30.5 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

UPASUAJI MARA NANE KUMSTAAFISHA TIGER WOODS

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


KILA Ufalme una mwisho wake, ndivyo ambavyo tunaweza kusema kwa sasa kwa bingwa wa dunia wa mchezo wa Golf nchini Marekani, Eldrick Tont, maarufu kwa jina la Tiger Woods.

Hauwezi kuwataja mastaa ambao wametikisa kwenye mchezo huo na ukaliacha jina la Woods, aliyeanza kucheza akiwa na umri wa miaka minne.

Kwa sasa ana umri wa miaka 41, ni wakati sahihi kwake kutangaza kutundika daluga na kuwaacha vijana wengine wanaochipukia waendeleze kuutangaza mchezo huo.

Jina la Woods limewahi kutajwa mara kadhaa kuwa ni kinara anayelipwa fedha nyingi duniania kuliko mwanamichezo yoyote kutokana na kuwa na mikataba mbalimbali.

Kwa sasa katika ramani ya wachezaji nyota wa Golf hayupo, ila limebaki jina tu, kutokana na ushindani uliopo pamoja na kusumbuliwa na matatizo ya mgongo.

Mbali na kuanza kujifundisha mchezo huo akiwa na miaka minne, lakini alipofikisha miaka 20 tayari alikuwa staa na kuanza kutwaa mataji mbalimbali.

Mwaka 1997 alitangazwa kuwa bora duniani, aliweza kudumu kwenye nafasi hiyo hadi mwaka 2010, hapo alianza kushuka kiwango baada ya kutangaza kuwa yupo kwenye mipango ya kufunga ndoa na mpenzi wake Elin Nordegren.

Hata hivyo hakudumu sana kwenye ndoa na mke huyo na baada ya kuachana kiwango chake kilizidi kushuka huku akiripotiwa kuwa anabadilisha wasichana mara kwa mara.

Mwaka 2011, nyota huyo katika orodha mpya ya wachezaji bora wa Golf alijikuta akiangukia nafasi ya 58, jambo ambalo liliwashituwa mashabiki wake wengi, lakini aliwatoa wasiwasi na kuwaambia lazima arudi katika nafasi yake.

Aliweza kupambana kwa miaka miwili na ilipofika Machi 2013 aliweza kurudi kwenye ubora wake na kushika nafasi ya kwanza, lakini alidumu hadi Mei 2014.

Kwa kuwa alikuwa anatumia nguvu nyingi katika mazoezi ili kuweza kurudisha kiwango chake, alijikuta akipatwa na maumivu ya mgongo, hivyo alilazimika kufanyiwa upasuaji 2014.

Baada ya hapo alikaa sana nje ya uwanja kutokana na kuugua, baada ya kurudi viwanjani alijikuta akidondoka kutoka nafasi ya kwanza hadi 104.

Ilipofika 2016 bado Woods alikuwa anashiriki michuano huku akiwa mgonjwa hivyo alikuwa anashindwa kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali na kujikuta akishika nafasi ya 500 kwa ubora duniani.

Hapo ndipo ndoto zake za kurudi kwenye nafasi ya kwanza au 10 zikaanza kugonga mwamba hasa kutokana na hali yake.

Mapema mwaka jana alijipa matumaini ya kurudi kwenye ushindani kutokana na hali yake kukaa vizuri, lakini bado tatizo la mgongo lilionekana kuzidi siku hadi siku na kujikuta akirudi hospitali kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Hadi kufikia sasa amefanyiwa upasuaji wa mgongo mara nane, hivyo amethibitisha kuwa hawezi kushiriki tena mashindano ya Golf.

“Sijui hatima ya afya yangu kwa siku zijazo, sijui kama nitaweza kukamilika kwa asilimia 100 na kuweza kurudi tena kwenye ushindani, nimefanyiwa upasuaji mara nane, lakini nitajaribu kupambana kuona kama kutakuwa na uwezekano wowote japokuwa ni asilimia ndogo sana.

“Nadhani umri wangu unachangia kuwa katika hali hii, hakuna mchezaji yeyote ambayo ana umri wa miaka 40 akawa na uwezo kama alivyokuwa kwenye miaka ya 20, kwa umri nilionao sasa siwezi kupiga mpira na ukaenda umbali wa zaidi ya mita 60,” alisema Woods.

Bingwa huyo mara ya mwisho kuonesha uwezo wake na kutwaa taji ilikuwa mwaka 2008, lakini kwa kipindi cha miaka miwili iliopita amefanikiwa kucheza mashindano sita tofauti huku akijaribu kupambana na hali yake.

“Nadhani mwisho wangu wa kushiriki mashindano makubwa umefikia mwisho, nilianza kupenda Golf tangu nikiwa na umri wa miaka minne, hivyo naweza kusema mchezo huo ni sehemu ya maisha yangu na nitaendelea kuwa hapo hadi mwisho wa maisha yangu, sio lazima nicheze tena, lakini naweza kutoa mchango wangu kwa namna tofauti.

“Afya yangu kwa sasa sio mbaya, inaendelea vizuri lakini ninaamini haifahi kurudi tena viwanjani, ila naweza kuwasikiliza madaktari wangu nini watakisema kutokana na hali yangu ilivyo,” alisema Woods.

Woods ataendelea kukumbukwa duniani katika mchezo huo pamoja na ustaa wake kwenye idara ya michezo duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles