31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Tumieni fursa ya mindombinu bora kujinufaisha kiuchumi-Serikali

Na Clara Matimo, Mwanza

Serikali imebainisha kuwa inapoendelea kuboresha miundombinu mbalimbali katika sekta ya uchukuzi nchini itahakikisha wawekezaji wazawa wananufaika ili wainue uchumi wao, familia zao na Taifa kwa jumla.

Hayo yamebainishwa jijini Mwanza leo Machi 5, 2024 na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alipokuwa akifungua Kongamano la siku mbili la Uwekezaji na Biashara katika miradi ya Reli ya Kisasa(SGR) lililoratibiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Amesema Serikali inatekeleza miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo uchukuzi ili kuwanufaisha wananchi wake ndiyo maana ilitunga sheria mpya ya uwekezaji namba 10 ya mwaka 2022 ili kutoa ahueni kwa wawekezaji wazawa ambayo imepunguza kiwango cha kujiandikisha katika kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuweza kufanya biashara kutoka Sh milioni 200 hadi Sh milioni 100.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akifungua kongamano la uwekezaji wa biashara katika sekta ya usafirishaji upande wa reli lililoandaliwa na TRC.

“Nawasihi sana Watanzania wenzangu watangaze na kulinda miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa gharama kubwa ndani ya nchi yetu kwani inatunufaisha sana, sekta ya uchukuzi kwa miaka mitano imechangia pato la taifa kutoka asilimia sita hadi 16,” ameeleza Kihenzile na kuongeza,” amesema Kihenzile na kuongeza kuwa:

“Mheshimiwa Rais  wetu Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anadhamira ya dhati ya kuinua uchumi wa watanzania na taifa lake alipoapishwa mwaka 2021 alikuta vipande viwili vya  ujenzi wa reli  hivi sasa tuna vipande saba na vipande sita viliishapata fedha na kuanza utekelezaji, viwili vimeishakamilika  siku chache zilizopita tumeanza majaribio kutoka Dar es Salaam  hadi Morogoro,” amesema. 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CPA Amos Makalla akizungumza kwenye kongamano hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CPA Amos Makalla aliwaasa wawekezaji kuiona fursa ya bandari kavu inayojengwa wilayani Misungwi mkoani humo pamoja na daraja la Kigongo Busisi ambalo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 85.

“Hivi karibuni tutazindua Mpango Mkakati wa kuendeleza Utalii katika Mkoa wa Mwanza,  naamini ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege lenye hadhi ya kimataifa pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa inayotumia umeme(SGR) kutoka Isaka hadi Mwanza ambao umefikia asilimia 35 vikikamilika na bandari ikiboreshwa mizigo mingi itasafirishwa hivyo kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Makalla.

Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kongamano hilo linakwenda kutekeleza maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya uchukuzi nchini kwani limelenga kujadiliana na kuzungumza na wadau na wawekezaji wa sekta ya usafirishaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kina ili kuainisha fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa akieleza lengo la kongamano hilo kwa washiriki( hawapo pichani).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori na Usafirishaji Tanzania (TATOA), Elias Lukumay amesema wako tayari kuendelea kutangaza maeneo ya kimkakati yatakayokuza biashara pembezoni mwa reli.

“Kwani tunaelewa kuwa biashara kubwa ya reli ni mizigo hivyo ni lazima tuwekeze kwenye maeneo tengefu kwa kujenga miradi mbalimbali ikiwemo  viwanda vikubwa na kuvutia kwenye maeneo ya kitalii na kadhalika,” amesema Lukumay.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori na Usafirishaji Tanzania(TATOA), Elias Lukumay akizungumza kwenye kongamano hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Sekta binafsi Tanzania(TPSF), Raphael Maganga.

Aidha, Lukumay ameipongeza Wizara ya Uchukuzi kupitia TRC kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza majukumu yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles