28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Ufisadi Katiba Mpya

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam
MCHAKATO wa kupata Katiba Mpya ya nchi unadaiwa kugubikwa na wingu la ufisadi hali iliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuhoji tenda ya uchapwaji wa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa kwa gharama ya Sh bilioni 6.
Hatua hiyo inakuja huku Watanzania wakiwa wanasubiri kupiga kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, ambapo inaelezwa taratibu za manunuzi zilikiukwa kwa baadhi ya kampuni zilizopewa kazi hiyo kuwa na walakini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, taasisi zote za umma zinatakiwa zitangaze zabuni kabla ya kutoa zabuni husika.
Kutokana na sheria hiyo, inaelekeza taarifa za zabuni husika hutangazwa kupitia jarida na tovuti ya PPRA jambo ambalo linadaiwa halikufanywa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa kazi ya uchapaji wa nakala hizo za Katiba Inayopendekezwa ilianza kufanyika tangu Desemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kila nakala ya Katiba Inayopendezwa inachapishwa kwa gharama ya Sh 3,000.
“Kwenye hizo kampuni zilizopewa hiyo kazi, nyingine hata uwepo wake una walakini, hii haikuwa kazi ya dharura kiasi hicho, lakini pia kutoa zabuni ya Sh bilioni 6 za umma kwa kujuana tu bila kufuata taratibu ni jambo la kushangaza,” kilipasha chanzo chetu.
Pamoja na hali hiyo, lakini inaelezwa Wizara ya Katiba na Sheria imeshindwa kutoa kazi hiyo kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali kama ilivyoahidiwa na Serikali mapema mwaka jana.
MTANZANIA ilimtafuta Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PPRA, Mcharo Mrutu, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, ambaye alisema PPRA tayari imeiandikia barua Wizara ya Katiba na Sheria kupata taarifa za kina juu ya taratibu za utangazaji wa zabuni hiyo.
“Tumewaandikia barua Wizara ya Katiba na Sheria ambao ndio waliotoa hiyo kazi, baada ya maelezo yao ya kina ndiyo tunaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo,” alisema Mrutu.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngole, alisema katika kutoa zabuni hiyo sheria na taratibu zote zilifuatwa, na wahusika wote muhimu walijulishwa ikiwamo PPRA na Mpigachapa Mkuu wa Serikali.
“Ninavyofahamu mimi, sheria ya manunuzi na kanuni zake na miongozo ya Serikali kuhusu manunuzi ilifuatwa kikamilifu ikiwamo kumshirikisha Mpigachapa Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mchapaji mkuu wa nyaraka za Serikali,” alisema.
Alipotafutwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, ambaye ofisi yake inadaiwa kutafuta wachapishaji hao, alisema wahusika wakuu katika suala hilo ni Wizara ya Katiba na Sheria na PPRA, kwamba ndio wanaoweza kujibu suala hilo.
“Kama una shaka na suala hili, hatua uliyochukua ni sahihi, watu wa sheria ndio watu sahihi kabisa kwa sababu ndio wanaoshughulikia suala hili na wanaweza kukwambia kama taratibu zilifuatwa ama la,” alisema Chibogoyo.
Alipoambiwa Wizara ya Katiba na Sheria imerusha mpira kwa ofisi yake, Chibogoyo alihoji: “Unaposema Katiba na Sheria unamaanisha nani, kwa maana ya Wizara ya Katiba na Sheria?
“Kama PPRA wamesema wanataka maelezo zaidi, kuna maelezo yatapelekwa huko na watakuwa na cha kusema,” alisema.
Mtanzania: Kwahiyo ofisi yako haina chochote cha kusema?
Chibogoyo: Mimi ninachoweza kukwambia tu ni kwamba umefuata taratibu sahihi kwa watu uliowauliza hili suala, kama kutakuwa na jingine kwa ufafanuzi watatoa.
Mtanzania: Lengo la kutaka kauli yako ni kwa sababu wewe ndiyo mpigachapa mkuu, na hili jukumu ni lako na hizo kampuni tatu umetafuta wewe, ndiyo maana tunataka kauli yako.
Chibogoyo: Haya mambo kama una taarifa ambazo ni muhimu kwa jamii njoo ofisini kwangu, ujieleze pale na mimi naweza kuchangia kitu, nikikukaribishe tu ofisini kwangu kesho.
Chanzo chetu cha habari kilisema baada ya kutolewa kwa kazi hiyo ya kuchapa Katiba Inayopendekezwa kwa kampuni binafsi, nyaraka zinazoenda serikalini husomeka kuwa Serikali imenunua karatasi kwa kampuni hizo, badala ya kusomeka kuwa kazi husika imechapwa na kampuni hizo.
Februari 7, mwaka huu, akiahirisha Bunge mjini Dodoma, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema Serikali itachapisha nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa ambazo zitasambazwa kwa watu mbalimbali nchi nzima.
Alisema hadi sasa tayari nakala 654,024 zimechapishwa na kugawanywa kwenye mikoa 11 nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles