23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

UKISTAAJABU YA FURY UTAYAONA YA CHEKA

francischeka2

Na MARTIN MAZUGWA

OKTOBA  29, 2016, macho na masikio ya wapenzi wa mchezo wa masumbwi yalikuwa yakisubiri kwa hamu kushuhudia pambano kali na la aina yake baina ya mabingwa wawili wa  uzito wa juu duniani, Mwingereza  Tyson Fury dhidi  ya raia wa Ukraine, Wladimir Klitchko.

Wawili hao walitarajiwa kupanda ulingoni kuwania mikanda ya WBA pamoja na WBO, pambano ambalo lilipangwa kufanyika katika Ukumbi wa Manchester Arena, uliopo katika Jiji la Manchester, nchini England.

Pambano hilo lilikuwa la marudiano la kisasi, ambapo Wladimir ambaye ni mshindi wa medali tatu za dhahabu za mashindano ya Olimpiki pamoja na mikanda mitatu ya WBO, WBA pamoja na WBC, alitaka kuudhihirishia umma wa wapenda masumbwi kwamba alipoteza kizembe mchezo dhidi ya Fury.

Wladimir, mwenye rekodi ya kushinda mapambano 64, huku akipoteza manne pekee, alikuwa kwenye maandalizi makali ya kumvaa Mwingereza huyo ambaye alipoteza mikanda yake baada ya kubainika alitumia dawa za kuongeza nguvu.

Bila ya kutarajia wakati akiendelea na maandalizi, Fury alitangaza kuahirisha pambano hilo kwa madai kuwa hakuwa fiti kupanda ulingoni dhidi ya mbabe Klitschko, ambaye alikuwa na shauku ya kulipa kisasi dhidi yake.

“Hali yangu  siyo nzuri, hivyo siwezi kupanda ulingoni dhidi ya Klitschko,” alisema Fury, alipokuwa anafanyiwa mahojiano na kituo cha Sky Sports cha nchini England.

Baadaye alitangaza kuwa amepata majeraha ya enka ambayo asingeweza kupanda ulingoni akiwa na majeraha.

Fury, mwenye umri wa miaka 28, katika pambano  lake la kwanza  dhidi ya Wladimir, lililofanyika Novemba mwaka juzi, alishinda kwa pointi.

Katika mahojiano yake na waandishi wa habari, Fury alisema kuwa Klitschko amepigwa na bonge la mtu.

Wakati hayo yakimalizika kwa wababe hao, nchini Tanzania Desemba 25, mwaka huu katika Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam, jambo kama hili lilijitokeza baina ya Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ dhidi ya Francis Cheka, ambapo pambano hilo liliahirishwa kutoka na promota kudaiwa kushindwa kukamilisha malipo.

Pambano hilo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kwa zaidi ya miezi mitatu na wapenda masumbwi, ambao walitaka kuona nani zaidi kati ya wababe hao ambao wamekuwa wakitambiana.

Kwa upande wa Dulla, alisema kuwa jambo hilo limemuumiza kwa kiasi kikubwa, kwani ametumia gharama kubwa katika maandalizi, ikiwamo kwenda kuweka kambi nchini Urusi.

Pia alisema kuwa, lengo lake lilikuwa kuangalia ubora wake kwa mkali huyo mwenye rekodi ya aina yake kwenye mchezo wa masumbwi nchini.

Aidha, kwa upande wa Cheka, alisema kuwa imekuwa tabia ya mapromota hapa nchini kuandaa mapambano pasipo maandalizi na kuwafanyia dhuluma, hivyo kwa kuwa amewahi kufanyiwa jambo hilo hawezi kurudia makosa.

Alisema kuwa anajua yataibuka maneno kuwa alikimbia pambano, jambo ambalo si kweli, kwani mchezo wa ngumi ni ajira kwake, hivyo hawezi kufanya mchezo wa kufurahisha watu huku yeye akizidi kuumia.

“Waache waongee, lakini ukweli ninao mwenyewe, aliyeumwa na nyoka hata akiguswa na jani lazima mwili wake ushituke,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles