23.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 20, 2021

Maofisa wanne NEMC mikononi mwa Takukuru

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MAOFISA wanne wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za ubadhirifu.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhususino wa Takukuru, Doreen Kapwani, Dar es Salaam jana, ilisema kuwa taasisi hiyo inawashikilia watumishi hao kwa tuhuma mbalimbali zinazochunguzwa, ikiwamo makosa ya rushwa.

“Tunapenda kuuthibitishia umma kwamba ni kweli Takukuru Makao Makuu inawashilikia watumishi wanne wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa tuhuma mbalimbali zinazochunguzwa na taasisi hii, ikiwemo makosa ya rushwa,” alisema Kapwani.

Aliwataja watumishi hao ambao wote wanashikiliwa katika ofisi za Takukuru zilizopo Upanga, Dar es Salaam kuwa ni pamoja na Deusdedith Katwale ambaye ni Ofisa Mazingira NEMC Makao Makuu.

“Wengine ni Ofisa Mazingira NEMC Makao Makuu, Magori Matiku, Ofisa Mazingira NEMC Makao Makuu, Obadia Machupa pamoja na Lydia Laurent Nyinondi ambaye ni Mhasibu Msaidizi NEMC Makao Makuu,” alisema Kapwani.

Alisema watuhumiwa hao wote wamekuwa wakichunguzwa katika makosa mbalimbali yakiwamo yale ambayo uchunguzi wake umekamilika.

“Miongoni mwa makosa hayo ni kula njama kutenda kosa, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuisababishia mamlaka hasara, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.

“Tunapenda kuujulisha umma pia kwamba Takukuru kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inatarajia kuwafikisha watuhumiwa hawa mahakamani kesho (leo) Juni 4, 2020,” alisema Kapwani.

Aidha, katika hatua nyingine, Takukuru Makao Makuu inamshikilia Eliud Kijalo ambaye ni ofisa katika Wizara ya Maliasili na Utalii kwa makosa ya ubadhirifu wa fedha zaidi ya Sh bilioni nne. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,961FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles