24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Urais Kongo njia panda

* Tshisekedi atangazwa mshindi, mshirika wa Kabila abwagwa

*Wapinzani Kanisa Katoliki, Ufaransa wapinga matokeo

KINSHASA, DRC

MGOMBEA urais wa upinzani kutoka Chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Felix Tshisekedi ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini hapa.

Mbali ya kutangazwa mshindi, matokeo hayo yamepingwa na mgombea mwingine mkuu wa kambi ya upinzani, Martin Fayulu Madidi.

Kelele za kushangilia ziliibuka katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) wakati matokeo hayo ya kihistoria yakitangazwa.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekuwa katika mzozo wa miaka miwili kuhusu mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye alikuwa amegoma kuondoka madarakani tangu mwaka 2016, wakati muda wake ulipomalizika baada ya karibu miongo miwili madarakani.

Mgombea aliyemteua mwenyewe, msiri wake na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Ramazani Shadary alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.

Mgombea mwingine wa upinzani, mfanyabiashara na Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Kampuni ya Mafuta, Fayulu ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kwenye kura za maoni kushinda, alishika nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa Mkuu wa CENI, Corneille Nangaa, Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zote na hivyo kutangazwa kuwa rais mteule.

Hata hivyo, inasubiriwa kuona namna wananchi watakavyoyapokea matokeo hayo baada ya Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini hapa kuonekana kuungana na Fayulu kuyapinga.

Akizungumzia idadi halisi ya kura, Nangaa alisema Tshisekedi alipata kura 7,051,013 akimshinda Fayulu aliyepata kura 6,366,732 sawa na asilimia 34.83.

Mgombea urais aliyekuwa akiungwa mkono na muungano wa vyama tawala (FCC), Shadary, alipata kura 4,357,359 sawa na asilimia 23.84 ya kura, huku mwitikio wa wapigakura ukiwa asilimia 47.56.

FAYULU ADAI KUPORWA USHINDI

Ushindi huo usiotarajiwa wa Tshisekedi unapingwa na Fayulu aliyetuhumu ni wa makubaliano ya nyuma ya pazia na Rais Kabila.

Alisema Serikali imeshirikiana na Tshisekedi kumpora ushindi baada ya kuona mgombea wake (Shadary) habebeki, hivyo kutafuta mbadala.

 “Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano na ukweli halisi. Raia wa Kongo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura milioni saba, haiwezekani. Alizitoa wapi hizo?

 “Nangaa (mwenyekiti wa CENI) anafuma kitambaa cheusi kwa uzi wa rangi nyeupe. Natoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo yao halisi.

“Nangaa na marafiki zake katika FCC (chama tawala), wamekuwa wakichakachua matokeo kumpa ‘kikaragosi wao ushindi’,” alisema Fayulu.

Awali, alikuwa alikiambia Kituo cha Redio cha Kimataifa cha Ufaransa (RFI) kwamba matokeo hayo ni mapinduzi halisi kupitia uchaguzi na akatoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo waliyonayo aliyosema ni ya kweli.

Hata hivyo, ni kinyume cha sheria kwa mtu au chombo kingine chochote kile mbali ya CENI kutangaza matokeo ya uchaguzi nchini hapa.

KANISA KATOLIKI LAPINGA MATOKEO

Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa kutokana na wingi wa waumini wake, lilisema matokeo rasmi yaliyotangazwa na CENI yanakinzana na matokeo yaliyoandaliwa na waangalizi wake.

Kanisa hilo liliongoza kwa wingi wa wangalizi wa uchaguzi 40,000 waliosambaa kote nchini hapa na kukusanya matokeo yaliyobandikwa nje ya vituo vyote vya kupiga kura

Lilidokeza kuwa Fayulu alishinda kirahisi akipata kura nyingi, kwa mujibu wa takwimu walizonazo.

Lakini pia Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Mchungaji Donatien Nshole, alitoa mwito kwa Wakongo wote kuhakikisha amani na wote wanaopinga matokeo watumie vyombo vya sheria bila kusababisha machafuko.

KAMBI YA KABILA YAKUBALI KUSHINDWA

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Barnabe Kikaya bin Karubi, ambaye ni mmoja wa washauri wakuu wa Rais Kabila amekubali matokeo hayo.

“Bila shaka hatujafurahia kuona mgombea wetu ameshindwa, lakini raia wa Kongo ndio wameamua. Hii ndiyo demokrasia, demokrasia imeshinda,” alisema.

USHIRIKA WA SIRI

Tshisekedi, kwa upande wake ameyafurahia matokeo hayo na kumsifu pia Kabila, akisema ni mshirika mzuri kisiasa.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika katika mji mkuu wa Kinshasa, Tshisekedi alisema atakuwa ‘rais wa raia wote wa Kongo’.

“Namshukuru Rais Joseph Kabila, ambaye leo hii hatupaswi tena kumchukulia kama adui bali kama mshirika katika mabadiliko ya kidemokrasia nchini mwetu,” alisema.

Kumekuwa na tetesi kwamba kucheleweshwa kwa shughuli ya kutangaza matokeo, ambayo awali yalikuwa yatangazwe Jumapili iliyopita, kulitoa fursa kwa Rais Kabila na Tshisekedi kuafikiana baada ya kuonekana Shadary hana nafasi ya kushinda uchaguzi huo.

Kabla ya matokeo kutangazwa kambi ya Tshisekedi ilikiri uwapo wa mazungumzo na Kabila, waliyodai yamelenga makabidhiano ya amani ya madaraka kwa vile mshindi (wao) ameshafahamika.

Aidha walisema chama chao hakina mpango wowote wa kulipiza kisasi dhidi ya mabaya ya utawala wa Kabila.

Tetesi za kuwapo mazungumzo hayo, ambayo kambi ya Kabila na Shadary iliyakana ikiendelea kusisitiza itashinda uchaguzi huo, ziliwatia hofu wafuasi wa Fayulu kuwa kuna njama za kuwapora ushindi.

UFARANSA YAOMBA UFAFANUZI WA MATOKEO

Kwa mujibu wa Reuters, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves, ameomba kuwepo ufafanuzi kuhusu matokeo hayo akisema ushindi wa Tshisekedi unaenda kinyume na uhalisia wa ushindani.

“Kanisa Katoliki lilifanya majumuisho yake ya kura na kutoa matokeo tofauti kabisa,” amenukuliwa na shirika hilo akisema.

Baadhi ya kura za maoni zilikuwa zinamwonesha Fayulu akiwa mbele ya wagombea wengine.

Lakini Msemaji wa Tshisekedi, Claude Lbalanky alisema siku ya jana ni njema kwa taifa na alikana kwamba kulikuwa na makubaliano ya siri na Kabila kumpa ushindi Tshisekedi.

“Tuna furaha sana tena sana. Hii ni siku njema kwa DRC. Mnafahamu kuwa maoni ya wananchi yameheshimiwa. Kwahivyo tumefurahia sana,” alisema.

Kuhusu madai ya uwapo makubaliano ya siri na Kabila, alisema: “Hilo si kweli. Ukweli ni kuwa hauwezi kuwa na makabidhiano ya madaraka bila pande mbili kuzungumza. Ilipobainika wazi tungekuwa washindi, tulikwenda kumwona Rais anayeondoka (Kabila) na kuzungumza jinsi shughuli ya mpito inavyoweza kufanyika vyema. Si kitu kingine.

“Tumeshuhudia jambo kama hilo likitokea Afrika Kusini wakati (Nelson) Mandela alipochukua madaraka kutoka kwa utawala fidhuli wa ubaguzi wa rangi.

“Ni lazima kuwe na mazungumzo ya aina fulani, kusema ‘ehee, nyinyi mmeshinda. Nitakuwa salama?’. Kwa hivyo, bila shaka hakukuwa na zaidi ya hayo. Hakukuwa na makubaliano yaliyoathiri matokeo ya uchaguzi huu.”

Tshisekedi mwenyewe pia amekiri kufanya mazungumzo na chama tawala, lakini yakijikita kuhusu maandalizi ya kipindi cha mpito baada ya kuonekana ameshinda.

Swali kuu kwa sasa ni jinsi wananchi na wadau wa kisiasa watakavyoyapokea matangazo hayo.

Na Kanisa Katoliki lilishatahadharisha mapema kabla ya matokeo kuwa litayakataa iwapo hayatakuwa ya kweli.

Kanisa hilo lilisema linamfahamu mshindi wa urais na kwamba alikuwa ni mshindi wa wazi.

UMOJA WA MATAIFA WAONYA

Lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na vurugu.

“Waelekeze mizozo yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi kwa mifumo na taasisi zilizopo kwa mujibu wa Katiba ya DRC,” msemaji wake Stephane Dujarric alisema akiwa mjini New York.

MATOKEO YA KIHISTORIA

Iwapo matokeo hayo yatathibitishwa, Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru mwaka 1960.

Tshisekedi aliungana na aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Union for the Congolese Nation (UNC), Vital Kamerhe.

Katika makubaliano ya muungano wao, iwapo watashinda urais, Tshisekedi anashika wadhifa huo na Kamerhe anakuwa waziri mkuu.

Rais Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 18.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CENI, matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa Januari 15 na rais mpya ataapishwa siku tatu baadaye.

Matokeo hayo, hata hivyo yanaweza kupingwa katika Mahakama ya Katiba.

Kabila ameshaahidi kukabidhi madaraka kwa mshindi wa uchaguzi huo, jambo ambalo likitokea itakuwa ni mara ya kwanza tangu DRC kupata uhuru kutoka kwa Ubelgiji.

Kwa mujibu ya baadhi ya wachambuzi wa mambo, ushindi huo uliotangazwa na CENI, ni wa kihistoria kwa UDPS na Tshisekedi mwenyewe.

UDPS ilikuwa imejaribu kwa miaka mingi kushinda uchaguzi DRC bila mafanikio.

AFRIKA KUSINI YATAKA MATOKEO YA MWISHO

Wakati huo huo, Serikali ya Afrika Kusini, ambayo ina ushawishi mkubwa katika siasa za DRC imeitaka tume ya uchaguzi kutoa matokeo ya mwisho na kuhakikisha uhalali na kuendeleza amani na utulivu, huku ikikataa kile ilichokiita uingiliaji wa mataifa ya magharibi kwa mambo ya ndani ya DRC.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa imeipongeza DRC kwa kuendesha uchaguzi huo na kuzitaka jumuiya za kikanda na kimataifa kujizuia kutoa taarifa zisizothibitishwa na kuwaruhusu maofisa wa uchaguzi kumaliza kazi yao.

UMOJA WA ULAYA WASUBIRI RIPOTI

Umoja wa Ulaya (EU), umesema unasubiri ripoti ya tathimini kutoka timu za waangalizi zilizotumwa kusimamia chaguzi kabla ya kutoa maoni yake na imetoa wito wa utulivu wakati ukweli ukisubiriwa.

Msemaji wa EU, Maja Kocijancic alisema umoja huo umeona sehemu ya malalamiko ya upinzani kupinga ushindi wa wenzao wa kambi hiyo na hivyo unasubiri mwitikio wa timu za waangalizi ikiwamo wa Afrika.

“Kwa sasa tunachoweza kufanya ni kutoa wito kwa wadau wote wa kisiasa nchini DRC kujizuia kuchochea au kuzua aina yoyote ya machafuko na kuruhusu mchakato wa kidemokrasia uendelee,” alisema.

MATOKEO YALIVYOPOKEWA TANZANIA

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania, wamepongeza ushindi huo wa upinzani nchini DRC.

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, alisema ushindi wa Tshisekedi ambaye ni mgombea kutoka chama cha upinzani, ni hatua nzuri ya kujenga demokrasia DRC.

Alisema kwamba ushindi huo ni hatua yenye mfano katika ukanda wa maziwa makuu.

“DRC yenye matatizo na migogoro na vita, wamefika mahali wakapiga kura na kukubaliana fulani kashinda, tena mpinzani,  hiyo si hatua ndogo.

“Kuna haja ya kuwapongeza na kuwaombea wakae katika hali ya amani na maelewano kwa sababu wamefika kwenye hatua nzuri.

“Pamoja na hayo, sina uhakika kama kunaweza kuwa na visasi juu ya viongozi wa Serikali iliyopita kwa sababu hakuna tetesi ya kuwapo sababu ya kutaka kulipa visasi.

“Licha ya changamoto nyingi za kiusalama kuwapo ndani ya DRC, binafsi sioni sababu yoyote inayoweza kuchochea kuwatenganisha wananchi chini ya utawala mpya ambao unatokana na kiongozi wa upinzani.

“Uchguzi huo si tu kwamba unajenga amani zaidi ndani ya nchi hiyo, lakini pia  unawaunganisha Wakongomani upya,” alisema Profesa Baregu.

Aliongeza kwamba baada ya chama tawala kuangushwa katika uchaguzi huo, upo uwezekano rais anayeondoka madarakani, Kabila, akafanya mchezo uliowahi kufanywa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Dmitry  Medvedev ambao walibadilishana madaraka.

Hata hivyo, alisema inawezekana ikawa ni vigumu kuusoma mchezo huo kati ya Tshisekedi na Kabila.

“Katika siasa, hakuna kitu kisichowezekana, inawezekana hawa watu wana mkataba wa kuachiana madaraka, lakini kwa ujumla wamekwenda vizuri,” alisema.

Alisema Tshisekedi ambaye amerithi siasa kutoka kwa baba yake, atakuwa na mengi ya kujifunza kuendesha Serikali pia kwa kuwa ametumia muda mrefu wa maisha kuishi Ubelgiji, inawezekana akapata ugumu wa kuzisoma siasa za ndani ya DRC.

Profesa Baregu alisema kilichombeba Tshisekedi katika ushindi huo ni hamu ya Wakongomani ya kuhitaji mabadiliko.

PROFESA MPANGALA

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alipongeza ushindi huo na kusema siasa za Bara la Afrika si rahisi upinzani kushinda.

Alisema kwamba ushindi huo wa upinzani ni fundisho kwa nchi nyingine barani humu kwa sababu imezoeleka vyama vilivyopo madarakani hung’ang’ania madaraka kwa kutumia kila mbinu kuhakikisha vinashinda uchaguzi.

Pamoja na ushindi huo, alisema Tshisekedi  ana changamoto nyingi ndani ya uongozi wake kwa sababu DRC ni nchi ambayo haijawahi kupata amani kwa sababu ya vikundi vingi vya waasi na uwepo wa ugonjwa wa Ebola pamoja na mataifa makubwa kutamani rasilimali za taifa hilo.

“Kwahiyo, chama kilichoshinda kinatakiwa kiwe na misingi ya busara katika utawala na kimuheshimu Kabila kama rais mstaafu na apewe haki zake zote.

“Kiongozi mpya na chama anatakiwa kuwa na busara za waasisi wa ukombozi wa Afrika, ajiulize kwanini Mandela aliwasamehe makaburu licha ya kumfunga kwa miaka 27, walimtesa, wakawatesa wapigania uhuru, wakaua watoto, lakini hakuwa na kisasi na wazungu na badala yake aliamua kushirikiana nao.

“Serikali mpya ya DRC ina wajibu wa kuunganisha wananchi na kuweka sera zitakazobana mianya ya unyonyaji ya mataifa makubwa yanayonyonya rasilimali za taifa hilo,” alisema Profesa Mpangala.

DK. BANA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema DRC imepitia kipindi kigumu tangu ilipopata uhuru mwaka 1960 kwa kuwa haijawahi kufanya uchaguzi ambao umekidhi vigezo vya kidemokrasia.

Alisema kwamba nchini DRC kumekuwa na vipindi vya mapinduzi na mauaji, hivyo uchaguzi huu umewapa nafasi Wakongomani kuwa na rais aliyechaguliwa kwa njia ya kura.

“Kwahiyo, sitegemei rais mpya afanye maajabu kwa taifa hilo ambalo limegubikwa na hali ngumu ya mapigano ya wenyewe na lenye ugonjwa wa Ebola.

“Kwa ujumla, Tshisekedi atakuwa na changamoto nyingi ndani ya uongozi wake, hususani kuleta utaifa na hatma ya yote, Wakongo wameamua kumchagua na kinachotakiwa sasa ni kumpa ushirikiano na yeye awe tayari kuongoza kwa ushirikiano.

“Lazima pia ajue vikundi vya wapiganaji ni kwa jinsi gani ataviweka mezani kwa mazungumzo au wale wababe wa vita ajue ni namna gani atawashughulikia kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Bana.

TSHISEKEDI NI NANI?

Felix Tshisekedi ni mtoto wa mwanzilishi wa UDPS, mwanasiasa mkongwe wa upinzani, marehemu Etienne Tshisekedi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, alifariki dunia Februari, mwaka jana na kumwachia mwanae msingi wa umaarufu uliomwezesha kupanda ngazi za uongozi katika chama kirahisi na hatimaye urais.

Marafiki zake humwita kwa jina la utani ‘Fatshi’ kutokana na unene kiasi alionao na pia ni ufupisho wa jina lake Fe(lix) na (Tshi).

Kwa muda ilionekana Tshisekedi (55), jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

Novemba 11, mwaka jana, yeye, Kamerhe na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Fayulu apambane na mgombea wa serikali, Shadary.

Lakini makubaliano yao yalidumu saa 24 tu, baada ya Tshisekedi na Kamerhe kudai kushinikizwa kufikia hatua hiyo na hivyo vyama vyao kujiondoa na kujitenga na Fayulu.

Tangu baba yake Tshisekedi alipoanzisha UDPS mwaka 1982, kimekuwa kama chama kikuu cha upinzani kuanzia wakati wa utawala wa dikteta Mobutu Sese Seko, kisha Laurent-Desire Kabila (baba yake Kabila) aliyeongoza tangu 1997 hadi alipouawa mwaka 2001.

Kujiondoa kwa Tshisekedi kutoka kumuunga mkono Fayulu kulizua shutuma kwa kuugawa upinzani uliokuwa umeonesha mwanzo mzuri kwa kuungana.

Tshisekedi ni baba wa watoto watatu na yeye na Fayulu ni waumini wa kanisa moja la Kipentekoste jijini Kinshasa, huku Shadary akiwa Mkatoliki.

Tshisekedi ana stashahada katika mauzo na mawasiliano kutoka Ubelgiji, lakini wakosoaji wake hutilia shaka hilo.

Wakosoaji wake pia wamekuwa wakisema hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa uongozi.

Lakini amepanda cheo katika chama kuanzia mwaka 2008 ambao alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

Machi, mwaka jana aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama baada ya kifo cha baba yake.

Alichaguliwa kuwa mbunge 2011, akiwakilisha eneo la Mbuji-Mayi katika Mkoa wa Kasai-Oriental, lakini alikataa kuutumikia kwa kuwa hakutambua kushindwa kwa baba yake na Rais Kabila katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2011.

Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa baba yake, aliwahi kuliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) mwaka jana, kuwa akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumwajibisha Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles