24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Uamuzi ni wako kuchagua kipato au Corona’

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Tanzania inaendelea na utoaji wa chanjo ya virusi vya Corona kwenye maeneo mbalimbali nchini tangu kuzinduliwa kwa mpango huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Ni katikati ya mpango huo ndipo linapenya agizo la kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma, hususan jijini Dar es Salaam.Agizo hilo;linamtaka  kila abiria kunavaa barakoa awapo kwenye vyombo vya usafiri wa umma.

Rais Samia Suluhu Hassan akichomwa chanjo ya corona Agosti 2.

Aidha, agizo hilo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, halikuishia hapo, bali lilienda mbali zaidi kwa kuwahimiza wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kuhakikisha wanabeba abiria waliokaa kwenye viti kwa maana ya ‘Level Seat’.

Awali, ni kweli uamuzi huo ulianza kutekelezwa na baadhi ya makondakta wa daladala zinazofanya safari zake katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam.

Lakini, kwa sasa mambo yamekuwa tofauti. Si kondakta wala dereva anayejali tena juu ya abiria kutovaa barakoa.

Shida iko wapi?

Makondakta wanasema hawana furaha tena na mpango huo kwani ni kama umekuja kupunguza riziki waliyokuwa wakiipata kwa sababu idadi ya abiria imepungua.

Abdalla Hussein au maarufu kwa jina la ‘Dulla’ ni dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya kituo cha usafiri cha Mawasiliano na Masaki jijini Dar es Salaam.

Dulla anasema kwa sasa kila kitu ni kama kimebadilika kwani mfumo wao wa mapato siyo kama ule wa awali.

Kwa mujibu wa Dulla, awali yeye na kondakta wake anayemtaja kwa jina la Ramadhani Juma, walikuwa na uwezo wa kufanya safari tisa hadi 10 lakini sasa wanalazimika kuishia sita hadi saba tu.

“Lakini kwa mimi wa Masaki nakiri kabisa kwamba suala hili la Corona limetuathiri pakubwa kwani naona kama ofisi nyingi zimefungwa na baadhi zikipunguza wafanyakazi, na wale wanaobaki basi ni wale wanaokwenda na magari yao.

“Hivyo, hata abiria wale tuliokuwa na uhakika wa kuwachukua kila siku kwa sasa hawapo, ila tunajua ni sababu ya Corona. Kwa sababu siwezi kuamini kwamba hawa wote wamenunua magari,” anasema Dulla.

Kipato kimeshuka

Wakati Dulla akigusia kusuasua huko kwa abiria, upande wake Rama anakazia kwa kusema kuwa hata kipato chao kimepungua.

“… Ngoja nikupe mfano ndugu yangu, zamani ulikuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa siku ukapata hata posho ya Sh 50,000, hii ina maana kwamba mlikuwa na uwezo wa kila mmoja kurudi nyumbani na Sh 25,000, siku imekubali mnapata hadi Sh 60,000.

“Lakini sasa hivi utakimbia mnaambulia Sh 25,000 tu, ambayo mtagawana kila mmoja Sh 12,500 wakati mwingine mnatoka na 10,000 hadi 6,000. Hivyo kwa kweli mambo yamebadilika sana. Ukweli ni kwamba mambo yemebadilika na baadhi ya wale tunaofanya nao safari za Masaki wameamua kupaki magari yao,” anasema Rama.

Mambo ni tofauti Posta

Wakati hao wa Mawasiliano-Masaki wakilalamika juu ya kukosekana kwa abiria kutokana na janga hilo la Corona, hali ni tofauti kwa upande wa wenzao wanaofanya safari za Makumbusho-Posta.

Kwa upande wao, wako makini katika kuhakikisha kila abiria anayepanda kwenye daladala zao anakuwa amevaa barakoa, huku wengine wakienda mbali kwa kuwasafisha mikono na vipukuswa ‘Sanitizer’.

Hassan Rashid ambaye ni Kondakta wa moja ya daladala zinazofanya safari za Makumbusho-Posta anasema wamelazimika kuhimiza suala la uvaaji wa barakoa kwa abiria wao ili kuhakikisha wanawakinga na wao pia kujikinga.

“Tunafanya hivyo ili kuhakikisha abiria wanaopanda wanakuwa salama wakati wote kwani barakoa inakugharimu Sh 1,000 lakini matibabu utatumia mara mia ya hiyo fedha iwapo utaleta uzembe.

“Hivyo, tunawahimiza abiria wetu kufanya hivyo, pamoja na kwamba kuna upungufu wa kipato tunaoupata kutokana na kubeba abiria walioketi kwenye kiti tu, lakini usalama ni muhimu kuliko fedha. Tunashukuru kwamba wengi wa abiria wanazingatia utaratibu huu,” anasema Rashid.

Kwa upande wake, Dereva Yusuf Masoud anasema haoni busara kulipa faini ya Sh 30,000 kwa sababu tu ya kujaza abiria wasiovaa barakoa.

“Hebu niambie, nikijaza huku ndani ukasimama, mwisho wa siku ukapata Corona mimi nitapata faida gani, jambo la msingi tunashukuru Mungu kwamba hata matajiri wetu nao wametuelewa sababu tayari walishakutana na Mkuu wa Mkoa akawapa maelekezo kuhusu vyombo vyao kubeba abiria walioketi tu,” anasema Masoud.

Beatrice Bruno ni mkazi wa Makumbusho ambaye anaamini utaratibu huo unapaswa kuigwa na makondakta wengine kwani unawasaidia abiria kuwa salama zaidi na mlipuko wa virusi vya Corona.

“Unajua kaka yangu, usalama wa afya yako ni jambo la msingi sana, hivyo pamoja na kwamba kuna baadhi ya abiria wanaopuuza utaratibu huu wa kuvaa barakoa lakini tunashukuru kwamba baadhi ya makondakta wanawakumbusha, huu ni utaratibu wa kuigwa kwa kweli,” anasisitiza Beatrice.

TAKWIMU ZA CHANJO NCHINI

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waizara ya Afya jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo kwa hiari iliyoanza kutolewa hivi karibuni katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.

Katika taarifa kwa Umma Agosti 15, juu ya maendeleo ya utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kwa Wanananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia kwa Katibu Mkuu (Afya), Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa:

Tathimini ya zoezi la utoaji chanjo tangu Mikoa yote izindue tarehe 04/08/2021, inaonesha mpaka kufikia tarehe 14.08.2021, jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo hiyo kwa hiari.

Ambapo amebainisha kuwa, kati ya hao waliopatiwa chanjo hiyo, walengwa 121,002 ni wanaume ambao ni asilimia 58 (58.3%) na Wanawake ni 86,389 sawa na asilimia 41 (41.7%).

“Natoa maelekezo kwa watoa huduma wote, kutumia dakika chache kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa kila mteja atakaye mhudumiwa kwa magonjwa mengine ili kumpa nafasi ya uelewa na baadae yeye kuchukua maamuzi sahihi juu ya chanjo katika vituo vyote na Hospitali.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe, akigawa barakoa kwa abiria baada ya kuwapa elimu ya kujikinga na Corona.

“Aidha pasiwepo na sababu yoyote ya Wananchi waliofika vituoni kukosa au kukataliwa kupata huduma ya chanjo” alibainisha kwenye taarifa yake hiyo kwa Umma.

Aidha, aliongeza kuwa, Serikali inaendelea kuratibu utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 (COVID-19) kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa hapa nchini.

Hadi kufikia tarehe 14.08.2021 jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo ya UVIKO-19 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 na chanjo imekuwa ikitolewa katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.

Katika taarifa hiyo pia amepongeza mamlaka za Mikoa, Wilaya na Mitaa kwa kuhamasisha zoezi la chanjo, ambapo ameomba pawepo pia na juhudi zaidi za kuongeza kasi katika maeneo ya pembezoni ya miji, mitaa na vijijni.

“Aidha nawaasa Wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19 kwa kunawa mikono na maji tiririka/kutumia vipukusi, kuvaa barakoa katika maeneo hatarishi, kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima na kufanya mazoezi kila mara”. Alimalizia Prof. Makubi katika taarifa yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles