25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simanzi, vilio vyatawala Dar

DSC_0691

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
SIMANZI na vilio vimetawala jana eneo la Kipunguni Ukonga jijini Dar es Salaam nyumbani kwa mhandisi mstaafu wa ndege, marehemu Luteni David Mpira (68), ambaye alifariki pamoja na familia yake ya watu watano baada ya nyumba yao kuungua na moto usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Mpira ambaye enzi za uhai wake alikuwa mwanajeshi, alikutwa na umauti huo saa tisa usiku pamoja na mke wake Celina Mpira (62), mtoto wake Lucas Mpira (37), shemeji yake Samuel Yegera (54) na wajukuu zake Celina Emmanuel (9) na Paulina Emmanuel (6) wakiwa wamelala ndani.
Huzuni na majonzi vilitawala muda wote katika eneo hilo la msiba ambapo ilipotimu saa 7:30 mchana majeneza yaliyokuwa na miili ya marehemu hao iliwasili ikiwa imebebwa katika gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ikitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilipokuwa imehifadhiwa.
Pamoja na makazi hayo kubaki wazi kutokana na nyumba yote kuungua, lakini wakazi wa eneo hilo walikusanyika bila kujali hali hiyo, huku wengine walionekana kukaa nyumba za jirani na eneo la msiba.
Baada ya kuingia kwa miili hiyo, vilio vilizidi huku waombolezaji wengine wakisimama juu ya miti ili kuweza kushuhudia miili hiyo ikishushwa katika eneo hilo kabla ya kuondolewa na kupelekwa katika makaburi ya Airwing yaliyopo Banana kwa mazishi.
Awali kabla ya kuwasili maiti hizo, mama wa watoto wawili, Fatuma Issa, alipoteza fahamu baada ya kulia kwa muda mrefu na baadae kuzinduka.
Msiba huo ambao umeonekana kuvuta hisia za watu, ulilazimisha kusimamishwa kwa shughuli za uzalishaji, zikiwamo biashara kwa wakazi wa eneo hilo ili kuweza kupata fursa ya kushiriki katika mazishi.

Makaburini
Wakati majeneza hayo yalipowasilia katika makaburi ilizingirwa na watu mbalimbali waliohudhuria mazishi.
Katika hali ya kuhuzunisha, wakati majeneza hayo yakiwa makaburini, ilipatikana taarifa ya kuonekana sehemu ya mguu nyumbani kwa marehemu, ambao ulihisiwa ni wa baba wa familia, marehemu Luteni Mpira na kulazimika kuingizwa katika kaburi lake bila kufunguliwa jeneza.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, aliongoza ibada ya mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliyesema msiba huo ni mkubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
“Msiba huu ni mkubwa, kwa niaba ya Serikali na mimi mwenyewe nimekuja kutoa pole, tukio hili limetushtua na kutuhuzunisha wengi, tunaomba Mungu awape nguvu wafiwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Dk. Bilal.
Alisema kuna haja ya wananchi kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kuzimia moto majumbani pamoja na kuwa makini katika ujenzi wa nyumba zao, hasa wanapoweka milango na madirisha ya chuma kuhakikisha yanafunguka kwa urahisi pindi inapotokea dharura.
Awali akizungumza wakati wa sala ya kuwaombea marehemu, Askofu Nzigilwa, aliwakumbusha waumini kutenda matendo mema pamoja na kuwa msiba huo umeleta huzuni na maswali mengi katika mioyo ya binadamu.
“Jambo hili linaleta uchungu na maswali mengi, lakini majibu yote yapo kwa Mungu, tunaomba awapokee ndugu zetu hawa waliomaliza muda wao duniani, hili ni tukio la huzuni kwa watu wa familia moja kuitwa na Mungu kwa wakati mmoja,” alisema Askofu Nzigilwa.
Aliwataka wafiwa kuwa na ujasiri huku wakimtegemea Mungu.
Mbali na Dk. Bilal viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik na Waziri asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni mmoja wa wanafamilia katika msiba huo.
Wengine ni Waziri wa Afrika Mashariki, Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles