23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Umiliki ardhi ni donda lisilopona kwa wanawake vijijini

Ashura kazinja, Morogoro

MBALI na sera na sheria kumruhusu mwanamke kumiliki ardhi, bado kumekuwapo vikwazo mbalimbali katika jamii vinavyofanya sheria hiyo kutotekelezeka na hivyo mwanamke kubaki kuwa tegemezi.

Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu, na mwanamke ndiye anayechangia asilimia 80 ya ushiriki kwenye kilimo, lakini imekuwa tofauti katika kumiliki ardhi ambapo tafiti zinaonesha wanaomiliki ardhi ni asilimia 24 tu, jambo  ambalo haliridhishi.

Changamoto kubwa inayomfanya mwanamke kukosa haki ya kumiliki ardhi katika jamii inatokana na mila potofu na uelewa mdogo miongoni mwao juu ya haki yake hiyo ya msingi.

Sababu nyingine ni uoga na kutokuwa na uwezo wa kugharimia kesi ili kujipatia haki.

Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Mkambarani, Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Theresia Berege, anasema haki ya mwanamke kumiliki ardhi bado ni changamoto kubwa, hasa kwa wajane ambao wamekuwa wakinyang’anywa mali zilizoachwa na waume zao ikiwamo ardhi ambayo ndio kitega uchumi kikubwa vijijini.

Berege anaiomba Serikali kuanzisha baraza la ardhi katika Kijiji cha Mkambarani ili kuwawezesha wanawake kushiriki katika kutoa uamuzi, pia kupeleka madai yao na kupatiwa ufumbuzi.

Anasema pia ni vyema mabadiliko yakafanyika katika hati za kimila na kutamka wazi kuwa umiliki wa ardhi kwa mume na mke kuwa wa pamoja ili kuepuka migongano pindi mmoja anapotangulia mbele za haki na hivyo ndugu kutaka kupora mali.

“Kwa vijijini changamoto hii bado ipo sana, mali nyingi zimekuwa zikiandikwa kwa jina la mwanamume, ikitokea akatangulia yeye inakuwa shida kwa mke. Mimi mwenyewe yalinikuta, lakini kwa sababu nilikuwa na uelewa nikaenda kudai haki yangu mahakamani, lakini wanawake wengi hawana huu uelewa,” anasema Berege.

Anatoa wito kwa vyombo vya uamuzi ikiwamo mahakama, kumwangalia zaidi mwanamke pale anapofungua kesi kwa ajili ya madai  ya mirathi au ardhi, kwamba kesi hizo zisichukue muda mrefu ili kupunguza gharama kwa mhusika.

“Hizi kesi ziendeshwe haraka, kwani utakuta kesi inachukua muda mrefu hadi miaka minne hatimaye mwanamke anakata tama. Waharakishe ili kuwapunguzia gharama za kesi, kutengenezwe utaratibu utakaomfanya aifikie haki yake kwa haraka na gharama nafuu,” anasisitiza.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mkambarani, Fatuma Gowelo, anaeleza adha anayokutana nayo yeye na ndugu zake baada ya kufiwa na wazazi wote wawili.

Anasema baada ya vifo vya wazazi wao, baba zao wadogo walijitokeza kudai mali likiwamo shamba lenye ekari 10 wakitaka liuzwe ili wagawane.

Gowelo anasema uamuzi wa kuuza shamba hilo umekuwa mgumu kwao kwa sababu wanalitegemea kwa ajili kujipatia riziki.

Anasema wadogo zake bado wadogo wanasoma shule ya msingi na wengine sekondari na hawana kitu kingine cha kuwawezesha kuishi hasa ukizingatia kuwa ngugu zao upande wa baba hawawasaidii kwa jambo lolote.

“Hatuna mzazi hata mmoja, alianza kufariki baba akafuata mama ambaye amefariki mwezi uliopita.

“Kifo cha mama naweza kusema kimetokana na baba yangu mdogo ambaye baada ya baba kufariki, akamleta mtoto nyumbani akidai ni wa baba alimzaa nje ya ndoa.

“Mtoto yule alipokuja nyumbani akamshitaki mama mahakamani ili kudai mirathi likiwamo shamba letu, mama akapata presha akafariki na sasa tumebaki wenyewe hatujui hatma yetu,” anasema Gowelo.

Akizungumzia suala la migogoro ya ardhi, Katibu wa Chama cha Taarifa na Maarifa, Kijiji cha Mkambarani, Amina Simba, anasema kata hiyo inachangamoto kubwa ya ardhi kutokana na kukosa mabaraza ya kutatua kesi zao na hivyo wananchi wengi hukimbilia katika kituo hicho kutafuta msaada.

Anasema wanawake wengi hawana uelewa wa namna ya kupata haki zao, huku mfumo dume nao ukiwa umeota mizizi na kumfanya mwanamke hata akinunua shamba au kitu chochote ni lazima ataandika jina la mwanamume ili kulinda ndoa yake.

Anaiomba serikali kusimamia suala la watoto wa nje ya ndoa, kwa sheria kutamka wazi kuwa kila mtoto wa nje arithi kwa mama yake ili kuondoa adha wanayokutana nayo wanawake walioko ndani ya ndoa iwapo baba atatangulia mbele ya haki.

Kwa kuliona hilo, Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na masuala ya haki za ardhi (Landesa) kwa kushirikiana na mashirika mengine 25 wameamua kuanzisha kampeni ya ‘Linda Ardhi ya Mwanamke’ itakayochukua takribani miaka 12 ili kumsaidia mwanamke kupata haki ya kumiliki ardhi.

Mwanasheria wa Landesa, Godfrey Massay, anasema  mwanamke akiwezeshwa kumiliki ardhi atakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa viwanda na kwamba ni muhimu akapewa nafasi kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Sheria za ardhi ni nzuri, lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo, mwanamke na mwanamume wote wana haki ya kumiliki ardhi kisheria, lakini sheria za kimila nyingi ni kandamizi ,” ansema Massay.

Anasema kwa upande wa mwanamke, sheria za kimila zimeonesha kuwa na matatizo, hali inayosababisha kuogopa kwenda mahakamani kudai haki zao huku wengine wakiwa hawazijui, kushindwa kumudu gharama za kuendesha kesi na hata kuogopa kutengwa na jamii.

Naye mchambuzi masuala ya ardhi kutoka Landesa, Khadija Mrisho, anasema kampeni ya ‘Linda Ardhi ya Mwanamke’ inalenga kumpatia haki yake ya kumiliki ardhi kwa kuhakikisha utekelezaji wa sera na sheria unawiana na changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi.

“Takribani miaka 19 na zaidi  sheria ya ardhi ya vijiji ipo, lakini je, ni wanawake wangapi wanaomiliki ardhi au kupata nafasi ya kuhudhuria katika mabaraza ya mashauri katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kijiji?’ anahoji Mrisho.

Anasema: “Ukimpa mwanamke ulinzi katika ardhi ataangalia masuala ya chakula, watoto, afya na elimu, kwahiyo utu wake na haki zake vinalindwa huku amani na upendo vikitawala katika familia.”

Anazitaja baadhi ya changamoto zinazomzuia mwanamke kupata haki  ya kumiliki ardhi kuwa ni utekelezaji mdogo wa sera na sheria, kutokuwapo utashi wa kuzitambua haki za mwanamke kumiliki ardhi na kuwepo kwa mila na desturi zinazotekelezwa zaidi katika jamii inayoishi vijijini.

“Ardhi inatajwa kama kitu cha ziada, zaidi wanasisitizia ujasiriamali na vikoba, kwanini ardhi isiwe kitu kikuu cha kumkwamua mwanamke kutoka katika umasikini? Tunataka jamii ambayo wanawake na wanaume wanakuwa na uwezo wa kupata na kumiliki ardhi kwa usawa kabisa,” anasisitiza Mrisho.

Kwa upande wake mmoja wa Wakurugenzi Landesa, Edda Sanga, anasema kampeni hiyo ni ya kipekee kutokana na kuwashirikisha wadau wengi ikiwamo Serikali, wanajamii na mashirika mengine na kwamba imekuja kwa wakati mwafaka.

“Kuna umuhimu sasa wa kumuona mwanamke ananyanyuliwa, anashiriki na kushirikishwa na kufanya uamuzi katika masuala yanayohusu ardhi na vyote vinavyotoka ardhini” anasema Sanga.

Ni wazi kampeni hii ya Linda ardhi ya mwanamke itakuwa yenye manufaa kwa wanawake wengi hususani wa vijijini, kwa kupatiwa elimu itakayowapa uelewa na kuwawezesha kumiliki ardhi itakayo wakomboa kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,636FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles