25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Usajili vyama vipya wasitishwa

Jaji Francis Mutungi*Jaji Mutungu asema hana fungu la kutosha

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesitisha kwa muda usajili wa vyama vipya vya siasa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA, Dar es Salaam juzi, Jaji Mutungi alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na ofisi yake kukosa fedha za kutosha.

“Hakuna amri yoyote ya kuzuia kusajili vyama vipya vya siasa, ofisi yangu inahitaji fedha za kufanyia uhakiki ili iweze kusajili vyama vipya ama kuvifuta vyama vya siasa visivyo na sifa.

“Serikali ikitoa fungu la kutosha kwa ajili ya Ofisi ya Msajili, tunaweza kufanya uhakiki kwa ajili kuvisajili vyama vipya na kuvifuta visivyo na sifa… hatua zote hizi zinahitaji fedha, fungu dogo lililopo haliwezi kusajili vyama vipya wakati vipo vya zamani ambavyo havina sifa,” alisema.

Jaji Mutungi alisema badala ya kusajili vyama vipya kwa fedha zilizopo, ofisi yake ilianza kuvifanyia uhakiki vyama vyote 22 vyenye usajili wa kudumu vilivyopo na tayari uhakiki umekamilika.

Alisema hawezi kusajili chama kipya wakati hata vilivyopo miongoni mwake vipo ambavyo havina sifa ya kuendelea kuwapo.

“Tutaanza kuvichinja vilivyopo ambavyo vimebainika havina sifa, kuna vyama havina hata akaunti, namba ya chama na vingine havina wanachama, tutavifuta wakati wowote,” alisema.

Alisema ofisi yake iko mbioni kuvifuta vyama vya siasa vilivyobainika kukosa sifa baada ya kufanyiwa uhakiki, ingawa hakutaka kuvitaja kwa kuwa wakati wake haujafika.

Jaji Mutungi alisema vyama vyote ambavyo havina sifa vinaweza kufutwa wakati wowote na kuwa wahusika tayari wamepewa notisi.

“Vyama vinavyofutwa hadi sasa vinajijua, vilishapewa notisi na vile ambavyo havitafutwa vinajijua, kwa sababu tayari vimepewa barua ya onyo.

“Baadhi vitafutwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kisheria yaliyoviwezesha kupata usajili wa kudumu.

“Jukumu kubwa la ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni kusimamia, kuboresha, kuendeleza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi nchini, majukumu ambayo yanatokana na Sheria ya Vyama vya Siasa Namba. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi Namba. 7 ya mwaka 2010,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema majukumu mengine ya ofisi yake ni kusajili vyama vya siasa na kuvifuta vyama ambavyo havikidhi matakwa ya sheria hiyo, na kusimamia ugawaji wa ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.

“Miongoni mwa sababu za kuvifuta vyama hivyo ni kutokana na baadhi yake havina ofisi za kudumu Tanzania Bara na Zanzibar au upande mmoja na vingine havina anuani ya posta,” alisema.

Alisema kuna baadhi ya vyama vimeshindwa kuonyesha akaunti ya fedha ya chama, hali inayotia shaka namna vinavyojiendesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles