25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Uchaguzi mdogo Embakasi Kusini ‘kuipasua’ NASA

ISIJI DOMINIC

MUUNGANO wa vyama vya upinzani, NASA, upo hatarini kumeguka kufuatia cheche za maneno wanazotupiana kuelekea uchaguzi mdogo wa eneo Bunge la Embakasi Kusini.

Tayari Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza Aprili 5, mwaka huu kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge maeneo ya Embakasi Kusini na Ugenya. Hata hivyo, macho ya wananchi wengi yapo katika eneo la Bunge la Embakasi Kusini ambapo vyama viwili vikuu ndani ya NASA; ODM na Wiper, vinapimana ubavu.

Desemba 21, mwaka jana Mahakama ya Juu Zaidi (Supreme Court) ilifuta matokeo yaliyompa Julius Mawathe wa Chama cha Wiper ushindi wa Embakasi Kusini kwa kile walichosema ukosefu wa ushahidi kutetea matokeo ya IEBC yaliidhinisha ushindi wa Mawathe.

Kufutwa matokeo hayo ya Embakasi Kusini kunafuatia malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani na mbunge wa zamani kupitia chama cha ODM, Irshad Sumra.

Uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini na Ugenya ilikuwa fursa pekee ya chama cha Jubilee kujiongezea idadi ya wabunge lakini Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Raphael Tuju, alisema baada ya mashauriano ya viongozi wameamua kutowasilisha majina ya wagombea.

“Hii inatokana na hatua ya kujenga uhusiano na vyama vyingine vikubwa na pia kuonesha uchaguzi si uadui huku tukiwa na matarajio makubwa,” alisema Tuju na kutaka vyama vitakavyogombea kuonesha ukomavu wa siasa katika kuhakikisha wanadumisha amani.

Licha ya chama cha Jubilee kutokuwa na mgombea katika uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini baadhi ya wanachama wa chama hicho wamesema watamuunga mkono Mawathe wa Wiper ambaye anapambana na Sumra wa ODM.

Aidha mgombea wa Wiper anaungwa mkono na chama cha Ford Kenya kinachoongozwa na Moses Wetangula ambacho pia ni chama kinachounda Muungano wa NASA kwa madai kuwa uongozi wa ODM ni wa kibabe na unakosa hekima ya kufanya kazi kama timu. Chama cha Amani National Congress hakina mgombea katika uchaguzi mdogo wa maeneo hayo mawili ya ubunge.

Wiper iliwaomba ODM kutowasilisha mgombea katika uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini na badala yake kuwaunga mkono ili kudumisha ‘handshake’ lakini wamekataa na kuwaambia wajitayarishe kwa mapambano.  

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alipuuza vyama vinavyomuunga mgombea wa Wiper akisema hawana ushawishi katika siasa za Nairobi na kwamba kuungana kwao ni dalili tosha ODM ni chama kikubwa ndani ya Muungano wa NASA na hakiwezi kushindwa na chama kimoja.

“Ni ushawishi gani walionayo Ford Kenya jijini Nairobi ambao wana wajumbe wawili tu wa Baraza la Kaunti?” alihoji Sifuna. “Tumevumilia vyama vingine kwa muda mrefu lakini ODM haitanyamaza tena wakati tunatakiwa kupiga kelele. Tumechoka kulea vyama vyingine kama watoto kila mara. Kama kuna mtu ana tatizo na namna tunavyowasilisha taarifa, basi kuna mengi yanakuja.”

Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu, aliwashutumu ODM kutokuwa wawazi akisema chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kinafurahia wakati mambo yanaenda vizuri upande wao na si kwa vyama vingine ndani ya muungano huo.

“Tutawavaa kaka zetu wakubwa. Kama vyama vingine vinaona eneo hilo la ubunge linastahili kuachiwa Wiper, kwanini ODM wanalazimisha kusimamisha mgombea? alihoji.

Hata ombi la kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, halijapokelewa vizuri na sasa kinachosubiriwa ni kuanza kampeni ambayo itatikisa Muungano wa NASA na mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu 2022.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles