Alichokihofia Dk. Benson Bana ndicho kimempata

0
1209

Javius Kaijage

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amefanya maboresho kidogo katika  serikali yake kwa kufanya  uteuzi na kuwabadilisha baadhi ya viongozi katika vituo vyao vya kazi.

Akitangaza uteuzi na utenguzi huo   Septemba 20, 2019, Ikulu jijini Dar es Salaam,  Katibu Mkuu Kiongozi  Balozi Mhandisi John Kijazi, alieleza kuwa Rais amefanya uteuzi na mabadiliko kadhaa ikiwamo Mkuu wa Mkoa, wilaya na mabalozi.

Miongoni mwa mabalozi 12 walioteuliwa na  Rais Magufuli  kuiwakilisha Tanzania katika  nchi mbalimbali, yumo   Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.  Benson Bana.

Jambo la kujiuliza ni je, uteuzi wa Dk. Bana katika nafasi ya ubalozi ambayo kimsingi inahusiana na masuala ya Diplomasia,  unamfaa au ni  wa kumuweka mtegoni msomi huyu aliyebobea katika Sayansi ya Siasa?

Nasema ni nafasi ya kumuweka mtegoni Dk. Bana   kwa maana ya kwamba wakati fulani yeye aliwahi kutilia shaka uteuzi ambao umekuwa ukifanywa na Rais Magufuli  kwa kuwahusisha wahadhiri wengi wa vyuo vikuu katika  nafasi mbalimbali za uongozi  tangu aingie madarakani.

Miongoni mwa hofu ya Dk. Bana dhidi ya wahadhiri wa vyuo vikuu pindi wateuliwapo kushika nafasi mbalimbali serikalini si ukosefu wa kujiamini kwao bali ni pengo linaloachwa katika nafasi zao walizokuwa wakifundisha na kutoa maarifa kwa watu wengine ambao kimsingi wangeweza kufanya kazi katika taasisi mbalimbali.

Katika hofu hii ya kuacha pengo ambayo imewahi kuonyeshwa na Dk. Bana, mtu mwingine anaweza kusema mbona siku hizi kuna wasomi wengi wanaoweza kuendelea kufundisha vyuo vikuu ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita?

Ni kweli siku hizi wapo wasomi wengi hadi wengine wanahangaika kupata ajira, lakini ikumbukwe kuwa kuna suala zima la uzoefu na wengi wa wahadhiri ambao wamekuwa wakiteuliwa na Rais ni wale wenye uzoefu.

Si tu Dk. Bana amekuwa akihofia suala la kuacha pengo, lakini pia amekuwa akitilia shaka juu ya uwezo wa kiutendaji kwa wahadhiri wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali serikali.

‘‘Vile vile, sina hakika kama utendaji bora unatokana na mhadhiri kutoka chuo kikuu kwa sababu na wao wanakwenda kujifunza huko serikalini.  Hii dhana kuwa vyuo vikuu vinakuwa na watendaji bora kuliko kwingine si sahihi kwa sababu unaweza kuwa Profesa lakini usijue kuandika stori, ila mwandishi mwenye uweledi vilevile anaweza kushika nyadhifa,’’ alisema Dk. Bana wakati akihojiwa na chombo fulani cha habari.

Inawezekana hofu ya Dk. Bana dhidi ya wahadhiri wanaoteuliwa ni jukumu lao la asili ya kwamba wasomi hawa wanatakiwa kuendelea kuambukiza  uwezo wao wa maarifa kwa wengine huku wakiendelea kufanya tafiti, kuelekeza, kutoa ushauri na ikibidi kukosoa  hasa pale mambo yanapokwenda kombo,  kuliko kupokea vyeo vya serikali ambavyo mwishowe  huwaziba midomo.

Historia ya muda mfupi inaonyesha kuwa wahadhiri kadhaa kabla ya kupewa nyadhifa walikuwa wazuri katika kukosoa na kuonyesha njia, lakini baada ya kulambishwa sukari ya madaraka wamegeuka makasuku wa kusifia tu.

Hata hivyo, pamoja na wahadhiri kuendelea kuhitajika vyuoni hususan wale wenye uzoefu,  lakini pia hata serikali wanahitajika kwani wakati mwingine si vizuri kuendelea kuongozwa na mambumbumbu au wale wenye uwezo mdogo katika kufikiria, kutafsiri na kutenda.

Hayati Nelson Mandela aliwahi kusema: ‘‘Nilijifunza kuwa ujasiri haikuwa kutokuwapo kwa hofu, ila ni kuishinda hofu hiyo. Mtu shujaa si yule ambaye  hahisi kutokuwa na  hofu bali ni yule mwenye kupigana nayo na hatimaye kuishinda.’’

 Hofu ya Dk. Bana dhidi ya wahadhiri wanaoteuliwa na Rais haikuwa yeye  kukosa ujasiri, bali ni mtazamo na uzoefu wake katika kuendelea  kuwatumia wasomi hawa wenye akili za ziada katika kuzalisha maarifa kwa wengine, lakini hana budi kuelewa kuwa kuteuliwa kwake kuwa balozi kunatokana na Rais kumwamini hivyo, ni wajibu wake kuishinda hofu na kuutumia vyema uhadhiri wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here