, Wazee na Watoto.

“Hivyo matokeo ya awali yameonesha mafanikio, inasaidia. Tumejaribu kuangalia walitumiaje dawa hiyo ya SP, tulichunguza hadi kondo la nyuma kuangalia iwapo vimelea vya malaria vilibaki, kwa sasa tunafanya majumuisho kati ya Machi na Aprili, mwaka huu tunatarajia kukamilisha,” alibainisha.

Alisema kimsingi kadiri mjamzito anavyotumia vizuri dawa hiyo, ndiyo inavyosaidia kuzuia madhara kwa mtoto anayezaliwa, hasa kuwa na uzito pungufu na kukabili tatizo la upungufu mkubwa wa damu kwa mama husika.

“Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwahimiza wajawazito kuhudhuria kliniki.

“Pamoja na utafiti huu, tunafanya pia mwingine huko Rufiji mkoani Pwani tukiangazia aina nyingine ya dawa kinga ambayo inaweza kuwa mbadala wa SP ikiwa itaonesha usugu katika kukabili ugonjwa huo,” alisema.

Alisema dawa hiyo inayofanyiwa utafiti iliyopendekezwa na WHO, imeonesha mafanikio Tanzania kama ilivyo kwa Kenya na Uganda.

“Tupo kwenye majumuisho kuitafiti kabla haijaruhusiwa kuanza kutumika rasmi, lazima nasi tujiridhishe,” alisisitiza.

Alisema pamoja na tafiti hizo, MUHAS kwa kushirikiana na wadau wengine sasa wanaendelea pia kufanya utafiti mbalimbali kumchunguza mbu aenezaye ugonjwa huo na mazingira ya mazalia kwa ujumla wake.

Mwisho

Ocean Road yaongeza idadi ya saratani watakazotoa huduma ya awali ya uchunguzi

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,464FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles