Uhamiaji: Raia wa nje wafichuliwe uhakiki daftari la wapigakura

0
504

Amina Omari -Tanga

IDARA ya Uhamiaji imewataka wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kutumia nafasi ya uhakiki wa daftari la kudumu la mpigakura kuwafichua raia wa nje waliojiandikisha kinyume cha taratibu.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Mbaraka Batenga wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema Watanzania pekee ndio wanaotakiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu.

Batenga alisema wapo raia wengine wa nje ambao wanapenda kujipenyeza kwenye mchakato kama uchaguzi ili kupata vitambulisho vya kupiga kura isivyo halali.

“Ningependa kuwataka Watanzania watumie nafasi iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwenda kuhakiki majina yao na kama wakibaini raia ambao hawana sifa, watupe taarifa ili tuwashughulikie,” alisema Batenga.

Alisema wanachokitaka Uchaguzi Mkuu ufanyike kwa usalama na amani, kusiwepo na malalamiko ya watu ambao hawana sifa.

“Tunataka Uchaguzi Mkuu upite salama na amani, hasa kwa watu ambao wanastahili kupiga kura na si ambao hawana sifa za kushiriki,” alisema Batenga.

Ofisa Habari Mwandamizi  wa NEC, Zawadi Msalla aliwataka wananchi kutumia fursa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuhakiki taarifa zao.

Alisema uhakiki huo ndiyo sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, hivyo ni vema wananchi wakahakikisha taarifa zao hazina kasoro zozote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here