24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MUHONGO AZUIA BEI MPYA YA UMEME

Profesa Sospeter Muhongo
Profesa Sospeter Muhongo

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.

Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa jana na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu alisema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.

“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.

“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.

Katika sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema hakuna ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize matatizo yake kifedha.

“Tanesco kila mwaka inapandisha bei, mbona hawajajikwamua? Mbona madeni yanazidi kuongezeka? Nyingine ni kwamba tunakopa fedha kutoka nje ya nchi na watakaolipa hilo deni ni Watanzania wote, sasa hatuwezi kukopa kulipa madeni ya Tanesco halafu shukrani tutakayoipata ni kupandishiwa bei ya umeme tena.

“Nyingine nenda ufuatilie Tanesco wana matumizi mabaya ya fedha, nimesitisha zoezi lao, sijui kama hizo fedha wamerudisha, unajua wanapeana wale walioko juu bonasi kati ya Sh milioni 40 na milioni 60 kwa mwaka,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema Ewura wanapaswa kupeleka ripoti ijadiliwe, kwani haiwezi kuwa Serikali ndani ya Serikali na haiwezi kupandisha bei bila waziri mwenye dhamana kujua kwa kuwa inapata bajeti kutoka bungeni.

 

MNYIKA APINGA

Kabla ya taarifa hiyo ya Profesa Muhongo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alipinga kitendo cha Ewura kuridhia uamuzi wa ongezeko hilo la bei ya umeme.

Mnyika ambaye ni Mbunge wa Kibamba, alisema uamuzi huo ni mzigo kwa wananchi na uchumi wa nchi na sababu zilizotolewa kuuridhia hazina msingi.

Mbunge huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, alitoa msimamo huo kupitia ujumbe wake alioutuma jana katika mitandao ya kijamii na alimtaka Profesa Muhongo, atengue uamuzi huo.

Aliongeza kwa kusema kuwa iwapo Magufuli na Muhongo hawatatoa kauli atalifikisha suala hilo bungeni kwa hatua zaidi.

 

EWURA

Ewura iliridhia ongezeko la bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 8.5 baada ya kuyafanyia uchambuzi wa kina maombi yaliyowasilishwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa ongezeko hilo la bei ya umeme juzi, Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlamgosi, alisema katika maombi ya awali yaliyowasilishwa Oktoba 4, mwaka jana, Tanesco ilipendekeza gharama za umeme ziongezeke kwa kiwango cha asilimia 18.19 jambo lililokataliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura.

“Itakumbukwa kwamba Aprili, mwaka huu (mwaka jana) baada ya uchambuzi tuliofanya tuliitaka Tanesco kupunguza gharama za umeme na kweli ilishuka kwa asilimia 1.1 na Watanzania tulinufaika na punguzo lile.

“Baada ya uchambuzi ule Oktoba 4, mwaka huu (mwaka jana), Tanesco iliwasilisha andiko lingine ambapo iliomba ongezeko la bei kutoka shilingi 242.20 hadi shilingi 286.28 kwa kila uniti moja ya umeme, ongezeko hilo ni kiasi cha asilimia 18.19,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles