Uandikishaji uchaguzi serikali za Mitaa waanza

0
754

waandishi wetu-Dar/mikoani

UANDIKISHAJI wapigakura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeanza, huku baadhi ya maeneo watu wakijitokeza wachache.

MTANZANIA ilitembelea katika vituo mbalimbali vya kujiandikisha Dar es Salaam na kukuta idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza, sababu ikitajwa kuwa ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Katika kituo cha Uzuri, Kata ya Manzese, Manispaa ya Ubungo walikutwa waandikishaji wakiwa na mawakala, huku kukiwa hakuna hata mtu mmoja aliyekuwapo kujiandikisha.

Mmoja wa waandikishaji katika kituo hicho ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini kwa sababu si msemaji wa Manispaa, aliliambia gazeti hili kuwa uandikishaji umekuwa wa kusuasua kwa sababu ya wananchi wengi kuogopa kujitokeza kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha.

“Hali ya hewa mbaya, ndiyo maana watu wameshindwa kujitokeza kwa wingi katika siku hii ya kwanza,” alisema.

Katika Kituo cha Ofisi ya Kata kilichopo Mtaa wa Kimamba, Kata ya Makurumla, wananchi walionekana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kimamba, Omary Suleyman, alisema wamekuwa wakifanya mikutano mbalimbali kuhamasisha wanachama na wananchi kwa jumla kuhusu faida ya kujiandikisha.

 “Tumezunguka kwenye mashina yote ya mtaa wetu kuwahamasisha kuhusu uandikishaji na wametusikia, ndiyo maana wanajitokeza kwa wingi,” alisema Suleyman.

DODOMA

Dodoma mjini watu wengi wamejitokeza kujiandikisha, huku mawakala wakiwa ni wa vyama viwili tu, CCM na Chadema.

MTANZANIA ilitembelea baadhi ya vituo vya Kisasa Sekondari na Msingi, Njedegwa West, Genge 21 na Shule ya Msingi Makulu, vilivyopo Kata ya Dodoma Makulu, Kisabuje na Nkuhungu West vilivyopo Kata ya Nkuhungu na Chang’ombe Shule ya Msingi na kujionea watu wengi wakiwa wamejitokeza.

Katika kituo cha Shule ya Msingi Dodoma Makulu, watu 203 walikuwa wamejitokeza mpaka majira ya saa 3.20 alaasiri kujiandikisha. Mtaa una wakazi 400.

Akizungumza na MTANZANIA, msimamizi msaidizi wa kituo hicho ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Msangalalee Magharibi, Getruda Katiega, alisema watu wengi wamejitokeza huku idadi kubwa ikiwa ni vijana.

Alisema mawakala waliojitokeza katika kituo hicho ni wa vyama viwili vya Chadema na CCM pekee.

Pia MTANZANIA ilitembelea Kituo cha Tawfiq, Kata ya Viwandani ambako hadi saa 8.30 mchana watu 63 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura kwenye mtaa huo wenye watu zaidi ya 400.

TANGA

 Katika Mkoa wa Tanga, MTANZANIA lilipita baadhi ya vituo ambavyo vinaandikisha wananchi na kukuta idadi ndogo ya watu waliojitokeza.

Vituo ambavyo gazeti hili liliweza kutembelea ni Msambweni namba moja na namba mbili, Kata ya Msambweni na Muungano B Kata ya Ngamiani Kusini Tanga Mjini ambako idadi ya wananchi ilikuwa ndogo, huku wengine wakieleza kutokana na mvua na wengine wakieleza kwamba ni taarifa kutokutolewa kwa wananchi kwa wakati.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Mtaa wa Madina, Kata ya Msambweni jijini Tanga, Zuhura Mwadawa alisema mwamko bado si nzuri kutokana na taarifa kutokufika kwa wakati kwa wananchi.

Zuhura alisema ni desturi kwamba wengi wanapotangaziwa ndio mwamko unakuwa mkubwa.

Alisema kama matangazo yamefanyika basi ni baadhi ya maeneo jambo ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa uandikishaji kwa siku ya jana huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha.

 “Lakini pia hata mawakala wa vyama hawakuwa wazi, kutokuwekwa wazi siku ya kuapishwa kwao… kubwa ambalo tunasisitiza ni wananchi kujitokeza kujiandikisha,” alisema.

 Mbunge wa Tanga Mjini, Alhaji Mussa Mbaruku (CUF), aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha huku akivitaka vyombo vya habari viendelee kuhamasisha wajitokeze kwa wingi.

Pia aliwataka mawakala wa vyama waachwe watimize wajibu wao kuhakikisha wanaoandikishwa ni wakazi halali wa mitaa husika ili uchaguzi huu usiwe na rabsha na wapigakura waweze kutekeleza wajibu wao.

MTWARA

Katika Mkoa wa Mtwara zaidi ya wananchi 76,000 wa Manispaa ya Mikindani wanatarajia kujiandikisha.

Akizungumza wakati wa kuzindua daftari la uandikishaji wapigakura, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema hatua hiyo ni muhimu ili kupata  viongozi watakaotuletea maendeleo.

Alisema hadi sasa Manispaa ya Mtwara Mikindani inatarajia kuandikisha zaidi ya wananchi 76,000 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

“Lazima wananchi wajue kuwa daftari hili si lile la kudumu la kupigia kura hili ni maalumu kwa ajili ya Serikali za mitaa.

“Mpiga kura lazima awe Mtanzania na lazima awe mkazi wa mtaa husika ili apate haki ya kupiga kura.

“Kila mmoja awe balozi wa kuwakumbusha wengine ili wananchi wajitokeze kwa wingi zaidi.

“Mabadiliko tunayotaka katika nchini yetu yanaanzia kwenye uchaguzi kujiandikisha na kuchagua kiongozi anayefaa kwa maendeleo ya mkoa wilaya na nchi yetu,” alisema Byakanwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda, alisema kuwa uchaguzi huo ni muhimu kwa kila mwananchi kujitokeza ili kuweza kutimiza haki yake ya kupiga kura.  

“Uzinduzi wa daftari la kupigia kura wananchi wanapaswa wahamasishwe kushiriki.

“Uchaguzi huu unamgusa mwananchi moja kwa moja ndiyo maana tunahamasisha kuwa lazima uangalie mtu mwenye sifa na mweye maadili ndio umchague kuwa kiongozi,” alisema Mmanda.

Naye mwenyekiti wa Mtaa wa Ligula Kati, alisema kuwa baada ya uzinduzi tayari uandikishaji umeanza katika ngazi ya mitaa ambako hata hivyo bado mwitiko sio mzuri kutokana na wengi wao kuwa makazini hali ambayo inaonyesha kuwa jioni inaweza kubadilika.

“Katika mtaa huu tunarajia kuandikisha wananchi zaidi ya 540 ambao tunaamini kuwa endapo tukihamasisha tunaweza kuwapata zaidi ya hao na mimi nimejitolea kuhamasisha kwa kuwapitia majumbani na kuwatangazia kupitia kipaza sauti ili kupata wengi zaidi,” alisema Sudi.

ACT WAZALENDO WAZUNGUMZA

Chama cha ACT Wazalendo kimeibuka na kuiomba Serikali kuondoa changamoto kadhaa zilizojitokeza wakati wa uandikishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mratibu Mawasiliano wa uchaguzi huo mwaka huu wa chama hicho, Mbarala Maharagande, alisema  uandikishaji huo ni muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo ni vema demokrasia ikatumika ili kukamilisha kwa amani na usawa.

Alisema ikiwa ni siku moja tu, chama hicho kimefanya utafiti mdogo na kubaini changamoto kadhaa ikiwamo  vituo vya Toangoma na Charambe kuhamishwa maeneo ya awali yaliyokubaliwa viwepo bila taarifa.

“Changamoto nyingine tuliyoiona ni mawakala kukaa mbali mita saba na waandikishaji, pia mawakala kukataliwa kuandika majina ya waliojiandikisha, hii inaweza kusababisha kuvuruga shughuli hii muhimu,” alisema Maharagande.

Alisema katika Kata ya Tandale yenye mitaa sita kimewekwa kituo kimoja, hivyo inaweza kusababisha msongamano ambao utawafanya wengine wakose fursa ya kujiandikisha.

“Tumebaini ukosefu wa wino kwa wasiojua kuandika ambao wanatakiwa kuweka alama ya dole, ni muhimu hili likafanyiwa utararibu kwa haraka ili kuwapa fursa wananchi wote kujiandikisha kwani ni haki yao ya msingi,” alisema Maharagande.

Pia alisema mvua zilizonyesha zimesababisha wananchi wengi kushindwa kufika vituoni, hivyo ni muhimu siku zikaongezwa ili wengi wajiandikishe.

Wakati huohuo, chama hicho kimewaomba wananchi na wenye mapenzi mema kukiunga mkono kwa kukiwezesha kumudu gharama za kampeni za uchaguzi huo ambao una umuhimu ndani ya jamii.

Habari hii imeandaliwa na CHRISTINA GAULUHANGA, TUNU NASSOR (DAR ES SALAAM), Ramadhani Hassani (DODOMA), FLORENCE SANAWA (MTWARA) na OSCAR ASSENGA (TANGA)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here