Uhalifu Afrika Kusini unafifisha juhudi za Ramaphosa kuvutia uwekezaji

0
1731

Mwandishi wetu

PAMOJA na sifa ya utajiri wa kiuchumi na rasilimali likichukuliwa kama Taifa lililostawi zaidi kimaendeleo barani Afrika, wengi hufikiria mara mbili mbili kuitembelea Afrika Kusini kitalii, kimasomo au kikazi.

Kundi hilo halihusishi wale vijana wanaozamia nchini humo kwa njia haramu kutafuta maisha wakiishi kigheto gheto na kuchanganyika na wenyeji, ambao hata hivyo mara nyingi huwapokea vibaya kwa mtazamo finyu kwamba ndio wachawi wa maendeleo na ustawi wao binafsi nchini mwao humo.

Hata hivyo, si wahamiaji haramu tu wanaopokewa vibaya na wenyeji bali pia wale waingiao kihalali hasa wenye ngozi nyeusi, huhesabiwa wamo humo kuwapora ajira, ambazo wao wenyewe mara nyingi huzisusa kwa sababu mbalimbali.

Sababu hizo ni kama vile uvivu, rekodi zao chafu kazini, kuchagua kazi, au mmiliki wa kampuni kwa vile wapo kwa sababu za kihistoria hawataki kufanya kazi kwa Wazungu waliopo nchini humo.

Ukiachana na ubaguzi huo wa wenyeji, ambao si makusudio ya makala haya, kuogopwa kwa Taifa hili na wageni kunatokana na kufahamika kwake kama moja mataifa vinara duniani kuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu.

Uhalifu huo ni pamoja na mauaji, mashambulizi, uvunjaji majumba, ubakaji na machafuko mengine ya kihalifu.

Kwa maneno mengine, Afrika Kusini inaongoza barani Afrika kwa vitendo vya mauaji yanayotokana na uhalifu.

Ndiyo maana vitongoji vingi ndani ya taifa hilo katika majimbo na miji mbalimbali ikiwamo Johannesburg, Capetown vina vibao vinavyotahadharisha watu kuwa wanakaribia au wako eneo hatari kwa ubakaji, uuaji, utekaji nyara, uporaji na kadhalika.

Hali na vitendo hivyo, wakati vikiijengea Afrika Kusini taswira mbaya vimechangia kukwamisha ukuaji wa uchumi wa taifa hilo kutokana na watalii kuogopa au kuikimbia kabla hawajamaliza ziara zao baada ya kukumbana au kunusurika na uhalifu.

Mbali ya utalii, uwekezaji wa kigeni unadorora kutokana na hofu kuwa uhalifu unatishia maisha yao au uwekezaji wao huo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizosomwa na Waziri wa Polisi, Bheki Cele, kwa wastani kuna matukio 57 ya mauaji kwa siku.

Kiwango hicho cha mauaji nchini Afrika Kusini, ambacho tayari kiko juu kwa viwango vya dunia, kimeongezeka kwa asilimia saba, na kumlazimu waziri huyu anayehusika na jeshi la polisi kuilinganisha hali hiyo na ‘uwanja wa kivita.

Jeshi la Polisi lilitoa takwimu za uhalifu Jumanne wiki hii zikionyesha kuwa watu 20,336 waliuawa nchini Afrika Kusini kati ya Aprili 2017 na Machi 2018, ikilinganishwa na watu 19,016 waliouawa katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia (yaani Aprili 2016-Machi 2017).

Cele anasema kiwango hicho cha juu cha mauaji “kinakaribiana na uwanja wa kivita – wakati kuna amani na hakuna vita.

Matukio mengi ya mauaji yamehusishwa na vurugu za magenge ya uhalifu katika mkoa wa Cape Magharibi, ambao mji wake mkuu ni Cape Town.

Kamati ya Bunge inasema juhudi za polisi kukabiliana na tatizo hilo hazijakuwa na ufanisi na kwamba makamanda wanapaswa kuimarisha uwapo wa usimamizi wa sheria katika maeneo yenye matukio mengi ya uhalifu.

“Kamwe isitokee tena tukaja hapa kutoa takwimu kama hizo. Haiwezekani Waafrika Kusini wanaishi katika hofu kama hiyo, msongo kama huo na mauaji kama hayo,” anasema Cele.

Matukio ya mauaji yaliongezeka kwa asilimia 6.9 katika mwaka wa kifedha wa 2017-18, ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia, kwa mujibu wa takwimu hizo. Mauaji ya wanawake na watoto yaliongezeka pia.

Ubakaji uliongezeka kwa asilimia 0.5, ambapo matukio 40.035 yalirekodiwa ikilinganishwa na matukio 39,828 ya mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa takwimu hizo za polisi.

Ingawa Afrika Kusini inajulikana kimataifa kwa uhalifu wake wa vurugu, lakini takwimu za kila mwaka zimekuwa zikipingwa mara kwa mara, hususani kuhusu ubakaji.

Ongezeko kwa ujumla ni ongezeko la mara moja kubwa kabisa tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi wa makaburu miaka 24 iliyopita, wachambuzi wa mambo wanasema.

Takwimu hizo zinafifisha juhudi za Rais Cyril Ramaphosa, ambaye aliingia madarakani Februari mwaka jana akiahidi kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Afrika Kusini na kuchochea sekta ya utalii ya nchi hiyo.

Takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la mashambulizi ya kingono kufikia 50,108 kutoka 49,660 mwaka 2016-17. Makosa mengi ya kingono yaliyorekodiwa yalikuwa ya ubakaji.

Hata hivyo, kuna ongezeko la idadi ya majambazi wanaovunja makazi ya watu, wanaokwapua mitaani na uchomaji moto watu au makazi. Kwa wastani kiwango cha uhalifu kilikuwa chini kwa zaidi ya asilimia nne.

Cele, ambaye amekuwa Kamishina wa Taifa wa Polisi tangu Oktoba 2011 wakati aliposimamishwa  kwa tuhuma za ufisadi, alisema Waafrika Kusini wanapokuwa barabarani wanalazimika kuwa waangalifu vinginevyo watatekwa au wawapo nyumbani wanatakiwa kujilinda mapema kwani nyumba au milango huweza kuvunjwa ghafla na kuanza kutembeza unyama kwa familia.

Gareth Newham, mtaalamu wa masuala ya uhalifu katika Chuo cha Masuala ya Usalama mjini Pretoria, alisema kiwango cha mauaji kinatambulika kama kiashiria cha machafuko Afrika Kusini”.

Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema kuna ongezeko la kiwango cha mauaji kipindi cha miaka mitano iliyopita baada ya kuanguka kwa asilimia 55 kipindi cha miaka 17.

Ongezeko hilo wanasema linatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukithiri rushwa katika jeshi la polisi, nyadhifa za juu katika vyombo vya uzingatiaji sheria kuteuliwa kwa kuzingatia uaminifu na viongozi wanasiasa badala ya sifa stahili.

Lingine wanasema ni kuzorota kwa mazingira ya uchumi hali inayosababisha pamoja na mambo mengine ukosefu wa familia, ambao unaenda kuigusa familia au kaya nzima.

Takwimu hizo zilikuja wiki moja baada ya takwimu nyingine rasmi za uchumi kuwashngaza wengi baada ya kufichua kwamba nchi ilikuwa katika mdororo wa uchumi.

Sarafu ilianguka kwa kiwango cha chini, ambacho hakikuwahi kuonekana tangu Ramaphosa aingie madarakani.

Wabashiri wa uchumi wanasema ukuaji wa uchumi ulikuwa chini ya asilimia moja mwaka jana.

Tatizo la ukosefu wa ajira tayari liko juu linazidi kukua na mfumuko wa bei kuumiza bajeti za watu masikini vibaya mno.

Hali ya ukosefu wa usawa na sababu nyingine kuu inayochochea uhalifu wa aina zote nchini Afrika Kusini, tafiti zilizopita zimethibitisha.

Kwa msingi huo, taifa hilo kamwe halitapunguza kiwango cha uhalifu wa aina zote iwapo uchumi hautakua na pengo la ukosefu wa usawa kupunguzwa.

Sababu hizo ikiwamo zinazochangiwa na sababu ya kihistoria ambayo weusi walinyanyaswa na weupe walioshikiliwa uchumi zinalifanya Taifa hilo kuwa tofauti na mengine.

Katika mataifa mengine kuna na yenye hali mbaya mno kiuchumi lakini hazina kiwango cha mauaji yanayotokana na uhalifu cha kutisha kama hicho cha Afrika Kusini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here