30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

WASAMEHE WAZAZI WAKO ILI UOKOE KIZAZI CHAKO – 2

Na Christian Bwaya,

MSINGI wa tabia za mzazi unaweza kuwa ama kuiga yale yaliyofanywa na wazazi wake au kupinga makosa waliyoyafanya wazazi wake. Tuliona kuwa mzazi anaweza kuwa na misimamo fulani fulani ambayo kimsingi inajaribu kuendeleza misimamo aliyoona kwa mzazi wake au kinyume chake.

Tulitoa mfano wa tabia ya kukemea watoto. Wazazi huwafokea watoto kwa kuamini kuwa bila kufoka mambo hayaendi. Hata pale ambapo kufoka hakuoneshi matokeo yoyote ya maana bado mzazi anaamini hiyo ndiyo njia sahihi.

Lakini, wakati mwingine mzazi aliyelelewa na wazazi wenye tabia ya kufoka bila sababu anaweza kufanya kinyume chake. Hutokea mzazi huyu akawa na tabia ya kupuuzia makosa ya watoto kupita kiasi.

Upole huu ni namna ya nafsi kupinga malezi ya kukemewa isiyostahili. Mzazi wa namna hii ‘hulipa kisasi’ kwa kunyamazia makosa ya wazi ya watoto. Anachukulia kukemea makosa yanayofanywa na watoto kama kuendeleza utamaduni ule ule ambao haukuupenda kwa wazazi wake.

Kwa kuwa tumeona yale uliyoyaona yakifanywa na wazazi wako, kwa kiasi kikubwa, yanaweza kuongoza namna unavyowalea wanao; unahitaji kuchukua hatua za kuachilia yote yale uliyowahi kutendewa ukiwa mtoto.

Samehe makosa ya wazazi

Pengine ni ukali waliokuwa nao wazazi wako; pengine uliumia kwa wazazi wako kupeana talaka hali ukiwa mdogo; pengine mzazi mmoja wapo alipanda chuki kwako dhidi ya mzazi mwenzake.

Unahitaji kuamua kusamehe. Msamaha wa dhati kwa wazazi unaweza kugeuza tabia yako ukiwa mzazi. Fanya uamuzi wa kuwasamehe wazazi wako.

Unaweza kuwasamehe wazazi kwa kuwasiliana nao. Njia moja wapo inayoshauriwa ni kuwaandikia barua wazazi hata kama wametangulia mbele ya haki. Andika barua kueleza hisia zako.

Barua hii si lazima waipate. Lakini kwa kuiandika itakusaidia kutafakari maisha yako na namna yalivyoathiri mwenendo wako leo. Kufanya hivyo kutakusaidia kufanya uamuzi wa kufunga mlango wa uchungu uliojijenga ndani yako na kuanza maisha mapya.

Katika barua jaribu kukumbuka matukio unayoyakumbuka ambayo pengine yalitesa ufahamu wako ukiwa mtoto. Labda wazazi walitumia lugha za vitisho. Labda walijenga mazingira ya hofu. Labda ni migogoro yao ya ndoa iliyoathiri mtazamo wako dhidi ya uhusiano wa ndoa. Andika barua ya msamaha na amua kuachilia. Fanya hivyo ukielewa kuwa hakuna mzazi ambaye angependa kuwatendea watoto yale ambayo yeye mwenyewe asingependa kutendewa.

Azimia kufanya tofauti

Baada ya kuwa umetambua maeneo ambayo wazazi wako hawakufanya vyema na ukasemehe, unahitaji kukusudia kwa dhati kuenenda tofauti.

Unafanya tofauti kwa kuelewa athari ya yale uyatendayo kama mtoto kwa tabia ya mwanao. Mtoto huiga mengi uyafanyayo. Kwamba tabia zako zina nguvu ya kujenga utamaduni usiokusudiwa utakaofuatwa na wanao.

Kwa mfano; namna unavyoongea na mke/mume wako; namna unavyostahi makosa yake mbele ya wanao; namna unavyokasirika anapokukosea; namna unavyompa/unavyopokea maagizo anayokupa; namna unavyowasema watu wasiokuwapo hapo nyumbani na maeneo mengine. Haya yote yana nafasi kubwa ya kuumba utamaduni endelevu kwa mtoto.

Vile unavyoonekana na kufanya kwa kiasi kikubwa hujenga taswira ya maisha ambayo ama mtoto huyaamini au kushindwa kuyaamini. Kwa kuelewa hivyo, maana yake unahitaji kukataa kuwa taswira ya mzazi anayesaidia mtoto kujifunza tabia zisizomfaa kwa maisha yake ya baadae.

Itaendelea…

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles