24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UMMA UNAHITAJI MAJIBU YA KINA TUKIO LA MOTO MBEYA

MLOLONGO wa matukio ya moto mkoani Mbeya, unazua maswali mengi kuliko majibu.

Katika toleo la jana la gazeti hili, tulichapisha habari juu ya tukio baya la moto lililosababisha soko la Sido mkoani Mbeya kuteketea na kuacha vilio na simanzi kubwa kwa wafanyabiashara ambao wamepoteza mali zao.

Tukio hili, limezidi kuweka rekodi ya matukio mabaya ya moto ambayo kwa miaka kadhaa sasa yamekuwa yakitokea mkoani Mbeya na hakuna mtu anayetiwa mbaroni kuhusika au chanzo chake kuelezwa vizuri.

Hali hiyo, imesababisha kuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa matukio hayo.

Inaonekana sasa inataka kuwa kama mazoea, kwa sababu hata watu ambao wamepewa dhamana ya kulinda masoko hayo, wanashangaa namna ambavyo moto huo hutokea.

Tukio la kuungua kwa soko la Sido, limeibua mjadala mzito kutokana na mazingira yake.

Wengi wanadai kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo hujuma katika tukio hilo kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha soko hilo lilinusurika kuteketea kwa moto mara mbili kati ya mwaka 2011 na 2014.

Lakini pia kumekuwapo na madai kuwa inawezekana tukio hilo limefanywa na kikundi cha watu kwa sababu zao wanazozijua.

Hatuwezi kukubali au kukata lakini tunaamini mamlaka husika zitakuja na majibu sahihi juu ya tukio hili.

Tukio hilo limewaacha wafanyabiashara zaidi ya 3,000 hawana cha kufanya.

Tunaamini kama kungekuwa na vifaa vya kuzimia moto, watu waliokuwa karibu wangeweza kwa namna moja au nyingine kupunguza tatizo.

Ukosefu wa miundombinu ya maji na umakini mdogo wa watendaji wa Halmshauri ya Jiji la Mbeya, inawezekana kuchangia uwapo wa matukio ya aina hii.

Tulitegemea kutokana na kuwapo matukio haya mara kwa mara, uongozi wa Jiji la Mbeya ungekuwa umejifunza jambo, lakini tunaona bado umelala usingizi wa pono.

Haiwezekani watu waliokabidhiwa dhamana wanaendelea kuingia ofisini kila siku bila kuwa na mipango makini.

Tunasema hivyo, kwa sababu kuna kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambacho kimekabidhiwa dhamana kubwa juu ya majanga haya.

Tunajiuliza, zimamoto mkoani Mbeya wapo makini katika kazi yao?

Sisi MTANZANIA, tunasema kamati iliyoundwa kuchunguza tatizo hili ije na majibu ya msingi ambayo kwa kweli yatatoa ufumbuzi wa matatizo haya, itoe dira, mwelekeo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Tunaamini itakuja na majibu ambayo bila shaka hayatazua maswali magumu kwa wakazi wa Mbeya, ambao kwa miaka mingi wamekosa majibu kutoka kwa vyombo vya dola yanapotokea majanga ya aina hii.

Hatutarajii porojo na kama watakuwapo watu waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Tunamalizia kwa kuishauri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Zimamoto kuendesha ukaguzi wa kina kuona kama wahusika wamefunga vifaa vya kuzuia moto na miundombinu mingine katika maeneo kama haya ya masoko na mengine, ili kuepuka majanga makubwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles