23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TUKIO LA MAMA ALIYEJIFUNGULIA NJE LACHUKUA SURA MPYA

 


NA WAANDISHI WETU- Dar es Salaam

Tukio la mkazi wa Wazo Wilaya Kindondoni  Dar es Salaam, Sonia Daudi, kujifungulia nje ya mlango wa Zahanati ya Madale, limechukua sura mpya baada ya mtu anayehisiwa kusambaza video za tukio hilo kudai kutishwa.

Akizungumza na Mtanzania jana, David Costantine alisema juzi asubuhi aliitwa na mmoja wa viongozi wa kata hiyo (jina tunalo) na kumtishia.

Alisema kiongozi huyo alimweleza kuwa alikuwa akimwona kuwa ni mtu mzuri lakini kutokana na kitendo alichokifanya hana maana yoyote tena.

“Aliniambia jana asubuhi (juzi) baada ya kuniita ofisini kwake kuwa alipokuwa ananiona   aliamini ni mtu wa maana, ila aliniuliza ni kitu gani kilichofanya nipige picha dispensary (zahanati),” alisema Costantine.

Costantine alisema ameamua kuripoti suala hilo katika Kituo cha Polisi cha Madale kwa kuhofia usalama wake.

“Nimeamua kuliripoti tukio hili polisi…unajua watu wameshasimamishwa kazi na yeye analeta jazba na vitisho, nimejiona sina usalama,” alisema Costantine.

MTANZANIA lilishuhudia nakala ya wito huo wa polisi ulioandikwa jana ukimtaka mtuhumiwa kufika kituoni hapo leo saa 2.00.

“Zingatia kuwa kukataa au kushindwa kufika kituoni bila sababu za msingi ni kosa sheria.

“Hatua kali za sheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yako ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwa kosa la kutotii amri halali,” ilisomeka sehemu ya wito huo.

Mwenyekiti wa Seriali ya Mtaa wa Madale Kata ya Wazo Wilaya ya Kinondoni, Gration Mbelwa, alithibitisha kupokea taaraifa za tukio hilo.

Alisema uamuzi uliochukuliwa na kijana huyo wa kwenda polisi ni sahihi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro, alisema kazi ya polisi ni kuchunguza jambo lolote linaloripotiwa hivyo kama mlalamikaji ameripoti litafanyiwa kazi.

“Jambo lolote linaloripotiwa katika kituo cha polisi jukumu la ofisa wa polisi ni kuchunguza kuona kama ni la kweli au siyo la kweli ili hatua nyingine za sheria ziweze kuchukuliwa.

“Kwa hiyo kama ameripoti si suala la ajabu kwa polisi kuchunguza, kama anasema hajaripoti basi mimi siwezi kuzungumzia,” alisema Muliro.

*Imeandaliwa na Angelina Kiduko (SJMC), Magreth Msangi (Tudarco) na Leonard Mang’oha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles