27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI yafanya matibabu kwa wagonjwa 28,800 ndani ya miezi mitatu

waandishi wetu

WAGONJWA 28,876 wenye matatizo ya moyo wametibiwa kati ya Julai na Septemba mwaka huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo, Dk. Peter Kisenge, wakati akieleza taarifa ya kazi zilizofanywa na kurugenzi yake katika kikao cha menejimenti kilichofanyika jana.

Dk. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema wagonjwa waliotibiwa katika taasisi hiyo wanaume walikuwa 12,566 na wanawake 16,310, huku 6,590 sawa na asilimia 22.8 walikuwa wagonjwa wapya.

“Tumeona wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi za Ethiopia, Malawi, Zimbabwe, Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Wagonjwa waliotibiwa na kurudi nyumbani walikuwa 27,882 na wagonjwa 994 walilazwa, kati ya hao 500 ni wanawake na 494 ni wanaume. Idadi ya vifo ilikuwa ni asilimia 6,” alisema Dk. Kisenge.

Alisema watoto waliotibiwa katika taasisi hiyo walikuwa 1,516 ambao wasichana walikuwa 800 na wavulana 716, huku 374 walikuwa wagonjwa wapya.

 “Wagonjwa wengi tuliowaona walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo, valvu, matundu, mishipa ya damu ya moyo na magonjwa ya moyo ya kuambukizwa yanayosababisha makovu katika  valvu za moyo kutokana na kupata mafindofindo kwenye tezi za koo,” alisema Dk. Kisenge.

Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo pamoja na kuwekewa vifaa vinavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri  walikuwa 352, kati ya hao watoto ni 87 sawa na asilimia 24.7 na hakukuwa na mgonjwa aliyepoteza maisha.

Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji Dk. Anjela Muhozya, alisema wamefanya upasuaji kwa wagonjwa 153, kati ya hawa 122 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua, 23 walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya damu na nane walifanyiwa upasuaji wa mapafu.

“Tumefanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao valvu zao zilikuwa na shida, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo na kupandikiza mishipa ya damu ya moyo. Wagonjwa waliopoteza maisha ni watatu sawa na asilimia 2.5,” alisema Dk. Anjela.

Alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika matibabu ya wagonjwa wa moyo ni wengi kufika katika taasisi hiyo huku mioyo yao ikiwa imechoka.

Aliwaomba watu kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kama wana matatizo ya moyo au la na kama watakuwa nayo waweze kupata matibabu kwa wakati.

Naye Cecilia Nthala kutoka nchini Malawi, ambaye mtoto wake anatibiwa katika taasisi hiyo, alishukuru kwa huduma ya matibabu ya moyo aliyoipata.

“Nilipata taarifa ya taasisi hii kupitia tovuti na mitandao ya kijamii, kwa kuwa mtoto wangu ana matatizo ya moyo, nikawa nafuatilia kwa ukaribu huduma mbalimbali  wanazozitoa, baada ya kuridhika nazo nikaamua kumleta mwanangu ili naye apate huduma ya matibabu.

 “Kwa kipekee ninawashukuru wauguzi na madaktari kwani muda wote wako karibu na mimi, najiona kama vile niko nchini kwetu Malawi. Ninawaomba muendelee kutoa huduma kama hii mliyoitoa kwangu kwa wagonjwa wengine mnaowatibu,” alishukuru Cecilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles