Ukisalitiwa usichukue maamuzi ya kuumiza

0
1245

Na Mwandishi wetu

Je, inapotokea umesalitiwa, nani unatakiwa umfuate?

Mara nyingi nimekuwa nikiona matukio mbalimbali ya kusalitiana baina ya wapendanao. Lakini swali la kujiuliza, je, mpenzi anaposalitiwa na mwenza wake kwa kutoka na mtu mwingine, anapobaini ukweli wa tukio hilo, anatakiwa amfuate yupi? Mpenzi wake? Au anayetoka naye?

Katika hili wengi huwachanganya akili, kutokana na kwamba, wakati huo unakuwa umepagawa kama mtu aliyepigiliwa msumali wa moto ndani ya moyo. 

Kutokana na hilo, ndio maana suala kama hili endapo likitokea, wapenzi hushindwa kuelewa namna ya kuchukua hatua sahihi ya kukabiliana na tatizo husika. Badala yake hushikwa na jazba na kufikia maamuzi mabaya.

Kushindwa kutulia kujua nini cha kufanya husababisha kuchukua hatua ambayo si nzuri inaweza kukushushia heshima kwa jamii, watoto na hata familia kwa ujumla.

Jambo kama hilo likikutokea, likakuumiza moyo na hata kukusababishia hasira kiasi gani, ni lazima kwanza utulie uweze kutafakari njia sahihi ya kuchukua ili kufanikisha kutatua mgogoro huo. 

Vinginevyo kukurupuka kwako kwa kudhani kumfuatilia mtu anayetoka na mwenza wako ni kuwa sahihi, hii inaweza kukusababishia ufikie maamuzi mabaya yatakayosababisha matokeo ya kuumizana au hata kuuwana.

Unapogundua usaliti fanya yafuatayo; Mosi, ni heri umfuatilie mwenzi wako na uweze kuongea naye kinagaubaga kuliko kumfuata yule anayetoka naye. 

Na pili, chukua maamuzi pasipo kuumizana. Mfano, unaweza kuondoka ili kuepusha kugombana na kuwa na hasira pamoja na kujilinda kwa kumpatia nafasi huyo anayedhani anampa usingizi zaidi yako. Nafikiri kufanya hivyo kwa mpenzi anayekupenda kwa dhati ni adhabu tosha ya kumfanya ajutie maovu yake na kujirekebisha mwenendo wa tabia yake. 

Lakini unapochukua maamuzi tofauti yaliyojaa hasira kwa kumfuatilia yule anayetoka na mpenzi wako, hilo litakuwa kosa na utapoteza muda wako. Lakini pia kwa upande mwingine inaweza kusababisha vurugu zaidi na hatimaye kusambaratisha kabisa uhusiano wako.

Kwa hivyo lazima mambo mengine upunguze ushindani. Kwa sababu suala la kupendana katika uhusiano wa kimapenzi si la kulazimishana. Ni jambo la makubaliano ya hiari kwa wote wawili. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here