30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Shahidi aeleza alivyomkuta juu ya dari mshtakiwa dawa za kulevya

Kulwa Mzee -Dar es salaam

SHAHIDI wa nne katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Shamim Mwasha na mumewe, Abdul Nsembo, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Pascal Daudi amedai mshtakiwa Nsembo alikutwa amejificha juu ya dari akiwa kavaa boxer (nguo ya ndani), huku akiwa kifua wazi.

Inspekta Daudi alidai hayo jana wakati akitoa ushahidi upande wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroine kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili Kakula mbele ya Jaji Elinaza Luvanda, shahidi huyo alidai alipata taarifa Aprili 30 mwaka jana kutoka kwa SSP Salmin kwamba kuna kazi ya kufanya usiku.

Alidai alijiandaa saa mbili usiku na ilipofika saa saba usiku, waliondoka ofisini kuelekea Mbezi Beach, Mtaa wa Upendo nyumba namba 9 kwa Abdul Nsembo ambako walifika saa 7:45 usiku.

Inspekta Daudi alidai waliimarisha ulinzi kwenye nyumba hiyo, akamwagiza Inspekta Msaidizi wa Polisi, Brown kumfuata mjumbe Jafari Adinani ambaye naye alikuja na Polisi Jamii, Nasoro Athumani.

“Walipofika tuligonga geti akachungulia mlinzi, tukajitambulisha, mlinzi akasema anafuata funguo kwa mama mwenye nyumba, baada ya dakika 15 walikuja wote, mlinzi akafungua geti.

“Tulimuuliza Shamim mumewe kama yupo, alijibu hayupo na harudi mapema, tulieleza azma yetu, Shamim aliomba ajiridhishe kwa kutupekua na alifanya hivyo kisha akaruhusu tuingie.

“Tuliingia wote akiwemo Shamim, tulipekua sebuleni, sehemu ya kulia chakula, stoo, chumba kilichopo eneo hilo, hatukupata kitu.

“Tulipanda ghorofani tukaona uchafu chini, kuna kipande cha gypsum kinaning’inia na alama za nyayo kwenye vumbi, tulipouliza, Shamim alisema kuna mafundi walikuja asubuhi kurekebisha matenki ya maji,” alidai Inspekta Daudi.

Alidai kuwa aliomba kuonyeshwa njia ya kupanda kwenye matanki, alionyeshwa akapanda kuangalia lakini hakuona kitu akashuka kuendelea na upekuzi katika vyumba vingine.

Inspekta Daudi alidai chumba cha dada wa kazi hawakukuta kitu, walipoingia chumba cha washtakiwa, aliona mazingira kulikuwa na watu wawili walilala kitandani si muda mrefu uliopita.

“Tulizidi kupata wasiwasi, tukarudi tena, Brown akapanda tena darini akiwa na tochi yenye mwanga mkali, mara tukasikia akisema yuko huku juu, akamshusha chini, Nsembo alikuwa kifua wazi, kavaa boxer, ilibidi tuende chumbani kwao akavaa jinzi na t-shirt.

“Tulipekua chumbani tulikuta silaha moja aina ya pistol, vikopo vinne vya unga, hati ya kusafiria na mwenyewe mshtakiwa alienda kutoa simu moja na kadi ya CRDB juu ya dari,” alidai Inspekta Daudi.

Aliendelea kueleza kwamba eneo la chini nje kulikuwa na geti limefungwa, wakaambiwa eneo la kuegesha magari, wakaomba geti lifunguliwe, likafunguliwa wakakuta gari aina ya Land Rover Discover yenye namba za usajili T 817 BQN.

Alidai walipopekua gari walikuta nyuma ya siti kwenye pochi la cover kuna mfuko wa kitambaa mweupe uliowekwa kwenye nailoni angavu, walipofungua huku washtakiwa wakishuhudia walikuta unga.

“Katika gari lingine hatukukuta kitu, tulipomaliza nilijaza hati ya ukamataji mali, nikaingiza vitu vyote, washtakiwa na walioshuhudia walisaini, vitu vyote nilikuwa navyo nikakabidhi Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.

“Hadi tunamaliza upekuzi ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi, tulifika ofisini na saa mbili nilikabidhi vielelezo hivyo kwa Inspekta Johari kwa ajili ya kuvitunza,” alidai shahidi huyo.

Aliomba kutoa kielelezo cha hati ya kukamata mali, lakini wakili wa utetezi, Juma Nasoro na Hajra Mungula walipinga kwa madai kuna makosa ya kisheria, hivyo hakistahili kupokewa.

Wakili Kakula alidai hoja za kupinga hazina msingi, hakuna mahali ambako washtakiwa wanabisha kwamba sio sahihi katika vitu vilivyoorodheshwa.

Akitoa uamuzi, Jaji Luvanda alipokea kielelezo hicho pamoja na gari Land Rover aina ya Discover kama kielelezo.

Washtakiwa walikamatwa Mei mosi mwaka jana Mbezi Beach nyumbani kwa Nsembo wakiwa na dawa zinazosadikika kuwa za kulevya aina ya heroine.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,848FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles