23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

UNAWEZA KUWA NA FURAHA KWA KUBADILI MTAZAMO WAKO

Na Christian Bwaya,

HUENDA unaposoma makala haya machozi yakakudondoka kwa sababu umeachwa na mpenzi wako. Mtu uliyempenda kwa moyo wako wote ameamua kukudhalilisha na kukuacha bila kujali hisia zako. Kujisikia vibaya katika mazingira kama haya,  inaeleweka.

Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kuwa katika maisha wakati mwingine tunakutana na wasaliti. Tunaishi na watu ambao tangu mwanzo wa uhusiano pengine wanafikiri namna watakavyotuumiza. Hiyo ndiyo furaha yao. Usiwaruhusu watu wa namna hii kukunyang’anya amani yako.

Kubali kuwa maisha ndivyo yalivyo. Sisi binadamu hatuwezi kubadili mambo mengi tunayokutana nayo. Hata kama tungekuwa na tahadhari namna gani, wakati mwingine hatuwezi kujua yatakayotokea katika siku za mbeleni. Mabaya yanapotokea tunajifunza kuyakubali na maisha yanaendelea.

Najua pengine unasoma ukurasa huu ukinishangaa nisivyoelewa hali yako. Umefukuzwa kazi muda si mrefu na huna mahali pa kwenda. Umefiwa na mtu umpendaye na hivi sasa huelewi kwanini imekuwa hivyo. Pengine unamlaumu Mungu kwa kuruhusu mabaya yote hayo yakupate. Naelewa.

Lakini fahamu kuwa katika maisha si lazima wakati wote mabaya yawapate wabaya. Wema nao hupatwa na mabaya na wabaya nao hupatwa na yaliyo mema. Ndio maisha.

Maisha yametuaminisha kuwa ukitenda mema, utalipwa mema. Ukiwa mtu mwema, basi mema yatakutokea. Dhana hii inatuaminisha kuwa kila mtu hupata malipo sawia na kile anachostahili. Kwa sababu hiyo, tunapopatwa na mambo magumu tusiyoyatarajia,  tunasikitika. Tunakuwa na maswali mengi kwanini Mungu anaruhusu watu wema kama sisi kupatwa na mabaya.

Kama tulivyotangulia kudokeza awali, sisi si watu maalumu. Hatuwezi kukwepa kupatwa na mabaya. Kama ambavyo watu wengine wanavyoweza kupatwa na majanga nasi pia tunaweza kukutana na yale yale. Hakuna sababu ya kuona uovu wako usiokuwapo kwa sababu tu umekumbana na mikasa migumu katika maisha.

Huenda umefiwa na mtu umpendaye. Kifo cha mtu wa karibu kinaumiza. Lakini je, unaweza kubadili ukweli huo kwamba umpendaye amefariki? Kwamba kuendelea kuishi maisha ya majonzi kunasaidia? Hapana. Kwamba masikitiko na majonzi yanawezi kugeuza chochote baada ya umpendaye kutangulia mbele ya haki maana yake ukubali ndivyo maisha yalivyo. Kifo ni sehemu ya maisha.

Pengine wewe ni mwanafunzi. Unaposoma maneno haya unasema; “ungejua nimefeli mtihani wangu na sasa nalazimika kurudi nyumbani kwa aibu!” Naelewa.

Matukio mabaya katika maisha yanaathiri namna tunavyojiona; yanaathiri kujiamini kwetu; yanatuumiza kwa sababu yanatufanya tuwe na wasiwasi na uwezo tulioamini kuwa tunao.

Lakini ndivyo yalivyo maisha. Siku zote yana pande mbili. Upande wa kwanza ni mtamu. Tunapokuwa kwenye kipindi kitamu tunafurahi. Tunafurahia maisha. Tunajiona watu maalumu tuliobarikiwa.

Punde tunajikuta kwenye upande wa pili. Tunajikuta tukipita kwenye nyakati zenye sura chungu na mbaya. Tunasikitika. Tunaugua. Hakuna tunachokibadili.

Hata hivyo, pande hizi mbili za maisha ndizo zinazofanya maisha yawe vile yalivyo. Unaweza kuufurahia utamu wa maisha kwa sababu unaujua upande mchungu wa maisha. Unaweza kufurahia urafiki mzuri kwa sababu unajua uchungu wa uadui.

Ndio kusema unapopita kwenye kipindi kigumu, huo si mwisho wa maisha. Kipindi kitamu kiko njiani.

Tunahitaji kubadili mtazamo tulionao kuhusu maisha. Tusiruhusu upande mbaya wa maisha kutunyang’anya furaha yetu. Tusiruhusu watu kutunyang’anya furaha yetu.

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles