22.8 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

TRA yafungua kituo cha huduma kwa walipakodi Mji wa lamadi

Na Derick Milton, Lamadi

Katika kuhakikisha inasogezea huduma zake karibu na wananchi, Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu imefungua kituo cha huduma kwa walipakodi katika mji wa kibiashara Lamadi ambacho kitahudumia wananchi wa Wilaya nzima ya Busega.

Akuzingumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo hicho leo Juni 12, 2021 katika mji huo, Meneja wa TRA Mkoa Charles Mkumbwa amesema awali wananchi na wafanyabiashara wa Wilaya hiyo walisafiri zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za TRA makao makuu ya Mkoa mjini Bariadi.

Mkubwa amesema kuwa mbali na wananchi kupata shida hiyo, hata mamlaka hiyo ililazimika kuweka vituo vya muda hasa kipindi cha ulipaji kodi na ukadiliwaji wa wafanyabishara katika miji ya Lamadi, Nyamikoma na Nyashimo Wilayani humo.

Anasema adha hiyo iliwasababishia wafanyabishara kutumia muda mwingi kutafuta huduma, lakini pia TRA kushindwa kufanya shughuli zake kwa ufanisi kutokana na kutokuwa na kituo cha kutolea huduma.

“Tumeamua kuweka ofisi hizi hapa Lamadi kutokana na Wilaya hii ya Busega asilimia 70 ya wafanyabiashara wake ambao wanalipa kodi TRA wanatoka hapa Lamadi, na kituo hiki kitahudumia Wilaya nzima,” amesema Mkumbwa.

Meneja huyo amesema kuwa kupitia ofisi hizo, TRA imeweka watoa huduma wa kutosha ikiwemo kuletwa meneja wa Wilaya, ambapo alibainisha kuwa huduma zote za kikodi na utolewaji wa leseni za udereva vitapatikana kwenye kituo hicho.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Wilayani humo Davis Mateko amesema kuwa wafanyabishara Wilayani humo wamekuwa wakiangaika sana tangu kuanzisha kwa Wilaya hiyo mwaka 2012 kufuata huduma za TRA.

“Leo tuna furaha kubwa sana kuletewa huduma hii karibu, tumeangaika sana, na tumeteseka kwa kiwango kikubwa kwanza kuletewa huduma hii, lakini pili kutafuta huduma, watu tumesafiri kwenda Bariadi au Magu Mkoani Mwanza,” amesema Mateko.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa wafanyabishara Mkoa, John Sabu aliwataka wafanyabishara mkoani humo kuacha tabia ya kukwepa kodi kwa kuwakimbia maafisa wa TRA na badala yake wawaone kama ndugu.

“Tukilipa kodi ndiyo tunaona maendeleo yanapatikana, tunaona barabara zinajengwa, zahanati kila kijiji, huduma za kijamii kwa wananchi zinaatikana ikiwemo elimu bila ya malipo, hivyo tuwe wazalendo kwa kulipa kodi,” amesema Sabu.

Kabla ya kuzindua kituo hicho, Mkuu wa Wilaya hiyo Tano Mwera ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wafanyabishara kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwani kufanya hivyo ndiyo maendeleo ya nchi yanapatikana.

“Tumepata huduma karibu..tuwashukuru sana TRA kwa hatua hii, ni wajibu wetu kama wafanyabishara kutimiza wajibu wetu kama walipa kodi, tusikwepe kodi, twende tukalipe kwa mujibu wa sheria,” amesema Mwera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles