26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Uoni hafifu chanzo cha ajali nyingi barabarani

AVELINE KITOMARY

JAMII nyingi hasa za Kiafrika imekuwa haioni au kutambua magonjwa ya macho kama yana athari kubwa kama yalivyo mengine yanayoikabili jamii.

Aidha, kuna imani imejengeka katika jamii kuwa kuvaa miwani ni kuharibu macho kitu ambacho madaktari bingwa wanasema sio kweli.

“Yaani mimi nakaa darasani miaka zaidi ya saba nikisomea kuhusu macho tu anakuja mgonjwa nampima nagundua kuwa tatizo lake linahitaji miwani, lakini baada ya kumpa anaenda huko mtaani watu wengine wanamwambia inaharibu macho, anaitupa anakaa bila kuivaa.

“Kinachonipa shida zaidi kuna watu hawataki kabisa kuleta watoto wao hospitali kwa madai kuwa mtoto akipewa miwani anaharibika, sijui ni nani anapotosha jamii kuhusua suala hili,” anasema Dk. Cprian Ntomoka ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Macho kutoka Hospiali ya CCRBT.

Hali ya matatizo ya macho inazidi kuongezeka kila siku kutokana na jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha, lakini asilimia kubwa ya magonjwa ya macho yanaweza kutibiwa kwa njia mbalimbali.

Takwimu za kidunia zinaonesha kuwa takribani watu bilioni 1.3 wanasumbuliwa na matatizo ya macho huku hapa nchini makadirio yakiwa ni milioni 1.8, sababu kubwa ikiwa ni afya ya macho kuwa na mgogoro.

Takwimu zilizotolewa na CCBRT katika siku ya maadhimisho ya afya ya macho duniani Oktoba 10 ugonjwa wa macho unaoongoza ni mtoto wa jicho kwa asilimia 39, upungufu wa macho kuona kwa asilimia 24.

Mengine ni kama shinikizo la jicho asilimia  18, magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, presha, mafuta mengi haya yanasababisha madhara kwa asilimia 10 pia kuna umri kwenda hasa uzee inachukua asilimia 18.

Licha ya ongezeko hilo madaktari wamesema kuwa asilimia kubwa ya watu hawajitokezi kupima afya ya macho hivyo huenda tatizo likawa kubwa zaidi kuliko namba zilizotolewa.

Dk. Ntomoko anasema matatizo ya macho pia yanaweza kuwa sababu ya kutokea kwa ajali za barabarani kutokana na madereva wengi kuendesha magari bila kupata vipimo sahihi vya macho.

Kwa mujibu wa Dk. Ntomoka kati ya wagonjwa 10 waliofika katika kliniki yake kwa siku moja wakiendesha gari watatu wanakutwa wanatatizo la afya ya macho.

“Watu wengine wanakuja wakiwa na uoni hafifu lakini anakuja akiendesha gari na ana leseni hao wapo wanakuja hospitalini ninampima lakini wanauoni ambao hauruhusu kabisa kuendesha.

“Kwa sababu sasa kuna mabadiliko zamani tulikuwa tunasema matatizo ya macho hayaui serikali wakaweka nguvu kwenye magonjwa yanayoua kama Ukimwi, afya ya mama na mtoto, lakini kwenye macho wamesahau huku watu wengi wakiendelea kupata madhara,” anasema.

Dk. Ntomoka anabainisha kuwa hata ajali inapotokea mamlaka husika huwa haziendi kupima uoni wa dereva kitu ambacho sio sahihi kwani hata uoni hafifu unaweza kusababisha ajali.

 “Ulishawahi kuona ajali ikitoke polisi wakawahi kumpima dereva macho, mara nyingi wanakimbilia kupima ulevi lakini hawapimi afya ya macho hawajui kama hata afya ya macho inachangia kusababisha ajili barabarani kwa sababu kuna watu hawaelewi wanaendesaha gari hawaoni vizuri na utakuta mtu kama huyo alishawahi kupima sehemu akaambia avae miwani akaacha kuvaa.

“Watu wengine wamekuwa wabishi kuvaa miwani na kwa sasa matatizo ya kuvaa haya yanashika namba mbili katika magonjwa ya macho kwa asilimia 24.

“Wagonjwa wote ninaowaona, watatu kati ya kumi wanashida inayotibiwa na miwani lakini wanatembea barabarani na wanakwambia wanaona lakini kitaalam uoni wao ni hafifu, ni sheria kupima macho kabla ya kupata leseni ila wapo wengine wanafoji vipimo kwa wahuduma wa afya wasio waaminifu.

“Wengine wanafanya kwa sababu hawajui umuhimu wa kupima afya ya macho waamke wafanye vitu kwa usahihi, dereva usikubali kuendesha chombo cha moto bila kuhakikisha unapima afya ya macho ili kuzuia ajali barabarani,” anasisitiza.

Anaongeza: “Nawaambia hii ni hatari kwa watumiaji wa barabara, vyombo husika vifuatilie kwa undani kuhakikisha afya ya macho ni namba moja katika vipimo, wawe na uhakika kuwa wanaoendesha magari wafanyiwe uchunguzi na madaktari wa macho. Wapo watu ambao macho yao yanashida ya kutofautisha rangi pia, hawa nao wanapaswa kumuona mtaalamu wa macho asaidiwe,” anashauri Dk. Ntomoka.

UVAAJI MIWANI KIHOLELA 

Dk. Ntomoka anasema kuwa watu wanaovaa miwani kiholela wako hatarini zaidi kupata magonjwa  ya macho kwa sababu huathiri mishipa ya macho.

 Anabainisha kuwa athari kwenye mishipa ya macho husababisha uoni hafifu au uwezo wa macho kuona.

“Kuna watu huwa wanapenda kuvaa miwani bila hata kujua madhara yake, nataka niwaambia kuwa miwani yoyote utakayovaa inamadhara kwa afya ya macho kwa sehemu kubwa.

“Uvaaji holela wa mewani husababisha mishipa ya macho kuharibika na hii mara nyingi inapelekea uoni hafifu hapo ndo matataizo ya macho yanapoanza  kwa baadhi ya watu,” anaeleza Dk. Ntowoka.

Kwa mujibu wa Dk. Ntowoka, asilimia 24 ya matatizo ya macho yanatokana na uoni hafifu baada ya mishipa ya macho kuathirika ambapo moja ya chanzo chake huwa ni uvaaji holela wa miwani bila kushauriwa na wataalamu.

Anaishauri jamii kuhakikisha watu wanapima macho kabla ya kuvaa miwani, ili kujua kiwango cha matatizo yao ndipo apatiwe inayomfaa.

“Nawashauri watu kabla hawajavaa miwani wakapime afya ya macho ili daktari aweze kumpa ile inayoendana na tatizo lake, uvaaji wa holela unaweza kuathiri zaidi macho yako,” anashauri.

MATATIZO YA MACHO KWA WATOTO

Dk. Ntomoka anasema zipo sababu kadhaa za watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo ya macho zikiwamo za kuzaliwa nazo na baada ya kuzaliwa.

Anasema kwa mwaka huu, watoto 200 wamefanyiwa upasuaji wa macho.

“Kuna sababu ambazo huwafanya watoto wazaliwe wakiwa na matatizo ya macho,  ambazo nyingine ni za kimaumbile mfano presha ya macho kwa mtoto hutokea kama anavyozaliwa na ulemavu. Kuna ugonjwa wa mtoto wa jicho ambao mtoto anaweza kuzaliwa nao, kupata maambukizi akiwa tumboni kutoka kwa mama aliyeugua rubella, kaswemde, Ukimwi na mengine.

“Wengine  wanakuja wakiwa na shida ya mtoto wa jicho, hawa huja kila wiki. Mwaka huu hadi kufikia sasa watoto 200 wamefika hospitalini ambapo kati yao asilimia 40 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho, wengine ni makengeza na mzio ambao unatokana na mazingira yanapomkataa mtoto.

“Wapo watoto wanaotibiwa kwa dawa na wengine kwa upasuajia. Mtoto anatakiwa atibiwe mapema kwa sababu akiwa mdogo mfumo wake wa jicho unakuwa haujakomaa hivyo ni vizuri wakawahi kupata matibabu,” anaeleza.

VITU HATARISHI KWA MACHO

Kwa mujibu wa Dk. Ntomoka, matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali vinaumiza macho. Hii ni kwa sababu uteute unaolainisha macho unakauka, na endapo macho yakiwa makavu yanaweza kuwasha, kutoa machozi, kuumia na wakati mwingine kuwa mekundu.

“Hii tunaita ‘Computer Vision Syndroms’ ni mkusanyiko wa usumbufu ambao mtu anapata kutokana na matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali.

“Ni changamoto kubwa, tunapokea wagonjwa wengi wanaofanya kazi za kutumia kompyuta huwa wanakuja wakilalamika kuumwa macho. Ni muhimu watu wakajua kuwa matumizi ya muda mrefu ya kompyuta, simu na vifaa vingine vyenye nwanga  mkali ni hatari kwa macho,” anabainisha Dk. Ntomoka.

Anaeleza kuwa katika kliniki yake anawaona wagonjwa watano hadi 10 kwa siku moja, ambao wamepata madhara ya macho kutokana matumizi ya vitu vyenye mwanga mkali.

“Madhara yanaweza yasionekane kwa sasa ila baada ya miaka kadhaa ukaanza kuumwa macho, katika kliniki yangu napata watu wengi wenye tatizo hilo. Kila siku naona wagonjwa 40 ambapo kati yao watano hadi 10 wanakabiliwa na matatizo hayo,” anafafanua.

Dk. Ntomoka anawataka watu kufata ushauri wa matumizi sahihi wa vifaa vyenye mwanga kama kupunguza mwanga na kupumzisha macho kwa dakika 20 kila baada ya saa moja.

“Watu wapate ufahamu juu ya matumizi sahihi ya kompyuta ili wasiweze kupata matatizo ya macho, wafate ushauri wa kutumia simu janja, kompyuta, TV, Tablet na zingine kama watu wanahitaji ushauri waende kwa madaktari wa macho ili waweze kushauriwa.

“Pia ni muhimu kupumzisha macho kwa  kila baada ya dakika 20 hadi 30 au kuvaa miwani inayochuja kiasi cha mwanga,” anashauri Dk. Ntomoka.

Dk. Ntomoka anasema watu wazima mara nyingi huugua macho kutokana na umri kuwa mkubwa au kusumbuliwa na baadhi ya magonjwa.

“Watu wazima asilimia 75 ya ulemavu wa macho unasababishwa na matatizo yanayozuilika na asilimia 40 inasababishwa na mtoto wa jicho. Sababu nyingine ni umri kuwa mkubwa, wengi hupata madhara kuanzia miaka 60. Pia kuna magonjwa yanayoathiri macho kama kisukari, wengine ni kuumia,” anabainisha Dk. Ntomoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,631FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles