30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Uchaguzi CWT kesho, Takukuru wakiwa mguu sawa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAKATI Uchaguzi Mkuu wa kuwapata viongozi wakuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ukitarajiwa kufanyika kesho Uwanja wa Jamhuri jijini hapa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma imewataka wajumbe wa mkutano huo kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Pia imetoa onyo kwa wagombea kujiepusha na vitendo vya kuwapangia nyumba za wageni, kuwapa vinywaji kuwagharamia usafiri wajumbe wa mkutano huo. 

Wiki hii imekuwa ya hekaheka ambapo  nyumba za wageni jijini hapa zimejaa walimu kutoka sehemu mbalimbali, ambao ni wajumbe wa mkutano huo waliokuja kuwachagua viongozi watakaokiongoza chama hicho nfazi ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema wajumbe wa mkutano huo wanapaswa kuzingatia taratibu za chama chao na sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya rushwa au kuwa katika mazingira ambayo yanaashiria uwepo wa vitendo hivyo.

“Kwa kuwa Takukuru ipo kila kona, tutashughulika na yeyoye ambaye tutapata au tutamhisi ameshiriki, anashiriki au anakusudia kushiriki katika vitendo vya rushwa kuhusiana na uchaguzi huo,” alisema Kibwengo.

Pia aliwataka kujiepusha na ufadhili wa  malazi, chakula, vinywaji na usafiri kama kishawishi kwani wote watoaji na wapokea rushwa wana hatia.

“Nawashauri wapambe wa wagombea wajihadhari na vitendo vya rushwa na kuepuka mazingira yenye viashiria vya rushwa kwani wanaweza kujikuta wanakosa fursa ya kufanya kampeni au hata kutoshiriki uchaguzi, hatutaki tufike huko,” alisema Kibwengo.

Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa wa Dodoma imemfikisha mahakamani muuguzi wa Zahanati ya Chamwino, Zabron Richard (32) baada ya kuomba rushwa ya Sh 100,000 ili amsafishe kizazi mke wa mkazi wa eneo hilo. 

Kibwengo alisema muuguzi huyo alifanikiwa kuchukua Sh 60,000 baada ya kukamilisha kumsafisha mzazi huyo kizazi. 

Alisema kukamatwa kwa muuguzi huyo kumekuja baada ya Mei 11 kupokea taarifa kutoka kwa mkazi wa Chamwino akihitaji huduma ya kusafishwa kizazi, lakini amekataliwa hadi atoe sh 100,000 wakati ni kinyume na sheria. 

“Baada ya tukio hilo, Takukuru iliweka mtego na kumbaini muuguzi huyo na  ilimfikisha mahakamani kutokana na kosa hilo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema Kibwengo.

Vilevile alisema Takukuru mkoani hapa inatarajia kumfikisha mahakamni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamatwa iliyopo wilayani Bahi, Yusuphu Chuma (39)  baada ya kukutwa na makosa manne ya rushwa. 

Kibwengo alisema uchunguzi unaonyesha kwamba Juni 2019 mtuhumiwa alighushi mihutasari miwili ya vikao vya kamati ya shule na mkutano wa walimu kuonyesha kwamba waliridhia kiasi cha Sh 469,500 kitolewe kwenye akaunti ya shule huku akifahamu kwamba ni uongo na aliiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi. 

Katika hatua nyingine, Takukuru imefanikiwa kurejesha mashamba 13 ya wakazi wa Kijiji cha Makole wilayani Kongwa baada ya kutaifishwa kutokana na kuchukua mkopo wa riba kwa Nelson Ndalu. 

Alisema mashamba hayo yenye hekari 30 yalichukuliwa na Ndalu, maarufu kama Osama, anayekopesha kwa riba ya asilimia  100.

Osama alidai kwamba aliwapokonya  mashamba hayo kutokana na kushindwa kulipa fedha alizowakopesha. 

“Baada ya Takukuru Kongwa kufanya uchunguzi, wamebaini hiyo ni tabia ya Osama ya kudhulumu wakazi wa eneo hilo, ambapo Mei 7 ameridhia na kurejesha mashamba hayo,” alisema Kibwengo. 

Pia Takukuru Dodoma imefanikiwa kurejesha kiwanja namba tatu kitalu Q Iyumbu New Town Centre kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma baada ya uchunguzi kubaini kwamba aliyekuwa Mhasibu wa CDA alimwezesha rafiki yake kukipata kwa njia ya udanganyifu. 

“Tumefanyia uchunguzi na kubaini jumla ya Sh milioni 43, yalionekana malipo hayo yalifanyika mwaka  2016 na kukatiwa stakabadhi Januari 2017 wakati malipo ni batili na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles