23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi aingilia kati mgogoro walimu, wazazi kugombea shule

Bethsheba Wambura, Dar es Salaam

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kinyamwezi iliyopo Pugu jijini Dar es Salaam ambao walikosa nafasi katika shule hiyo na kuhamishiwa katika majengo ya Shule ya Msingi Kinyamwezi wameagizwa  kurudi katika shule yao ili kuwapisha wanafunzi wanaoanza elimu ya msingi na awali mwaka huu.

Majengo hayo ya Shule ya Msingi Kinyamwezi ambayo yalijengwa tangu mwaka 2016 yalikuwa hayajaanza kutumika kwa sababu yalikuwa hayajatimiza vigezo vya kusajiliwa kama shule kutokana na kukosekana ofisi za walimu na vyoo hivyo wanafunzi wa sekondari waliokosa nafasi walipelekwa kwa muda kusomea hapo wakati wakisubiria majengo yao kukamilika na wale wa msingi na awali wakisubiria usajili wa shule yao.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, leo Alhamisi Januari 10, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusikiliza malalamiko ya wazazi wa eneo hilo na amesema amefikia hatua hiyo baada ya kuwepo kwa mgogoro kati ya wazazi waliweka kambi katika shule hiyo kwa siku nne, walimu wa sekondari na mratibu wa elimu wa Kata ya Pugu.

Amesema katika Manispaa yake walifaulu wanafunzi 21,000 na nafasi zilizopo katika shule za sekondari ni za wanafunzi 12, 000 pekee hivyo kupelekea wanafunzi wengine kukosa nafasi za kuendelea na masomo ya Sekondari na kati ya wanafunzi walikosa nafasi ni wamo wa Sekondari ya Kinyamwezi jambo lililowalazimu kuwahamishia katika majengo hayo.

“Tuliona tukiwaacha nyumbani wanafunzi waliokosa nafasi wataenda kufanya mambo yasiyofaa na zaidi wangechelewa kuanza masomo, na tungeweza kuwapeleka shule za mbali zenye nafasi ila huko pia wangepata adha ya usafiri hivyo tukafikiria jambo la busara ni kuwapeleka katika shule ya msingi wakati majengo ya shule yao yakiendelea kujengwa,” amesema Mkurugenzi huyo.

Naye Diwani wa Kata ya Pugu, Boniventure Mfulu, amesema mgogoro wa shule hizo ulikuja baada ya wakazi waliokuwa wanakaa Kipawa kuhamishiwa huko kupisha ujenzi na upanuzi wa uwanja wa uwanja wa ndege hali iliyosababisha wanafunzi kuongezeka kuliko idadi ya shule zilizopo lakini ambapo ameshukuru Mkurugenzi kwa maamuzi aliyotoa kwani yatarudisha amani katika eneo hilo.

Awali akizungumza kwa niaba ya wazazi waliokusanyika na kuweka kambi katika shule hiyo ya msingi wa siku nne, Dennis Masanga, mkazi wa Pugu Kinyamwezi amesema wao waliamua kugomea wanafunzi wa sekondari kupelekwa katika shule ya msingi kwasababu wamekuwa wakiisubiria kwa muda mrefu lakini waliambiwa haijakidhi vigezo vya kuwa shule iweje hao wengine wapelekwe.

“Tuliandikisha wanafunzi 125 wa shule ya msingi na wanafunzi 50 wa elimu ya awali (chekechea) lakini tangu mwaka jana tuliambiwa  haijakidhi kuwa shule lakini tulishangaa wanafunzi wa sekomdari wanaletwa hapa, je hawa watoto wetu wadogo tuwapeleke wapi, “ amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles